Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Mujibur Rahman, Mwakilishi wa Bunge la Bangladesh, ambaye alisafiri kwenda Iran kushiriki katika hafla ya kihistoria ya kumuaga Kiongozi Shahidi, akisisitiza uhusiano wa kina kati ya mataifa ya Iran na Bangladesh, alisema kuwa; ushiriki wa ujumbe wa bunge la nchi yake katika mazishi na kumbukumbu ya Ayatullah Khamenei ni ishara ya mshikamano wa Umma wa Kiislamu.
Alisema: “Waislamu ni kama mwili mmoja, na maumivu au msiba unaoupata upande wowote wa Umma wa Kiislamu unapaswa kuwa jambo linalowahusu Waislamu wote.”
Mwakilishi huyo wa Bunge la Bangladesh, akieleza kuwa; Umma wa Kiislamu leo unakabiliwa na dhuluma na mashinikizo katika sehemu mbalimbali za dunia, alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonesha msimamo mkubwa wa kupambana na Uzayuni, na Mwenyezi Mungu amelijaalia ushindi taifa la Iran; habari ambayo imewaletea furaha wananchi wa Bangladesh.
Aliufafanua uhusiano kati ya Iran na Bangladesh kuwa ni wa kina na wa kindugu, na akaongeza: “Tulikwenda Iran kushiriki katika Swala ya maiti na ibada za mazishi, na tunamuomba Mwenyezi Mungu amrehemu marehemu huyo, amsamehe na ampe daraja ya juu Peponi. Dhamira ya Ayatullah Khamenei (ra) ilikuwa ni kutawala kwa mafundisho ya Qur'ani na Sunnah katika nchi za Kiislamu na kujitahidi kuleta umoja wa Umma wa Kiislamu. Kwa hakika, alikuwa miongoni mwa askari mashujaa wa Mwenyezi Mungu katika njia ya kufanikisha lengo hilo tukufu.”
Mujibur Rahman aliendelea kwa kuelezea misimamo ya kisiasa ya Bangladesh kuhusu maendeleo ya eneo, akisema: “Sera yetu ya mambo ya nje imejengwa juu ya msingi kwamba; popote Umma wa Kiislamu unapofanyiwa dhuluma, tunapaswa kuchukua msimamo na kupaza sauti dhidi yake. Serikali pamoja na Jamaat-e-Islami Bangladesh mara nyingi zimelaani mashambulizi ya Israel na vitendo dhidi ya Waislamu kupitia taarifa rasmi, maandamano na mikusanyiko ya wananchi.”
Mwakilishi huyo wa Bunge la Bangladesh pia alisema kuwa; Jamaat-e-Islami Bangladesh, ikiwa na zaidi ya wanachama na wafuasi 10,000, imeandaa maandamano makubwa ya kupinga mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya ardhi ya Iran. Akiweka mkazo juu ya umuhimu wa umoja wa Waislamu chini ya Qur'ani na Sunnah, aliongeza kuwa mbali na uungaji mkono huo wa wananchi, kiongozi wa upinzani na Dkt. Shafiqur Rahman, Amir wa Jamaat-e-Islami Bangladesh, pia amechukua misimamo thabiti ndani ya Bunge kulaani hatua za Marekani na Wazayuni dhidi ya mamlaka ya Iran.
Akiielezea furaha yake kuhusu ushindi wa Iran katika vita vya tatu vya kulazimishwa na madola makubwa ya dunia, alisema: “Sisi daima tutasimama pamoja na mataifa yaliyodhulumiwa, waathirika wa vita na wale waliopoteza maisha na mali zao. Sera yetu ni kwamba hatutamdhulumu yeyote wala hatutakubali kudhulumiwa.”
Mwishoni, Mujibur Rahman alitoa shukrani kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zake za kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu, kupanua shughuli za kidini na kitamaduni, pamoja na kuitumikia dunia ya Kiislamu. Pia alielezea matumaini yake kuwa njia hiyo itaendelea kwa nguvu zaidi katika kuutumikia ubinadamu na Umma wa Kiislamu.
Maoni yako