Jumatatu 27 Julai 2026 - 08:30
Hatua mpya za vyombo vya usalama vya Bahrain dhidi ya Maulamaa wa Kishia zafichuliwa

Hawza/ Shirika la Salam la Demokrasia na Haki za Binadamu nchini Bahrain limesikitishwa na kulaani ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na vitendo visivyofaa vilivyofanywa dhidi ya idadi ya maulamaa wa dini ya Kishia nchini humo.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Shirika la Salam la Demokrasia na Haki za Binadamu nchini Bahrain limesikitishwa na kulaani ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na vitendo visivyofaa vilivyofanywa dhidi ya baadhi ya maulamaa wa kidini ya Kishia nchini humo. Maulamaa hao walikamatwa na vyombo vya usalama tarehe 9 Mei 2026 (19 Ordibehesht 1405 H.Sh.).

Shirika hilo, katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, lilisema kuwa; maulamaa waliokamatwa walifanyiwa vipigo vya kimwili, matusi ya maneno na vitendo vya kuwavunjia heshima vilivyochochewa na misingi ya kimadhehebu. Aidha, chini ya mateso na udhalilishaji, walilazimishwa kutia saini kumbukumbu za mahojiano na kukiri madai ya uongo. Taarifa hiyo ilieleza kuwa vitendo hivyo si tu ukiukaji wa wazi wa viwango vya kimataifa na vya ndani vya haki za binadamu, bali pia vinapingana kabisa na taarifa ya hivi karibuni ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Bahrain iliyodai kuhakikisha haki za kisheria za watuhumiwa.

Shirika hilo, likirejelea kupokea ripoti zilizothibitishwa, lilisisitiza kuwa; maulamaa wa Kishia wamekumbana na mfululizo wa hatua za kimfumo zilizokiuka haki za msingi za waliokamatwa na zinazochukuliwa kuwa ni vitendo vya kuwavunjia heshima utu wa binadamu. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, baadhi ya maulamaa hao walipigwa na maafisa wa uchunguzi na kutukanwa kwa maneno yenye misingi ya kimadhehebu. Pia walitishiwa kufanyiwa ukatili wa kingono, kunyang'anywa uraia, na kudhihakiwa kwa sababu ya imani yao ya kidini. Taarifa hiyo iliongeza kuwa; vitendo hivyo vinapingana na madai ya Bahrain kuhusu kujitolea kwake katika kuvumiliana kidini na kuishi kwa amani. Vilevile, mawakili hawakuruhusiwa kupata nyaraka za kesi kwa ajili ya kuzichunguza na kuandaa utetezi.

Shirika la Salam liliongeza kuwa; yaliyowakuta maulamaa hao yanaonesha matumizi mabaya ya mamlaka ya kisheria na vyombo vya utekelezaji wa sheria, ukiukaji wa Katiba na kuingilia uhuru wa mhimili wa mahakama. Pia lilisema kuwa hatua hizo zinapingana na wajibu wa kimataifa wa Bahrain, hususan mapendekezo ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kupinga Mateso (UN Committee Against Torture), ambayo iliitaka Bahrain kujiepusha na matumizi ya mateso au unyanyasaji. Kwa mujibu wa shirika hilo, hali hiyo imeibua mashaka makubwa kuhusu uadilifu wa mchakato wa sasa wa kimahakama na kiwango cha kuzingatia dhamana za kesi ya haki, kwa kuwa mwenendo wa kesi hiyo unaonesha dalili za kuwa ni mchakato wa juu juu unaolenga kutoa mwonekano wa uhalali wa kisheria kwa vitendo visivyo halali vilivyofanywa dhidi ya watuhumiwa.

Mwishoni, shirika hilo lilitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na huru kuhusu ukiukaji huo wote wa haki na vitendo vya unyanyasaji, kuwachukulia hatua wahusika, kuwaachilia mara moja maulamaa waliokamatwa, na kuwapatia huduma za matibabu wanazohitaji.

Shirika la Salam pia lilisisitiza kuwa; ni lazima mchakato wa kimahakama katika kesi hiyo upitiwe upya, na taarifa zinazohusiana na kesi hiyo ziondolewe usiri ili umma uweze kufahamishwa kwa uwazi na kuhakikisha kuwa mamlaka ya kiutendaji na ya kimahakama hayatumiwi vibaya.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha