Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, kwa mujibu wa hati ya malalamiko iliyowasilishwa na watawa wanawake wa New York, sheria hiyo inaweza kuzilazimisha taasisi za kidini kushiriki katika kuwezesha kujiua kwa msaada wa daktari, kwa kuwapa wagonjwa taarifa kuhusu hatua hiyo, kuhalalisha kitendo hicho kupitia ushauri, kuzungumza kuhusu suala hilo na wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyotibika, kuwasaidia kukamilisha taratibu zinazohitajika ili wastahiki kupata dawa za kukatisha maisha, na kuwaandaa kisaikolojia kwa hatua hiyo.
Walalamikaji katika kesi hiyo wameiomba mahakama iamue kwamba watawa hao wasilazimishwe tena na taasisi au kampuni kufanya jambo hilo, na kwamba ikiwa mtu yeyote wa kanisa atakataa kushirikiana nao katika utekelezaji wa sheria hiyo, asiadhibiwe.
Rosary Hill Home, taasisi ya hisani inayosimamiwa na Masista wa Dominican Hawthorne, ni mmoja wa walalamikaji katika kesi hiyo. Taasisi hiyo imehudumia takribani wagonjwa maskini 45,000 wa saratani mjini New York, ikitoa huduma za bure hadi mwisho wa maisha yao bila kujali imani yao ya kidini au asili yao ya kitamaduni.
Mama Mkuu Mary Edward, Mkuu wa Masista wa Dominican Hawthorne, alisema: "Kwa zaidi ya miaka 125 tumekuwa tukiwahudumia maskini wanaokaribia kufariki kutokana na saratani, tukiamini kwamba huduma hii ni neema kutoka kwa Kristo mwenyewe. Wajibu wetu ni kuwapa faraja, maombi na huduma za tiba zenye huruma wale wanaoteseka, si kuwahamasisha kufa kwa sababu ya sera za kiuchumi!"
Aliongeza: "Tunatumaini mahakama itatoa uamuzi wa haki ili tuwe huru kuhifadhi imani yetu, kwa sababu sisi ni waaminifu waliokabidhiwa na Mwenyezi Mungu kuwahudumia watu, si watumishi wa Shetani."
Chanzo: Fox News.
Maoni yako