Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, taarifa zilizopokelewa zinaonesha kuwa "Rais wa Syria", Muhammad Al-Jolani (Ahmad Al-Sharaa), katika siku za hivi karibuni alipokea "ushauri" kutoka kwa serikali ya Iraq ukimtaka kutojiingiza katika suala la Lebanon. Ujumbe huo umetolewa wakati ambapo Marekani na Saudi Arabia zinaongeza shinikizo kwa lengo la kuisukuma Damascus ichukue nafasi katika makabiliano dhidi ya Hizbullah.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, ujumbe wa Iraq ulikuwa na "onyo" kwamba, "kujihusisha kokote kwa Syria katika medani ya Lebanon kutakuwa na athari za moja kwa moja kwa Syria yenyewe." Upande wa Iraq uliiarifu Damascus kwamba, "iwapo Mashia wa Lebanon au Hizbullah watakabiliwa na hatari kutoka ndani ya ardhi ya Syria, makundi ya Muqawama ya Iraq hayatabaki mikono mitupu," na kwamba, "kila hatua ambayo Syria itachukua kuielekea Lebanon huenda ikajibiwa na hatua kama hiyo ya Iraq kuielekea Syria."
Vyanzo hivyo viliongeza kuwa; Baghdad imeikumbusha Damascus kwamba; kuingia katika mkondo huo kutafungua milango ya athari za kiusalama na kikanda ambazo hazitakuwa na manufaa kwa Syria, wala hazitasaidia juhudi zake za kuimarisha utulivu wa ndani au kujenga upya uhusiano wake na nchi jirani.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Al-Jolani aliwaarifu maafisa wa Iraq kuwa serikali ya Marekani kweli ilimtaka aingilie suala la Lebanon na kuchukua msimamo dhidi ya Hizbullah, lakini alisisitiza kuwa amekataa ombi hilo. Alieleza wazi kuwa Damascus haina mpango wa kuingilia medani ya Lebanon wala kurejea katika sera za zamani za kuingilia masuala ya nchi nyingine, aidha alisema kuwa; kipaumbele cha uongozi wake katika hatua ya sasa ni kulinda utulivu wa Syria na kuepuka kufungua medani mpya za migogoro.
Katika muktadha huo, vyanzo vilifichua kuwa Ali Al-Zaidi, Waziri Mkuu wa Iraq, anatarajiwa kufanya ziara mjini Damascus mwezi huu. Katika ziara hiyo atafanya mazungumzo na Rais wa Syria kuhusu mustakabali wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili pamoja na mafaili yenye sura za kidini na kisiasa.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Al-Zaidi na Al-Jolani watajadili agenda za hatua za kiuchumi zitakazojumuisha usambazaji wa mafuta kwa Syria, kufunguliwa tena kwa njia ya kusafirisha mafuta kwenda kwenye kiwanda cha kusafishia mafuta cha Banyas, pamoja na kufungua soko la Iraq kwa bidhaa za Syria.
Kiongozi huyo wa Iraq pia atazungumza na uongozi wa Syria kuhusu "hali ya Mashia nchini Syria na namna ya kuhakikisha kunakuwepo dhamana zinazohitajika za kulinda haki zao na kuhifadhi maeneo yao matakatifu, hususan Haram ya Bibi Zainab (as)." Aidha, pande hizo zitajadili mbinu za kuimarisha ushiriki wa makundi mbalimbali ya wananchi wa Syria katika taasisi za serikali, sambamba na mkondo wa utulivu unaolengwa na Damascus.
Al-Zaidi pia atawasilisha kwa Al-Jolani suala la "Walebanon na Wasyria ambao walipoteza makazi yao au walihamishwa kutoka vijiji vya pembezoni mwa mkoa wa Homs baada ya kuanguka kwa utawala wa zamani," ili kujadili namna ya kuweka mazingira yanayofaa kwa kurejea kwao.
Inafaa kutajwa kuwa, ratiba ya ziara ya Al-Zaidi inajumuisha kutembelea Msikiti wa Umayyad na Haram ya Bibi Zainab (as), ambapo inatarajiwa kutangaza kurejea kwa ziara za kidini katika Haram hiyo tukufu pamoja na kurejea kwa mazuwari wa Iraq, ikiwa ni sehemu ya kufufua shughuli za kidini kati ya nchi hizo mbili.
Ujumbe huu wa Iraq umetolewa wakati ambapo Marekani inaongeza shinikizo la kuisukuma Damascus kushiriki katika suala la Lebanon. Katika muktadha huo, vyanzo vya taarifa vilisema kuwa kauli za hivi karibuni za Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu uwezekano wa kuitaka Syria kuchukua hatua dhidi ya Hizbullah, zinapaswa kueleweka zaidi kama sehemu ya shinikizo la kisiasa na propaganda za vyombo vya habari kuliko kuwa mipango ya utekelezaji wa moja kwa moja. Vyanzo hivyo viliongeza kuwa jumbe za awali za Syria, zilizowasilishwa kwa Hizbullah kupitia njia za Uturuki na wahusika wengine wa kikanda, zilisisitiza kwamba Damascus haina nia ya kujiingiza katika masuala ya Lebanon na inalenga kufunga ukurasa wa yaliyopita.
Misimamo hiyo inaendana na tathmini zinazoonesha kuwa ushiriki wowote wa Syria katika mzozo wa aina hiyo hauwezekani bila kupata uungwaji mkono wa wazi kutoka Uturuki, jambo ambalo hadi sasa halijapatikana, kwa kuwa Ankara ina wasiwasi kuhusu mpangilio wowote ambao unaweza kuimarisha ushawishi wa Israel nchini Syria na Lebanon.
Vyanzo vinavyofuatilia maendeleo haya vinaeleza kuwa; ujumbe wa Iraq hauwezi kutenganishwa na mazingira ya kikanda yaliyofuatia maziko makubwa ya Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei nchini Iraq, maziko ambayo yanaonekana kuwa ishara ya kiwango kikubwa cha mshikamano na uhamasishaji ndani ya jamii za Kishia katika eneo hili. Kwa mujibu wa mtazamo huo, ushiriki wowote wa Syria katika makabiliano dhidi ya Hizbullah hautatazamwa kama suala la Lebanon au Syria pekee, bali kama onyo la kupanuka kwa wigo wa makabiliano hadi katika medani nyingine mpya za eneo hili.
Maoni yako