Jumamosi 18 Julai 2026 - 14:50
Iran ndiyo nchi pekee iliyosimama pamoja na Yemen kwa kutegemea wajibu wake wa Kiislamu na kibinadamu

Hawza/ Ali Al-Emad amesisitiza kuwa; mapambano ya kuvunja mzingiro dhidi ya Yemen ni wajibu wa kitaifa na jukumu lisiloweza kuachwa, wala si hatua ya kisiasa au chombo cha shinikizo la kijeshi.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Ali Al-Emad, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah ya Yemen, katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al-Masirah, alisisitiza kuwa, mapambano ya kumaliza mzingiro dhidi ya Yemen si mbinu ya kisiasa wala nyenzo ya shinikizo la kijeshi, bali ni wajibu wa kitaifa ambao hakuna uwezekano wa kuurudia nyuma.

Akirejelea mateso ya wananchi wa Yemen kwa kipindi cha miaka 11 iliyopita, alisema: Uongozi wa Yemen unaendelea kutekeleza wajibu wake kwa wananchi wake, na njia ya kuvunja mzingiro itaendelea kwa nguvu licha ya hujuma zote za Saudi Arabia.

Al-Emad, akizungumzia hatua za hivi karibuni za Saudi Arabia dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a, alisema: Mashambulizi ya Saudi Arabia yamefichua tena kwa kila mtu nafasi halisi ya nchi hiyo. Riyadh imeamua kuendelea na mzingiro dhidi ya wananchi wa Yemen kwa kutekeleza miradi ya Marekani na utawala wa Kizayuni, hata kama hatua hiyo itaisababishia Saudi Arabia yenyewe madhara makubwa ya kijeshi na kiusalama.

Kiongozi huyo wa Yemen aliongeza kuwa; mshikamano wa serikali na wananchi wa Yemen katika operesheni ya "Kuvunja Mzingiro" unaonyesha utayari kamili wa wananchi kudai haki zao na kumaliza hali hiyo.

Akitaja matatizo yanayowakabili mamilioni ya Wayemeni, alisema: Mamilioni ya wahamiaji wanasubiri kurejea nyumbani bila kupitia mateso ya safari ndefu na gharama kubwa. Aidha, maelfu ya wagonjwa wamenyimwa haki ya kupata matibabu, huku wanafunzi na wananchi wengine wakinyimwa haki yao ya msingi ya kusafiri kwa uhuru.

Al-Emad pia alirejelea vifo vya wagonjwa wengi vilivyosababishwa na kushindwa kusafiri kwa ajili ya matibabu na akauliza: Ni nani aliyeipa Saudi Arabia haki ya kuwazuia raia wa Yemen kutumia anga ya nchi yao na huduma za mashirika ya ndege ya kiraia?

Mwishoni mwa sehemu hiyo ya mahojiano, alisisitiza kuwa, Saudi Arabia inapaswa kutambua kuwa hatua ya Yemen inatokana na wajibu wa serikali kwa wananchi wake. Alitaja pia wahanga wa ajali za barabarani, vitendo vya unyang'anyi, utekaji na vifo vya wasafiri wanaolazimika kutumia njia mbadala zenye ugumu mkubwa, akisema kuwa; kumaliza mateso hayo ni matakwa ya haraka na yasiyoweza kuahirishwa ya wananchi wa Yemen.

Iran imethibitisha wajibu wake wa kibinadamu kwa kuwaunga mkono wananchi wa Yemen

Ali Al-Emad, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah ya Yemen, aliendelea katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Al-Masirah kwa kuishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuchukua hatua ya kuanzisha safari za ndege kwa ajili ya kuisaidia Yemen.

Alisisitiza kuwa; marubani wa Iran walitekeleza jukumu hilo kwa ari ya kujitolea na kwa kutambua hatari zilizokuwepo, na hivyo wakasimama bega kwa bega na wananchi wa Yemen.

Al-Emad alisema: Iran ndiyo nchi pekee iliyotekeleza wajibu wake wa kidini na kibinadamu na kuisaidia Yemen wakati muungano wa kijeshi wa Kiarabu ulikuwa ukitumia uwezo wake wote kuendeleza mzingiro dhidi ya wananchi wetu. Hatua hiyo ni mfano halisi wa umoja wa Umma wa Kiislamu.

Mjumbe huyo mwandamizi wa Ansarullah, akizungumzia mwitikio mkubwa wa hatua hiyo miongoni mwa wananchi wa Yemen na katika nchi nyingine za Kiarabu, alisema: Hata watu wengi wanaoipinga Ansarullah waliiunga mkono hatua hiyo. Msimamo huo unaonyesha umuhimu wa hatua ya Iran kwa wakati mwafaka na kufichuka ukweli wa misimamo ya Saudi Arabia mbele ya maoni ya umma.

Akiikosoa vikali Riyadh, aliongeza: Saudi Arabia imeonesha kuwa iko tayari hata kuhatarisha usalama wa viwanja vyake vya ndege na maslahi ya wananchi wake ili kuendeleza miradi ya Kizayuni katika eneo hili.

Riyadh, huku ikizuia safari za ndege za kiraia kwa kisingizio cha "kulinda mamlaka ya nchi", wakati huohuo inaruhusu ndege za kivita za kigeni kutumia ardhi yake kushambulia Yemen. Hivyo imezidi kudhihirisha sera zake za viwango viwili na zisizo na mantiki.

Al-Emad alieleza kuwa; serikali na wananchi wa Yemen wako tayari kikamilifu kusimamia mapambano haya. Alisema kuwa abiria wote wa safari hizo za ndege, kuanzia viongozi wa ngazi za juu hadi wagonjwa na waandishi wa habari, walishiriki kwa kutambua kikamilifu hatari zilizokuwepo na kwa roho ya kujitolea kwa shahada ili kuvunja mzingiro. Hakukuwa na dalili yoyote ya kurudi nyuma wala hofu, na azma ya Wayemeni ya kufikia heshima na uhuru ilimshangaza adui.

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah alisisitiza kuwa; serikali ya Yemen kwa sasa kwa uratibu kamili, inaendelea na juhudi za kujenga upya na kuufanya Uwanja wa Ndege wa Sana'a urejee kufanya kazi. Pia aliionya Saudi Arabia kwamba mzingiro huo utavunjwa kikamilifu mapema au baadaye, na kwamba ukaidi wowote mpya utakabiliwa na jibu kali zaidi. Alisema matukio ya hivi karibuni yalikuwa ni "ujumbe mzito wa onyo" kwao.

Mwishoni mwa mazungumzo yake, Al-Emad aliwataka wakazi wa maeneo mbalimbali ya Saudi Arabia kuwa waangalifu dhidi ya sera za uharibifu za ukoo wa Aal Saud, ambazo zinaipeleka nchi yao kwenye uharibifu wa miundombinu kwa ajili ya kulinda maslahi ya kundi dogo la watu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha