Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Ali Al-Qar'awi, Mkurugenzi wa Kituo cha Masuala ya Kifikra na Kiutamaduni cha Ataba Tukufu ya Imam Hussein (as) mjini Karbala, katika mahojiano na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza mjini Mashhad, alifafanua vipengele vya kimkakati, kisiasa, kijamii na kimawasiliano vya mazishi makubwa yaliyohudhuriwa na mamilioni ya watu kwa ajili ya Hadhrat Imam Khamenei. Alisema tukio hilo lilikuwa zaidi ya hafla ya kuuaga mwili wa marehemu, na akabainisha: "Kwa mtazamo wa kimkakati, mazishi haya ya mamilioni ya watu yalikuwa zaidi ya sherehe ya kuaga; yalikuwa maonesho ya nguvu ya ushawishi na ya umoja wa safu katika kukabiliana na nyakati za misukosuko."
Aliongeza kuwa, ushiriki huo mkubwa uliipa fikra na utamaduni wa Kishia utambulisho imara usiotetereka, na kuwapelekea maadui wa Mhimiili wa Haki ujumbe kwamba mhimili huo hautavunjika wala kutengana mbele ya mikondo ya uovu na ubeberu, bali utaendelea na njia yake ukiwa na mshikamano mkubwa zaidi kuliko hapo awali.
Akizungumzia upande wa kisiasa wa tukio hilo, Al-Qar'awi alisema: "Mazishi haya yalikuwa ujumbe wa kimkakati kwa wote wanaodhani kwamba kupitia mauaji au kuwaondoa viongozi wa dini wanaweza kuvunja uhusiano kati ya Umma na Marjaiyya. Mwamko huu wa wananchi kwa vitendo umeunda ngome ya ulinzi ambayo kuanzia sasa itaongeza kwa kiwango kikubwa gharama ya jaribio lolote la kuvamia heshima ya Marjaiyya na wanazuoni wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu, na itazima fikra yoyote ya uchokozi."
Aliendelea kusema kuwa; katika medani ya vyombo vya habari, tukio hilo limevunja propaganda zote za Magharibi zilizokuwa zikidai kuwepo kwa pengo kati ya mataifa na viongozi wa dini, na limeuonesha ulimwengu kwamba uhusiano wa Umma wa Kiislamu unatokana na itikadi, si kwa maslahi ya muda mfupi.
Mazishi ya Mamilioni ya Watu; Hatua Muhimu ya Kuimarisha Mhimili wa Muqawama
Mkurugenzi wa Kituo cha Masuala ya Kifikra na Kiutamaduni cha Ataba Tukufu ya Imam Hussein (as), huku akiendelea kuzungumzia athari za kikanda za tukio hilo la kihistoria, alisema: "Kwa muda mfupi, mazishi haya yalisababisha msukumo mkubwa wa kisaikolojia na kiimani ndani ya jamii. Kuvumilia kusubiri kwa saa nyingi ili kuuaga mwili mtukufu kulidhihirisha kwamba azma ya wananchi ya kuendelea katika njia ya Muqawama ni kubwa zaidi kuliko mahesabu ya kimada yanayofanywa na maadui."
Alibainisha kuwa subira hiyo ya hiari na iliyojaa shauku ilikuwa mazoezi ya kuwajengea watu uwajibikaji mbele ya malengo makubwa ya Umma wa Kiislamu.
Al-Qar'awi, akisisitiza athari za muda mrefu za tukio hilo, aliongeza: "Mazishi haya yalikuwa hatua ya kihistoria iliyobatilisha mipango yote ya ubeberu wa dunia ya kuleta mifarakano kati ya mataifa ya Iran na Iraq. Maadui wamekuwa wakijaribu daima kuchochea hisia za utaifa ili kujenga ukuta wa kutokuaminiana kati ya mataifa haya mawili, lakini ushiriki huu wa mamilioni ya watu umethibitisha kwamba katika nyakati nyeti za kihistoria, uhusiano wa kiroho na wa kifikra kati ya Iran na Iraq ni wa kina kiasi kwamba hakuna njama yoyote inayoweza kuuvunja."
Mwishoni, alisisitiza kuwa; mbali na uhusiano wa kisiasa, sababu kuu ya umoja huu ni uhusiano wa kiimani na kiitikadi. Alisema kitovu cha mshikamano huo ni imani ya pamoja na thabiti ya mataifa haya mawili kuhusu kungojea kudhihiri kwa Mwokozi wa wanadamu wote, Hadhrat Imam Mahdi (aj).
Alieleza kuwa imani hiyo ya mustakabali wenye mwangaza na uliojaa uadilifu ndiyo kamba inayounganisha nyoyo za waumini na kuupa Mhimili wa Muqawama kina cha kimkakati na uhalali wa kimungu; ni uhusiano unaovuka mipaka ya kijiografia na utaendelea kuwa hai na wenye nguvu hadi pale haki ya kudhihiri itakapodhihirika.
Maoni yako