Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, mji wa Baalbek ulishuhudia mkusanyiko mkubwa wa mshikamano; hatua iliyofanyika kama ishara ya shukrani na uaminifu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa ushiriki mkubwa wa wananchi wanaouunga mkono muqawama, pamoja na ushiriki mpana wa viongozi na sura mbalimbali za kisiasa, kijamii na kidini za eneo hilo, katika mazingira yaliyosheheni kaulimbiu za kuunga mkono muqawama na Iran na kulaani hujuma dhidi ya Lebanon na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika hotuba zilizotolewa katika hafla hiyo, meya wa Baalbek, Ahmad Al-Tufayli, alisisitiza kwamba; kusimama imara na kuwa na subira ndio njia pekee ya kuzuia uchokozi, na akasema: “Msimamo huu wa kishujaa na uthabiti huu wa hali ya juu ndio jambo litakalomlazimisha adui kujisalimisha, hasa baada ya haiba ya majeshi yenye nguvu zaidi duniani kuvunjika. Na kwa baraka za msimamo huu thabiti, usitishaji vita utawekwa kwa masharti yatakayohiifadhi heshima ya Umma wa Kiislamu na matarajio yake.”
Kwa upande mwingine, Sheikh Fadi Sukriyya, msemaji wa “Harakati ya Kuunga Mkono Muqawama”, akilisifu jukumu la kihistoria la Iran, alisema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitimiza ahadi yake na kuifanya kuwa uhalisia; ilitimiza kaulimbiu iliyotolewa tangu wakati wa kuasisiwa Mapinduzi haya yenye baraka: ‘Hatua kwa hatua kuelekea Al-Quds’, kaulimbiu ambayo mwangwi wake bado unasikika hadi leo.”
Sheikh Sukriyya pia alikosoa sauti zinazopinga muungano huu, na kwa kurejea Aya ya Qur’ani:
﴿وَتَعَاوَنُوا عَلَی الْبِرِّ وَالتَّقْوَی﴾
aliuliza: “Je, kuondoa dhulma, kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kupambana na maadui wa ubinadamu na kutoa damu katika njia ya haki, si miongoni mwa viwango vya juu kabisa vya wema na uchamungu? Sisi tunashirikiana na watu hawa katika kufanya mema, ilhali wengine wanashirikiana katika dhambi na uchokozi.”
Wakati huohuo, Sheikh Tamer Hamza, mkuu wa Idara ya Tablighi na Shughuli za Hizbullah, akijibu mitazamo ya kisiasa ya wapinzani, alisema: “Baadhi wanadai kwamba; sisi tunatetea maslahi ya Iran na wanajaribu kueneza fikra kwamba yanayotokea ni ‘vita vya wengine katika ardhi yetu’. Maneno haya ni uongo mtupu na hayana msingi wowote, uhalisia unaonyesha kwamba Iran imeitetea Lebanon, kijeshi na kisiasa.”
Aliendelea kwa kusema huku akirejelea matokeo ya njia ya diplomasia: “Iran ilijitahidi kuhakikisha kwamba Lebanon inashiriki katika mazungumzo na kuwa sehemu muhimu ya mchakato huo, Jamhuri ya Kiislamu imeweza kupata ushindi mkubwa wa kisiasa na kidiplomasia dhidi ya Wazayuni; ushindi ambao kwa upana wake unazidi hata ushindi wa kijeshi uliopatikana dhidi ya meli za kivita na vikosi vya Marekani katika eneo hili na katika Ghuba.”
Afisa huyo wa Hizbullah pia alisema: “Iran ilisimama bega kwa bega na Lebanon wakati Dhahiya ya Kusini iliposhambuliwa, Tel Aviv na Haifa zikawa malengo ya mashambulizi, na Lebanon ikawa kipengele cha kwanza katika meza ya mazungumzo, haya ndiyo mazungumzo ya mashujaa na wenye nguvu, wale ambao wanamiliki karata halisi za nguvu. Wakati baadhi wanataka mazungumzo ya moja kwa moja na adui chini ya usimamizi wa Marekani, Lebanon leo inafanya mazungumzo kwa kutegemea karata yake kuu ya nguvu, nayo ni Muqawama wa Kiislamu, na kwa msaada wa watu wote huru na wenye heshima, hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Maoni yako