Jumapili 31 Mei 2026 - 18:20
Wananchi wa Bahrain walilaani uporaji wa mali za wakfu wa Mashia unaofanywa na watawala wa nchi hiyo

Hawza/ Vikosi vya mamluki na wanamgambo wa kiraia wanaohusishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain viliweka mzingiro mkali wa kiusalama katika mji wa Al-Diraz.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, vikosi vya mamluki na wanamgambo wa kiraia wanaohusishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain viliweka mzingiro mkali wa kiusalama katika mji wa Al-Diraz ili kuwazuia Mashia kwa wiki ya 85 mfululizo kutekeleza Swala ya Ijumaa ya pamoja.

Kuanzia asubuhi ya siku ya Ijumaa, tarehe 29 Mei 2026, vikosi vya mamluki, vikisaidiwa na magari ya kijeshi pamoja na vikosi vyenye silaha, viliongeza uwepo wao katika maeneo yanayozunguka Msikiti wa Imam Sadiq (as), huku vikiwa katika hali ya tahadhari kwa ajili ya kuanza maandamano ya wananchi ya kupinga vita ambavyo utawala wa Al Khalifa umevianzisha dhidi ya Mashia nchini Bahrain.

Licha ya mzingiro huu wa kiusalama, maandamano ya wananchi yalifanyika katika maeneo mengi ya Bahrain, waandamanaji walitaka magereza yasafishwe, na wanazuoni wa dini pamoja na wafungwa wa kisiasa waachiwe huru mara moja.

Pia walilaani marufuku ya kufanyika kwa Swala ya Ijumaa iliyowekwa na mfumo tawala, na wakasisitiza kukataa udhibiti rasmi juu ya masuala ya kidini pamoja na mashinikizo yanayoendelea dhidi ya uhuru wa kidini.

Wananchi wa Bahrain pia walikataa uporaji wa mali za wakfu za Mashia unaofanywa na Serekali, pamoja na kuvamiwa kwa matukufu yote, shakhsia, taasisi na misingi ya Madhehebu ya Jaafari, na wakatoa wito wa kusitishwa kwa sera za ubaguzi, ukandamizaji wa kimadhehebu pamoja na mzingiro uliowekwa dhidi ya ibada na alama za kidini za Waislamu wa Kishia.

Pia walisisitiza msimamo wao wa kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mapambano yake ya kuzuia uchokozi wa Marekani na Wazayuni, na wakatangaza utii wao kwa shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Sayyid Ali Khamenei.

Waandamanaji walitoa wito wa kusitishwa kwa uwepo wa Marekani na kufukuzwa kwa kambi za kijeshi za kigeni ili mamlaka kamili ya taifa na usalama wa ndani ya nchi vipatikane.

Pia walisisitiza umuhimu wa kusitishwa kwa makubaliano ya kuhalalisha uhusiano na adui wa Kizayuni, kufukuzwa balozi wa utawala wa kivamizi kutoka nchini na kufungwa kwa ubalozi wake mjini Manama.

Mamlaka za Bahrain zimekuwa zinapiga marufuku kufanyika Swala ya Ijumaa ya pamoja tangia tarehe 4 Oktoba 2024. Hatua hii ilikuja kufuatia msisitizo wa wananchi juu ya kuandaa hafla za kumbukumbu ya shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, pamoja na kuandaa maandamano ya kuunga mkono Muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon, Palestina na Yemen, na kupinga makubaliano ya kuhalalisha uhusiano na utawala wa Kizayuni.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha