Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Papa Leo wa Kumi na Nne, huku akirejelea kuendelea kwa mgogoro wa kibinadamu huko Ghaza, amewataka viongozi wote wenye dhamana kuchukua hatua kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa eneo hilo na kuanza mchakato wa ujenzi upya.
Papa Leo wa Kumi na Nne ambaye alikuwa ameenda katika makazi yake ya mapumziko ya kila wiki katika mji wa Castel Gandolfo karibu na Roma, alipokuwa akitoka katika makazi hayo alizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala ya kimataifa.
Papa huyo ambaye pia alichapisha waraka wenye anuani ya “Ubora wa Ubinadamu” kuhusu misingi ya kumlinda mwanadamu dhidi ya athari za akili mnemba na teknolojia mpya, alitangaza kuwa: Kanisa Katoliki linaendelea kushirikiana katika suala hilo na kampuni ya “Anthropic”.
Akiwaonya watu kuhusu matumizi ya kijeshi ya akili mnemba, alisema: “Leo vita vinaendeshwa kwa kutumia akili mnemba, huko Lebanon pia tumeshuhudia mifano mingine; vita vinavyoendelea bila kujali maisha ya binadamu.”
Kiongozi wa Wakatoliki duniani, huku akijibu swali kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanaharakati wa “Msafara wa Kimataifa wa Sumud” waliokamatwa na jeshi la Israel katika maji ya kimataifa, alisisitiza: “Ni lazima kwa mara nyingine tena tudai kuheshimiwa kwa haki za kibinadamu za watu wote.”
Papa Leo wa Kumi na Nne pia huku akirejelea hali mbaya ya Ghaza alisema: “Kwa masikitiko makubwa, watu wa Ghaza bado wananyimwa misaada ya kibinadamu, hili ndilo lililosababisha kuibuka kwa maandamano, matatizo na hata hatua kama za kusafirishwa kwa msafara wa majini.”
Aliongeza kuwa: “Haya si madai tu, bali ni wito wa dharura; ninawaomba viongozi wote kuwasaidia watu wa Ghaza, kusimama pamoja nao na kuanza mchakato wa ujenzi upya, watu bado wanaishi katika mateso na maumivu.”
Mwisho, Papa alisisitiza kwamba; chuki na vurugu, katika sehemu yoyote duniani, huleta matokeo mabaya na yenye uharibifu mkubwa.
Maoni yako