Alhamisi 28 Mei 2026 - 10:58
Maonesho Makubwa ya Sanaa Kufanyika Dar es Salaam Yakiwa na Ujumbe wa Ubinadamu na Umoja

Hawza/ Kituo cha Utamaduni cha Iran Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Sanaa Bunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeazimia kufanya maonesho maalumu ya sanaa yatakayowakutanisha wanafunzi, wasanii, wabunifu pamoja na wapenda sanaa kutoka maeneo mbalimbali nchini, katika tukio litakalobeba ujumbe wa ubinadamu, mshikamano na uelewano wa kitamaduni.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maonesho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Kupitia Macho Mbalimbali kuelekea Ubinadamu” yanatarajiwa kufanyika siku ya kesho Ijumaa tarehe 29 Mei 2026 katika ukumbi wa Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Tanzania, ambapo washiriki watapata fursa ya kushuhudia ubunifu wa hali ya juu unaoakisi maadili ya jamii na nguvu ya sanaa katika kuunganisha watu.

Waandaaji wa tukio hili wameelezea kuwa; maonesho hayo yamelenga kuonesha namna ambavyo sanaa inaweza kuwa daraja muhimu la kuimarisha mahusiano ya kijamii, kukuza elimu ya utamaduni na kuhamasisha maadili ya kibinadamu kupitia mitazamo tofauti ya wasanii na wabunifu.

Katika tukio hilo, wageni na washiriki watapata nafasi ya kutembelea maonesho ya kazi mbalimbali za kisanii zilizotengenezwa na wanafunzi, sambamba na kushiriki ziara maalumu ya maonesho ya “Shirazis” ambayo yanatajwa kuwa sehemu ya vivutio vikubwa vya siku hiyo.

Aidha, kutakuwepo na darasa maalumu kuhusu utengenezaji wa filamu za uhuishaji (animation), ambapo washiriki watapata elimu na uzoefu kuhusu mbinu za kisasa za ubunifu katika sekta ya sanaa na mawasiliano ya kidijitali, jambo linalotarajiwa kuvutia vijana wengi wenye vipaji vya ubunifu.

Maadhimisho hayo pia yataambatana na shughuli ya kuwaenzi wanafunzi mashahidi wa Minab pamoja na majadiliano maalumu kuhusu nafasi ya ubinadamu katika muziki wa Kiafrika, hatua inayolenga kuonesha mchango wa sanaa na muziki katika kuijenga jamii yenye maadili, huruma na mshikamano.

Kwa mujibu wa waandaaji, tukio hilo litafanyika kuanzia saa 13:00 mchana na litakuwa wazi kwa umma bila kiingilio, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo yenye kubeba ujumbe mkubwa wa amani, umoja na maelewano ya kitamaduni kupitia lugha ya sanaa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha