Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Chama cha Wanazuoni wa Ahlul-Bayt cha Uturuki kimetoa taarifa katika kuunga mkono uongozi wa Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
وَنُرِیدُ أَن نَّمُنَّ عَلَی ٱلَّذِینَ ٱسْتُضْعِفُواْ فِی ٱلْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّة وَنَجْعَلَهُمُ ٱلْوَٰرِثِینَ
(Al-Qasas: 5)
Leo hii moyo wa Umma wa Kiislamu unapiga kwa wakati mmoja kati ya huzuni kubwa na heshima thabiti. Kwa upande mmoja kuna wahanga waliotolewa kutokana na mashambulizi ya kinyama ya ubeberu na Uzayuni, na kwa upande mwingine kuna dhihirisho la azma ambayo haijaruhusu bendera hii tukufu kuanguka chini.
Kiongozi mpendwa wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei;
Sisi katika Chama cha Wanazuoni wa Ahlul-Bayt cha Uturuki (AHLA-DER), katika kipindi hiki cha kihistoria, tunamuomba Mwenyezi Mungu kutoka ndani ya nyoyo zetu kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani uwe umejaa kheri na baraka kwa Umma wa Kiislamu.
Kwanza kabisa, tunatoa pole zetu za dhati kutokana na kuuawa kishahidi watu wa thamani katika familia yako, hususan baba yako mtukufu ambaye alikuwa nuru inayoangaza daima katika ulimwengu wa Kiislamu – kiongozi wetu mpendwa. Wao kama babu yao Imam Husain (a.s) walijiunga na msafara wa mashahidi kwa kujitoa mhanga kwa ajili ya heshima ya Uislamu na wanyonge.
Pia damu ya mabinti wetu wasio na hatia ambao waliuawa kinyama katika Shule ya Shajarah Tayyibah, miche hiyo michanga ya nuru, imeonesha tena kwa ulimwengu uso halisi wa ukatili wa Uzayuni na ubeberu wa kimataifa.
Kadhalika tunawakumbuka ndugu zetu wote ambao katika miji mbalimbali ya Iran walikunywa sharubati ya shahada katika mapambano haya matakatifu, au wale walioungana na mashahidi wa Karbala huko Ghaza, Lebanon na maeneo mengine.
Kutokana na hasara hizi kubwa, pamoja na kutoa pole zetu kwako na kwa Umma wa Kiislamu ulio katika maombolezo, pia tunatoa pongezi kwa shahada ya wapendwa hawa waliopata daraja tukufu kama hilo.
Katikati ya mashambulizi ya usaliti na mipango ya giza ya maadui, kuchaguliwa kwako kwa busara ya Baraza la Wataalamu na kwa uangalizi wa Imam wa Zama (a.t.f.s) kuwa kiongozi wa tatu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Walii Faqihi wa Waislamu kumebatilisha ndoto za maadui.
Elimu yako, ujasiri wako, uchamungu wako na malezi yako katika madrasa ya shahada ni ushahidi mkubwa kwamba amana hii tukufu imewekwa mikononi mwa mtu mwaminifu. Tunakupongeza kwa moyo wote kwa kushika nafasi hii tukufu ambayo husikiliza kilio cha wanyonge na haisalimu amri mbele ya ubeberu, na tunaamini kuwa uchaguzi huu umetuliza nyoyo za waumini.
Sisi kama wanazuoni wa Ahlul-Bayt wa Uturuki tunatangaza kwa ulimwengu wote kwamba:
Mikono itakayonyooshwa dhidi ya wasio na hatia, mapema au baadaye itavunjwa na kofi kali la muqawama. Shambulio lolote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linahesabika kuwa shambulio dhidi ya jiografia yote ya Kiislamu na dhidi ya matukufu yetu.
Sisi ni watoto wa Umma ambao, bila kujali rangi, madhehebu au mitazamo, tumeungana chini ya bendera ya Wilaayat al-Faqih. Jaribio lolote la vituo vya fitna halitaweza kamwe kuvunja umoja huu uliomwagiliwa kwa damu ya mashahidi.
Sisi kama wanazuoni wa Ahlul-Bayt na jamii ya Ahlul-Bayt nchini Uturuki tunatangaza kwamba; katika harakati hii tukufu chini ya uongozi wako tutasimama daima katika safu ya haki na uadilifu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupe afya njema, maisha marefu na ushindi katika jukumu hili zito.
Roho za mashahidi wetu ziwe katika furaha na bendera ya Uislamu ibaki juu na imara milele.
Chama cha Wanazuoni wa Ahlul-Bayt cha Uturuki (AHLA-DER)
9 Machi 2026 (1404/12/18)
Istanbul
Maoni yako