Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ahmad Rabiei-Zadeh, Naibu wa Teknolojia na Mkurugenzi wa Idara ya Akili Mnemba ya Kituo cha Utafiti wa Kompyuta na Sayansi za Kiislamu, katika kikao cha tatu cha mfululizo wa vikao vya “Akili Mnemba na Utafiti wa Kidijitali wa Qur’ani” katika Maonesho ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu yanayofanyika katika Muswala wa Imam khomein (r.a) mjini Tehran, alielezea changamoto za miundo ya lugha ya kimataifa na akatangaza maendeleo ya mifumo yenye uwezo wa kurejea vyanzo kwa usahihi na kufikia kiwango cha usahihi kwa asilimia 77 katika uga mahsusi wa tafsiri.
Katika wasilisho la uchambuzi, alieleza mafanikio ya kituo hicho katika kuifanya turathi ya Kiislamu kuwa ya kidijitali, akachambua kwa kina changamoto za kimsingi za miundo mikubwa ya lugha ya kimataifa, na akafichua mikakati ya Kituo cha Noor katika kuendeleza zana mahiri, sahihi na muhimu zaidi—zinazoaminika kwa watafiti.
Naibu wa Teknolojia na Mkurugenzi wa Maabara ya Akili Mnemba ya Kituo hicho, mwanzoni mwa hotuba yake huku akisisitiza juu ya dhamira ya kituo hicho, alisema: Sisi katika Kituo cha Noor tunajiona kuwa na wajibu wa kwenda sambamba na ukuaji na mabadiliko yanayotokea katika teknolojia ya habari. Katika miaka hii, hatukupuuza akili mnemba kama moja ya nyanja zenye matumizi makubwa na zenye mvuto ambazo zinaweza kuleta mageuzi, ili kuwasilisha bidhaa mpya. Jitihada hizi zimekuwa katika uwanja wa programu pamoja na ujenzi wa mkondo wa fikra, mafunzo na kuwawezesha watafiti kutumia teknolojia katika sayansi za Kiislamu. Tumejaribu kuhusisha matawi mbalimbali ya jamii ya kielimu, kuanzia maraji' na maulamaa hadi wanafikra, wanafunzi wa hawza na watafiti, ili kwanza wafahamiane na teknolojia hizi, kisha waweze kutumia uwezo uliopo na kutambua changamoto zake.
Akielezea mafanikio ya awali ya Kituo cha Noor katika utafiti wa kidijitali wa Qur’ani, alisema: Bidhaa nyingi za Qur’ani zimefikia hatua ya kukamilika, muhimu zaidi ikiwa ni hifadhidata pana ya Qur’ani inayojumuisha zaidi ya anuani 400 za tafsiri za Shia na Sunni katika zaidi ya juzuu 2000, pamoja na zaidi ya tarjuma 150 katika lugha hai 30 za dunia. Hifadhidata hii kwa mujibu wa wageni ni kubwa na ya kipekee zaidi nchini. Nyuma ya pazia la programu hizi zote, kuna zaidi ya uwezo 50 unaotegemea akili mnemba ya kiasili kwa ajili ya uchakataji wa maudhui au utoaji wa huduma za utafiti. Uwezo kama uchambuzi wa kisarufi na kimofolojia wa maneno ya Qur’ani mojakwamoja, uwekaji lebo wa aya katika zaidi ya juzuu 140,000 za vitabu, utafutaji wenye muundo wa kisarufi, uingizaji wa mada kiakili na ulinganishi wa kimatamshi wa aya—vyote hivi vilirahisisha michakato ya utafiti iliyokuwa ikichukua muda na gharama kubwa. Aidha, utoaji wa matini kutoka takribani kurasa milioni tatu za makala na juzuu 55,000 za vitabu visivyochapwa kwa kompyuta, pamoja na kulinganisha neno kwa neno Qur’ani na zaidi ya tarjuma 60 za Kifarsi, ni miongoni mwa huduma za kimsingi zilizozitoa hazina za kielimu kutoka kifungoni na kuziweka mikononi mwa watafiti kwa baraka ya teknolojia.
Kufichua Udanganyifu na Upendeleo wa Miundo
Rabiei-Zadeh katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akirejelea kuingia katika enzi ya akili mnemba zalishi na miundo mikubwa ya lugha, alisisitiza ulazima wa kuendeleza miundo ya ndani (ya kitaifa) na kusema: Huenda ikaulizwa kwa nini, licha ya uwepo wa miundo ya kigeni, tunatafuta kutengeneza muundo mahiri wa Kiislamu? Jibu liko katika changamoto za kimsingi za miundo hiyo.
Mojawapo ya changamoto muhimu ni “udanganyifu” au kuzalisha taarifa zisizo sahihi. Kwa mfano, tulipouliza muundo wa kigeni kuhusu maneno yasiyo ya Kiarabu katika Suratul-Waqi‘a, uliorodhesha maneno sahihi lakini ukatoa anuani za aya zisizokuwamo katika sura hiyo. Au katika mfano mwingine, ulitoa orodha ya makala za kisayansi zenye majina ya waandishi maarufu na anuani za hifadhidata za ndani ambazo hazikuwepo kabisa. Haya mawazo ya kubuni huondoa kabisa imani ya mtafiti. Changamoto nyingine ni upendeleo. Miundo hii imefunzwa kwa data nyingi ambazo wakati mwingine zina mwelekeo maalumu; hivyo matokeo yake yanaweza kuwa na taarifa zisizo sahihi, au zenye mwelekeo kwa itikadi au madhehebu fulani. Masuala haya yanaleta ulazima kwwtu sisi kuingia katika uwanja huu na kubinafsisha roboti mahiri kwa mahitaji ya ndani kuwa mara dufu, ili mpango uwe mikononi mwa miundo yenye uaminifu na yenye nyaraka.
Kuzaliwa kwa Msaidizi Mahiri wa Qur’ani
Naibu wa Teknolojia wa Kituo cha Noor akitambulisha mfumo wa “Mazungumzo Mahiri na Tafsiri za Qur’ani Tukufu”, ambao umetengenezwa kama moja ya suluhisho la changamoto hizi, alisema: Mfumo huu uliozinduliwa mwezi uliopita, unawawezesha watafiti kufanya mazungumzo yenye ubora na yenye marejeo na zaidi ya juzuu 2000 za vitabu vya tafsiri. Sifa yake kuu ni maudhui tajiri na utoaji wa majibu kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Tofauti na utafutaji wa jadi, mashine yenyewe mbali na kurejesha matokeo, huyachambua na kuyaweka katika makundi, na kuwasilisha kauli mbalimbali. Faida yake kubwa ikilinganishwa na miundo ya kigeni ni kutoa marejeo ya moja kwa moja kwa vyanzo asilia; kwa kila dai, hutolewa anuani sahihi ya kitabu, juzuu na ukurasa ili mtumiaji aweze kuhakiki kwa mbofyo mmoja. Mchakato wa nyuma ya pazia unajumuisha uchambuzi wa swali la mtumiaji, upanuzi wa maana yake kwa ajili ya utafutaji jumuishi, uteuzi wa nyaraka sahihi zaidi zinazohusiana, na hatimaye uzalishaji wa jibu lililounganishwa na la kiuchambuzi kwa kutumia akili mnemba zalishi. Tathmini zetu zinaonesha kuwa usahihi wa mfumo huu katika uga mahsusi wa utafiti wa Qur’ani unafikia zaidi ya asilimia 77, ilhali usahihi wa miundo ya kigeni katika uga huu ni takribani asilimia 40.
Kuunda Zana kwa Mtafiti wa Kisasa
Rabiei-Zadeh akieleza upeo wa baadaye, aliutaja mfumo huu kuwa ni kipande cha fumbo kubwa zaidi na akasema: Tupo katika hatua ya kuendeleza uwezo mpya kama utafutaji wa kimaana katika aya, uchambuzi wa sauti na muhtasari mahiri wa maoni ya tafsiri chini ya kila aya. Lengo la mwisho ni kuunganisha mfumo huu na miradi mingine kama “Mazungumzo Mahiri na Hadithi”, “Mazungumzo na Matini za Fiqhi” na “Mfumo Mahiri wa Kihistoria” ili kufikia “Msaidizi Mahiri Jumuishi wa Sayansi za Kiislamu” atakayefunika mahitaji yote ya watafiti. Lengo hili linahitaji miundombinu imara ya uchakataji, maudhui yaliyofanyiwa uchakataji na algorithimu za hali ya juu. Mwishoni alisema: Wengi wana hofu ya akili mnemba kuchukua nafasi ya mwanadamu. Bado tuko mbali na hatua hiyo; lakini jambo moja ni hakika—wanadamu walio na vifaa vya akili mnemba bila shaka watachukua nafasi ya watafiti wasiobobea katika zana hizi, na hili linaongeza ulazima wa kunufaika na uwezo huu katika tafiti za Kiislamu.
Kikao hiki cha kitaaluma kilihitimishwa kwa kipindi cha maswali na majibu pamoja na kubadilishana mawazo kati ya mzungumzaji na washiriki.
Maoni yako