Jumamosi 21 Februari 2026 - 17:18
Sababu za ushindi na kushindwa kwa mataifa katika nyakati nyeti na ngumu za kihistoria/ Sifa 10 maalumu za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

Hawza/ Khatibu wa Ijumaa wa Qom alisema: Leo vita vya kiutambuzi na kimtazamo vimetawala akili na dhamiri ya Iran, Uislamu na mhimili wa Muqawama. Ikiwa mtu ataingia katika vita hivi na akafanya kosa la kimahesabu, tutakumbana na taabu nyingi.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafi katika khutba za Swala ya Ijumaa tarehe mosi Esfand 1404 (20 February 2026), zilizofanyika katika Muswalla wa Quds mjini Qom Iran, huku akitoa pongezi kwa kuwasili kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, alichambua maendeleo ya kimataifa na kusema: Hali ambayo leo nchi yetu na ulimwengu wa Kiislamu wanaipitia ni hali ya kipekee. Taifa letu kubwa tarehe 22 Bahman mwaka huu liliunda tukio la kushangaza; liliuonesha ulimwengu utukufu wake wa kifikra na mshikamano wake, na pia likaonesha nguvu mpya mbele ya maadui wa Uislamu, Iran na Mapinduzi. Utukufu na fahari ya 22 Bahman ulikuwa wa kipekee na wa hali ya juu.

Aliendelea kusema: Mataifa yote wakati fulani hufika katika vituo nyeti na vya mgeuko; katika nyakati hizo ufahamu na mwamko ni jambo la msingi sana. Utafiti wa historia ya Uislamu, Iran na dunia unaonesha kuwa; katika hali ngumu ya kihistoria iliyojitokeza, wakati mwingine mataifa yaling'ara na kushinda, lakini wakati mwingine yalighafilika na kushindwa. Sisi tuna Badr, Khaybar na Ahzab ambavyo vilisababisha maendeleo ya Uislamu, na pia tuna Uhud na Siffin ambapo upande wa haki ulishindwa.

Imamu wa Ijumaa ya Qom alibainisha: Katika historia ya Iran na eneo hili pia, wakati mwingine Iran ilishindwa katika vita na wakati mwingine ilishinda. Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa ni nukta ya mgeuko na mwamko wa taifa; Ulinzi Mtakatifu wa miaka minane na wa siku 12 ni alama angavu katika historia yetu ya kisiasa; katika jaribio la mapinduzi ya hivi karibuni pia, ufahamu na mwamko wa taifa tukufu la Iran vilizuia hasara kubwa. Lakini katika vita vya Iran na Uthmani, Iran na Urusi, kupoteza Bahrain na mapinduzi ya 28 Mordad, mambo kama kutokuwa na ufahamu na udhaifu vilizuia ushindi.

Ayatullah A‘rafi aliongeza kuwa: Leo tuko katika hali maalumu. Tarehe 22 Bahman ilizalisha nguvu kubwa, lakini lazima pia tuzitambue sababu za kushindwa kwa mataifa.

Sababu za kushindwa kwa mataifa katika nyakati nyeti na ngumu kihistoria

Sababu ya kwanza: Kosa katika uchambuzi na ukosefu wa ufahamu unaohitajika: Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini aliendelea: Leo vita vya kiutambuzi na kimtazamo vimetawala akili na dhamiri ya Iran, Uislamu na mhimili wa Muqawama. Ikiwa mtu ataingia katika vita hivi na akafanya kosa la kimahesabu, tutakumbana na tabu nyingi.

Aliongeza: Leo baadhi ya matukio yaliyo wazi yameondolewa katika fikra za vijana. Kuanguka kwa utawala wa kifalme usio na mantiki ambao msingi wake ulikuwa juu ya dhulma na uonevu ni fahari kubwa ya taifa la Iran. Ninyi mliuangusha utawala dhalimu wa Pahlavi uliokuwa umezama katika ufisadi na uharibifu na ulioungwa mkono na maadui. Utawala wa Pahlavi ndio ulioruhusu kwa mara ya kwanza ukoloni kuingia nchini na kuhalalisha utegemezi.

Alisisitiza: Iran daima ilikuwa dola yenye himaya, ikiwa na ushindi na kushindwa kwa pamoja, lakini Pahlavi aliandika utegemezi katika wasifu wa Iran. Leo wapo wasioijua misingi hii, na hvyo ndio vita vya kiutambuzi na kimtazamo.

Sababu ya pili: Udhaifu katika mshikamano wa kijamii: Aliongeza kuwa; udhaifu katika mshikamano na umoja ni sababu nyingine inayoweza kusababisha kushindwa kwa mataifa katika vipindi nyeti.

Sababu ya tatu: Kulegea kwa azma na dhamira: Mjumbe wa Mafaqihi wa Baraza la Walinzi alisema: Ikiwa wakoloni watachukua azma na dhamira yetu, tutashindwa. Azma ndiyo siri kuu ya ushindi. Mwenyezi Mungu katika Aya ya 46 ya Suratul-Anfal anasema:
“Wala msizozane mkashindwa na nguvu zenu zikaondoka.”

Sababu ya nne: Hofu na huzuni mbele ya adui: Alisema: Mwenyezi Mungu katika Aya ya 139 ya Aal ‘Imran anasema: “Wala msilegee wala msihuzunike, nanyi mtakuwa juu ikiwa nyinyi ni waumini.” Mwenyezi Mungu katika aya hii anasisitiza kutokuogopa mbele ya maadui na analitaja hilo kuwa ni sababu ya ushindi.

Sababu ya tano: Kukosekana maandalizi ya kijeshi: Akinukuu aya isemayo: “Waandalieni kadiri ya mnavyoweza nguvu…” alisema kuwa; kukosa maandalizi ya kijeshi na nguvu za kujihami ni hatari kwa mataifa.

Sababu ya sita: Udhaifu katika uhusiano na uongozi: Alisema: Udhaifu katika mawasiliano na utiifu kwa uongozi ni sababu nyingine ya kushindwa. Leo uongozi wetu umejidhihirisha kwa kiongozi mwenye hekima, mpambanaji na mwenye busara, ambaye kila neno lake huleta uhai, hujenga jamii na kuanzisha harakati. Kujitenga na mhimili huu wa uongozi ni hatari nyingine.

Sababu ya saba: Udhaifu katika imani na msaada wa Mwenyezi Mungu: Alisema: Mwenyezi Mungu katika Aya ya 173 ya Aal ‘Imran anasema: “…Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni Mtegemewa bora.”

Imani na kusimama imara; sharti la kwanza la ushindi

Alisisitiza kuwa; sharti la kwanza la ushindi katika jamii ya waumini ni kumwamini Mwenyezi Mungu na kusimama imara katika njia Yake. Mwenyezi Mungu katika Aya ya 126 ya Aal ‘Imran anasema:
“Na msaada hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hekima.”

Alitahadharisha Wapiga porojo wajue kwamba; Iran ni nchi ya Uislamu, Ramadhani na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, na haitainama mbele ya maadui wa uhuru wa kujitegemea.

Kisha akanukuu aya isemayo: “Ikiwa mtavumilia na mkamchamngu na hata maadui wakikutokeeni kwa ghafla, basi hapo Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa Malaika elfu tano wanao shambulia kwa nguvu.”
na kusema kuwa Qur’ani inasema ikiwa mtakuwa na subira na msimamo, Mwenyezi Mungu atawatuma malaika kuwasaidia. Msiruhusu udhaifu kuingia ndani yenu.

Masharti ya ushindi na kuvuka hatari

Alizitaja nguzo hizi kuwa:
1- Kumuamini Mwenyezi Mungu;
2- Utambuzi na uchambuzi sahihi;
3- Umoja na mshikamano;
4- Utiifu kwa uongozi;
5- Ujasiri na kutokuogopa;
6- Azma, msimamo na subira;
7- Maandalizi ya kijeshi.

Akilihutubia taifa la Iran alisema: Mtumainini Mwenyezi Mungu. Maadui ni dhaifu na wanyonge. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu taifa hili litawashinda maadui, na njia ya Muqawama huko Palestina, Iraq, Lebanon na Yemen na ulimwengu wa Kiislamu na Iran itaendelea kwa fahari.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha