Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Mousavi — ambaye pia ni mwalimu mashuhuri ndani ya hawza ya elimu ya dini ya Najaf — alisisitiza kuwa, hali ya sasa ya eneo inaonyesha “msisimko wa kijeshi na kisiasa usio na mfano.” Akiielezea hali iliyopo kama mabadiliko ya mpangilio wa bao kikanda,” alibainisha kuwa; matukio yanayoendelea si ya ghafla, bali ni sehemu zinazoungana za mradi mpana wa kurekebisha mizani ya nguvu.
Alisema: Dhana ya kwamba mabadiliko ya kisiasa hutokea bila kuhusiana na muktadha wa kikanda na kimataifa ni mtazamo mwepesi unaojaribiwa kupandikizwa katika fikra za umma. Kwa mujibu wake, kutenganisha masuala kwa njia ya bandia na kuyajadili nusu nusu kunalenga kuishughulisha jamii na mambo ya pembeni na kuifanya ipuuze mabadiliko makubwa.
Ayatollah Mousavi aliongeza kuwa; baadhi ya mikondo ya vyombo vya habari ima haina uchambuzi sahihi wa kisiasa au hufanya kazi ndani ya ajenda zinazolinda maslahi ya wahusika wa nje.
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad akirejelea pia taarifa kuhusu kuhamishwa kwa watu elfu tano wa wanachama wa ISIS kutoka Hasakah kwenda Iraq, alisema; hatua hiyo imefanyika sambamba na ripoti kuhusu mipango ya Marekani ya kuandaa upya uwanja wa Syria na kuandaa mazingira ya harakati za baadhi ya pande.
Alionesha wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuwaweka watu hao katika kambi ndani ya Iraq, huku akisisitiza kuwa suala hilo haliwezi kuchambuliwa nje ya mfumo mpana wa usalama.
Ayatollah Mousavi pia alirejelea kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani kutoka katika kambi ya al-Tanf na kuikabidhi kwa kundi la al-Julani, akasema; kambi hiyo ina nafasi ya kimkakati katika mlinganyo wa pembetatu ya Syria–Iraq–Jordan.
Aliuliza ni kwa lengo gani uhamishaji huo wa wanajeshi wa Marekani umefanyika, na akataja uwezekano wa kuhamishiwa ndani ya Iraq au kaskazini mwa nchi hiyo. Aliongeza kuwa; harakati hizi zinaashiria zaidi upangaji upya wa kijeshi kuliko kujiondoa.
Ayatollah Mousavi aliunganisha pia mabadiliko haya na kuchelewa kwa uchaguzi wa rais wa Iraq, huku akisema; kusimama kwa michakato ya kikatiba hakutenganishwi na hali ya mvutano wa kikanda.
Alibainisha kuwa; uteuzi wa waziri mkuu kwa mujibu wa katiba unategemea kwanza kuchaguliwa kwa rais, na kuhusisha mgogoro huo na baadhi ya mikondo ya kisiasa kabla ya kutatuliwa kwa suala hilo ni operesheni ya vyombo vya habari ya kupotosha fikra za umma.
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad alizungumzia pia misimamo ya karibuni ya Turkey kuhusu Iraq, huku akisema; inaweza kueleweka ndani ya muktadha wa mabadiliko yanayoendelea katika eneo na inaonyesha kuwa Iraq si nje ya mchakato wa kuchorwa upya kwa maeneo ya ushawishi.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatollah Mousavi alizungumzia mvutano kati ya Marekani na Iran, huku akisema; vitisho vya karibuni vya Washington havijafanikiwa kuunda muafaka wa kikanda dhidi ya Tehran.
Aliongeza kuwa baadhi ya nchi zinazohifadhi kambi za kijeshi za Marekani zimetangaza kwamba, kulengwa kwa kambi hizo hakutachukuliwa kama uvamizi wa mamlaka yao, bali kama sehemu ya makabiliano kati ya Washington na Tehran. Kwa mtazamo wake, hali hii imebadilisha mizani ya uzuiaji wa kijeshi na kufanya mahesabu ya Marekani kuwa magumu zaidi.
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad alisisitiza kuwa, kwa mujibu wa msimamo uliotangazwa na Iran, mazungumzo yanayoendelea yanahusu tu suala la nyuklia, na mada kama uwezo wa makombora au ushawishi wa kikanda hazimo katika ajenda.
Ayatollah Mousavi alitathmini tofauti za mitazamo ndani ya serikali ya Marekani pamoja na shinikizo la utawala wa Kizayuni kuwa ni ishara ya mvutano wa ndani kuhusu namna ya kusimamia faili hilo.
Mwishoni, aliitaka mikondo ya kisiasa ya Iraq kuimarisha mshikamano wa ndani na kutegemea uwezo wa wananchi ili kuwa tayari kwa mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea.
Akinukuu kanuni ya Qur’ani isemayo: “Na waandalieni nguvu kadiri mwezavyo”, alisisitiza kuwa; kutegemea kujisalimisha au maridhiano ya moja kwa moja si dhamana ya kuilinda nchi; bali uelewa wa umma, umoja wa kitaifa na nafasi ya uongozi wa kidini ni nguzo kuu za kuilinda Iraq.
Katika hitimisho la hotuba yake, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad, alibainisha kuwa licha ya changamoto, Iraq ina uwezo wa nguvu na ustahimilivu, na hakuna mradi wa kigeni unaoweza kulazimisha matakwa yake juu ya nchi hiyo wakati wananchi wana uangalifu na taifa lina mshikamano.
Maoni yako