Shirika la Habari la Hawza, Katika fikra za Qur'ani Tukufu, imani imefungamana na heshima na utukufu ('izza), na katika msamiati wa Qur'ani hakuna nafasi kwa Muislamu aliyeingiwa na hofu na udhaifu. Mapambano kati ya safu ya imani na safu ya ukafiri ni sunnah isiyobadilika; kwa sababu ukafiri kwa asili yake unapinga kudhihiri kwa Uislamu halisi, na hutumia uwezo wake wote kujaribu kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu (ijapokuwa nuru ya Mwenyezi Mungu haiwezi kuzimwa). Katika uwanja wa mapambano kama huu, kunyamaza, kulegea na kuwaogopa maadui si "tahadhari" hata kidogo, bali ni kutoka katika njia ya tauhidi.
Qur'ani Tukufu, katika kuonesha sura ya muumini, inatoa ufafanuzi wa kimkakati kuhusu 'amali njema', ambao katika msongamano wa tafsiri finyu za leo kuhusu muumini, umesahaulika:
«لَا یُصِیبُهُمْ ظَمَأٌ وَلَا نَصَبٌ وَلَا مَخْمَصَةٌ فِی سَبِیلِ اللَّهِ وَلَا یَطَئُونَ مَوْطِئًا یَغِیظُ الْکُفَّارَ وَلَا یَنَالُونَ مِنْ عَدُوٍّ نَیْلًا إِلَّا کُتِبَ لَهُمْ بِهِ عَمَلٌ صَالِحٌ.»
Hakiwapati kiu, wala uchovu, wala njaa, kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawendi mahali panapo waghadhibisha makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na maadui, ila huandikiwa kuwa ni kitendo chema.
(Suratu Tawbah, Aya ya 120)
Katika uchambuzi wa sasa wa jamii za Kiislamu, 'amali njema' mara nyingi imepunguzwa na kuhusishwa tu na ibada za mtu binafsi (Swala, Saumu, Zaka na mfano wake). Lakini kwa mujibu wa mantiki ya aya hii, kuwaghadhibisha maadui wa Mwenyezi Mungu yenyewe ni 'amali njema ya msingi; na hicho ndicho kiini ambacho kutokukielewa ndiko kulikousukuma Umma wa Kiislamu katika hali ya udhaifu na kutokuwa na msimamo katika kipindi chote cha historia.
Ili kuelewa zaidi 'amali njema' iliyotajwa katika aya hii, turejee katika Suratul-'Asr:
«وَالْعَصْرِ. إِنَّ الْإِنْسَانَ لَفِی خُسْرٍ. إِلَّا الَّذِینَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ.»
Naapa kwa zama. Hakika mwanadamu yumo katika hasara. Isipokuwa wale walioamini, wakatenda mema, wakausiana kushikamana na haki, na wakausiana kusubiri na kustahimili.
Ikiwa tutayachukulia maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Suratul-'Asr kuwa ndio mizani ya kupima uokovu, tutafahamu kwamba kutoka katika hasara ya milele kunawezekana tu kwa imani, ambayo miongoni mwa sifa zake muhimu kabisa ni 'amali njema'. Kwa mtazamo wa Qur'ani, miongoni mwa vitendo vinavyohesabiwa kuwa 'amali njema' na vinavyomtoa mtendaji wake katika safu ya wenye hasara, ni kupiga hatua katika njia inayowaghadhibisha makafiri.
Aya hii inayozungumziwa ni ukweli wa kimkakati ambao Umma wa Kiislamu unapaswa kuurejea ikiwa unataka kujinasua kutoka katika minyororo ya ukoloni na udikteta. Kughafilika na msingi huu hakusababishi tu hasara za kimwili na kiroho, bali pia husababisha kupotoshwa na kufutika kwa utambulisho wa Kiislamu.
Kwa mantiki ya Qur'ani, Muislamu dhaifu, asiye na msimamo na mwoga hastahili kuwa katika kiwango cha askari wa safu ya haki; kwa sababu utukufu ('izza) ni wa Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na Waumini. Hivyo basi, kila harakati inayofanywa katika safu ya haki ambayo haiwakasirishi maadui wa dini ya Mwenyezi Mungu, uhalali wake wa kimapinduzi na wa kiimani unapaswa kutiliwa shaka.
Mustafa Amini
Maoni yako