Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Dkt. Khaled Qaddoumi, mwakilishi wa Harakati ya muqawama wa Kiislamu wa Palestina (Hamas) ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ya Alhamisi katika kongamano la mtandaoni lenye kichwa cha habari kisemachi “Madrasa ya Soleimani; Busara ya muqawama na Mustakabali wa Safu ya Haki”, huku akiitukuza kumbukumbu ya mashahidi wa safu ya muqawama—hasa shahidi Jenerali Haj Qassem Soleimani—alisisitiza: Haj Qassem Soleimani hakuwa tu shujaa wa ulimwengu wa Kiislamu, bali pia shujaa wa ubinadamu, na alama ya utetezi wa utu, umoja wa Umma, na muqawama dhidi ya Uzayuni na misimamo mikali.
Qaddoumi alisema: Tumekusanyika katika siku hizi kuenzi kumbukumbu ya mashahidi wakubwa, hasa Shahidi wa Quds, kamanda mujahid Haj Qassem Soleimani; mtu ambaye katika eneo zima alitambuliwa kama ndugu mkubwa na mshirika mwaminifu.
Akitaja mwitikio wa adui Mzayuni baada ya kuuawa kishahidi kwa Soleimani, aliongeza: Sherehe na furaha za adui Mzayuni baada ya shahada ya Haj Qassem, zenyewe ni ushahidi bora kabisa kwamba walimlenga mtu aliyekuwa ameipa miradi ya Uzayuni mapigo mazito na ya kudumu, na aliyetoa huduma kubwa kwa usalama wa eneo na kwa lengo la Palestina.
Mwakilishi wa Hamas nchini Iran, katika kufafanua mtazamo wa shahidi Soleimani kuhusu suala la Palestina, alisema wazi: Kwa mtazamo wa Haj Qassem, kuiunga mkono Palestina halikuwa chaguo la kisiasa, bali jukumu la kimungu na la kibinadamu. Alisisitiza daima kwamba kuitetea Palestina ni wajibu ambao watu wote huru duniani—bila kujali dini, madhehebu au utaifa—wanawajibika nao; na leo tunaona kuwa mataifa mbalimbali, hata yasiyo ya Kiarabu na yasiyo ya Kiislamu, yamesimama pamoja na watu wa Palestina.
Qaddoumi aliutaja “umoja wa Umma wa Kiislamu” kuwa ni mhimili wa pili wa fikra za shahidi Soleimani na akasema: Palestina ni suala jumuishi na linalounganisha. Haj Qassem alisisitiza daima kuimarisha mahusiano kati ya mataifa na madhehebu yote ya Kiislamu katika muktadha wa kuiunga mkono Palestina, na alipendekeza kwamba, Shia na Sunni, Waarabu na Wasiokuwa Waarabu, wasimame katika safu moja mbele ya adui wa pamoja—yaani utawala wa Kizayuni. Aliamini kwamba Palestina ni Qibla na mhimili wa umoja wa Umma.
Akitaja mabadiliko ya miaka ya karibuni, alibainisha: Ingawa katika muongo uliopita Umma wa Kiislamu ulikumbwa na fitna za kimadhehebu na migogoro ya ndani, lakini Dhoruba ya Al-Aqsa ilirudisha tena umoja wa damu, juhudi na dira ya Umma, na ikaonesha kwamba adui wa kweli ni utawala wa Kizayuni, na kwamba njia sahihi ni njia ya muqawama na mshikamano.
Mwakilishi wa Harakati ya Hamas nchini Iran alitaja nguzo ya tatu ya fikra za shahidi Soleimani kuwa ni “kushikamana na muqawama”, na akasema: Leo baadhi ya watu wanazungumzia kunyang’anywa silaha na kuachana na upinzani, ilhali uzoefu wa kihistoria umethibitisha kuwa lugha pekee ambayo utawala wa Kizayuni unaielewa ni lugha ya muqawama, —kwa vipengele vyake vyote, iwe kijeshi, kisiasa, kihabari au kijamii—ni haki halali ya mataifa yaliyo chini ya ukaliaji; na kadiri ukaliaji unavyoendelea, ndivyo muqawama nao utaendelea.
Akilaani aina yoyote ya kuhalalisha au kurekebisha uhusiano (normalization) na utawala wa Kizayuni, aliongeza: Kujipatanisha na kusalimu amri si kosa la kisiasa tu, bali ni upotofu wa kimaadili na kibinadamu; kwa sababu badala ya kumuadhibu mkoloni aliyetiwa doa la damu ya watoto na wanawake, humpa u-halali. Hali hii ni wakati ambao leo hata mataifa ya Magharibi katika mitaa ya Marekani na Ulaya yanafanya maandamano dhidi ya uhalifu wa Wazayuni na yanadai kuvunjwa kwa mahusiano ya serikali zao na utawala huu haram.
Qaddoumi, mwishoni, alisisitiza: Lau asingekuwapo Haj Qassem Soleimani, haijulikani misimamo mikali ya Kizayuni na ugaidi wa takfiri vingesababisha maafa makubwa kiasi gani kwenye dini na makabila mbalimbali katika eneo hili ambalo ni chimbuko la dini za mbinguni. Leo, dini zote, madhehebu yote na mataifa yote huru duniank, yanajiona yana deni juu ya damu ya shahidi huyu mkubwa.
Maoni yako