Jumamosi 3 Januari 2026 - 23:00
Sheikh Ahmad Qablan aikosoa vikali Serikali ya Lebanon

Hawza/ Hujjatul-Islam Sheikh Ahmad Qablan, Mufti Mkuu wa Jaafari wa Lebanon, amesema: “Tumejikuta katikati ya nchi ambayo inaendelea kuporomoka kila siku.”

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Ahmad Qablan, Mufti Mkuu wa Jaafari wa Lebanon, katika mnasaba wa kuingia Mwaka Mpya wa Miladi, alitoa ujumbe akiwahutubia wananchi wa Lebanon na kusema: Kwa kuwa tupo mwishoni mwa mwaka mmoja na mwanzoni mwa mwaka mpya, na tumejikuta katikati ya nchi ambayo inaendelea kuporomoka mfululizo, huku muundo wake wa kihistoria ukikabiliana na migogoro mizito ya kisiasa, ya mamlaka na ya kifikra, ninaona ni wajibu wangu kuvuta hisia za vituo vya mamlaka, hususan taasisi rasmi za nchi, kwamba tunaishi katika wakati wa kifo cha kitabibu (clinical death), hasira za kijamii, kisiasa na kimaisha, pamoja na migogoro ya wazi ya kimataifa na ya kijeshi.

Aliongeza: Leo, uhalisia wa nchi unakabiliana na hali ya kuendelea kwa sura bila maudhui na misimamo mitupu; migogoro inayolenga misingi ya kitaifa na mwelekeo wa jadi na wa kisiasa wa Lebanon. Hali hii imetuweka katikati ya mlingano unaothibitisha kuporomoka na kuiacha nchi kuelekea kusikojulikana. Tatizo la kutisha ni kwamba mamlaka iliyopo, isiyo na maana wala mizizi, imezama katika ukaidi wa maradhi; haina uamuzi wa kitaifa, haina mageuzi ya kiutawala au ya kimaisha, wala haina dhamira yoyote ya kuijenga upya nchi au kuokoa vipaumbele vyake vya msingi.

Sheikh Qablan pia alibainisha: Leo tunaishi katikati ya serikali isiyofanya kazi, mwili wa kiutawala usio na faida, timu ya kazi isiyo na kazi, na kundi la mawaziri wasio na uwezo; ilhali raia wa Lebanon ndiye mwathirika mkubwa wa mkanganyiko huu. Familia ya Lebanon na thamani inayodhamini mradi wa kitaifa imepata hasara kubwa zaidi, na kutoaminiana kisiasa na kitaifa kumeenea kiasi cha kumeza hata chembe zilizobaki za imani.

Akiashiria kwamba kinachohitajika ni kuwatumikia wananchi na kutekeleza wajibu wa kitaifa kabla ya mlipuko kamili—kwa sababu hatari ya kweli haiko katika kushindania viti bali katika kusimamishwa kwa makusudi taasisi za kitaifa na mamlaka—alisisitiza: Tatizo si pengo la kikatiba, bali ni pengo la kisiasa lililogeuzwa kuwa chombo cha kusimamisha, kudanganya na kupindua vipaumbele ili kuunda mizani ya bandia kwa mujibu wa maagizo ya nje yanayonufaika na uharibifu. Matokeo yake, serikali imeachwa bila mwelekeo na bila uwezo halali; na hapa mgogoro mkuu ni pengo la makusudi na uongozi unaoivuta serikali kuelekea kushindwa kwa jumla.

Kiongozi huyu wa Kiislamu wa Kishia wa Lebanon, akisisitiza kwamba hakuna nchi inayoweza kujengwa bila mageuzi na uongozi wa kitaifa wenye mamlaka, na kwamba Lebanon leo haina muundo, haina uwajibikaji, haina mahakama huru, haina vyombo vya udhibiti vinavyofanya kazi, wala haina mipango ya mshikamano wa kitaifa, alisema: Mageuzi maana yake ni mabadiliko, lakini hakuna mabadiliko yanayotokea, ilhali nchi imezama katika ufisadi wa kisiasa na kifedha—hasa katika suala la kubebesha raia wa Lebanon gharama za kufilisika kifedha ili kuridhisha Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF).

Aliendelea: Haya yote yanatokea katika hali ambayo serikali haijabeba gharama yoyote ya haki ya kisiasa au kifedha, haijamwajibisha mtu yeyote licha ya ukubwa wa janga, na haijamuuliza yeyote; hata waliokamatwa waliachiliwa, kiasi kwamba kushindwa hakuhitaji tena uhalalisho.

Mufti Qablan akaongeza: Kinachohitajika ni kuipa nchi thamani ya kivitendo, si kuendesha magurudumu tasa ya mamlaka. Maslahi ya umma ndiyo yanayopaswa kuendeshwa, si kupoteza muda na kusimamisha mambo, kwa sababu mfumo wa jumla wa nchi uko hatarini. Uokozi unawezekana tu kupitia mipango na sera za kitaifa, mbali na roho ya kulipiza kisasi na orodha za kigeni zinazopelekea kuharibiwa Lebanon.

Hatari kubwa ni kwamba serikali haitaki kucheza jukumu lake kuu

Alisisitiza kuwa: Kwa masikitiko, raia wa Lebanon yuko nje ya hesabu za serikali; hana ulinzi wa kijamii, hana dhamana za afya, elimu au msaada, wala hata uhifadhi wa misingi ya haki za msingi. Hakuna kitu hatari zaidi kuliko kuzoea kuporomoka na kukubali kama hatima ya kitaifa.

Mufti wa Jafaria wa Lebanon alisisitiza: Kinachohitajika ni mamlaka ya Lebanon, si miamala ya kimataifa. Hatari kubwa ni kwamba serikali haitaki kutekeleza jukumu lake la msingi, hususan katika maeneo ya kusini, Bonde la Biqaa na Dahieh. Licha ya misimamo yake mikali na kelele katika masuala ya ndani, serikali haijarejesha mamlaka yake wala haina nia ya kuyarejesha, hasa kusini mwa mto; na kwa kuhofia  tishio la Kizayuni, imekuwa hata isiyojali kuuawa kwa watu na raia wake wenyewe, wala haioni hilo kama kipaumbele cha kitaifa.

Hakuna serikali yoyote Lebanon iliyozoea kushindwa kama serikali hii

Sheikh Qablan, akisisitiza kwamba; uamuzi wa kisiasa ama haupo au umejikita katika magamba ya juu juu, na kwamba mchezo wa unyonge na ubinafsi umefikia kilele chake—kiasi kwamba hakuna serikali yoyote Lebanon iliyozoea kushindwa kama serikali hii—alisema: Hali hii inatishia dhana yenyewe ya dola. Kwa msingi huo, mwaka 2025 ulikuwa mwaka wa maafa katika ngazi ya mamlaka na ya kitaifa, kwa sababu mamlaka iliyopo haitaki kutekeleza jukumu la mdhamini wa kitaifa, wala hata haitaki kujiokoa yenyewe; ilhali haiwezekani kupuuza masuala ya kitaifa, migogoro yenye mizizi na maamuzi ya hatima.

Hakuna mbadala wa jeshi na muqawama

Aliendelea kusema: Ili kuiokoa Lebanon, ni lazima kubainisha aina na kina cha migogoro, hususan migogoro ya mamlaka, kwa sababu Lebanon iko hatarini na haina mdhamini wa kweli isipokuwa dola imara kutoka ndani, yenye mamlaka ya kitaifa na uwezo wa kimkakati wa kimuungano, mbali na orodha za kimataifa. Vipaumbele ni vingi, miongoni mwavyo ni jeshi na muqawama kama dhamana ya mamlaka ya kitaifa, na hakuna mbadala wa jeshi na muqawama.

Sheikh Qablan, akisema kwamba silaha iliyoiweka huru Lebanon na kulinda uwepo wake kwa miongo kadhaa haiwezi kuondolewa, na kwamba kukana ukweli huu ni usaliti, akasema: Hatutaisaliti Lebanon. Macho yote yanatazama mshtuko mkubwa wa kisiasa ili kuzalisha upya Lebanon yenye nguvu na uhai, na matumaini yanaelekezwa kwenye uchaguzi wa bunge kama fursa ya kuimarisha mamlaka ya Lebanon. Nguvu za kisiasa zinapaswa kuitikia kwa sauti ya kitaifa na ya pamoja inayolingana na kiwango cha hatari zinazoitishia Lebanon.

Kiongozi huyu wa Kishia wa Lebanon alihitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza: Mwaka 2026 utakuwa mwaka wa hatima, na thamani ya kitaifa ya Lebanon inatokana na uchaguzi wake wa serikali ya kitaifa. Bila dola ya kitaifa yenye mamlaka, Lebanon iko katika migogoro hatari zaidi ya kimaisha.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha