Jumanne 30 Desemba 2025 - 22:30
Kinachopangwa kwa ajili ya Lebanon ni zaidi ya suala la silaha na kinaelekezwa kwenye mkondo wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi

Hawza/ Ali Fayyadh alisema: Hizbullah ni chama kikubwa zaidi cha kisiasa kwa kuzingatia uungwaji mkono wa wananchi nchini Lebanon, na uzito pamoja na nafasi yake haviwezi kupuuzwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kwa lengo la kuheshimu damu safi zilizomwagika na kudhihirisha uaminifu kwa kujitolea kulikofanywa kwa ajili ya kuilinda heshima ya taifa na watu wake, Hizbullah iliandaa hafla ya kumbukumbu ya shahidi mtukufu Muhammad Ibrahim Alaauddin, anayejulikana kwa jina la “Abu Ali Murtadha”, katika mji wa Majdal Salm. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Ali Fayyadh, mjumbe wa Muqawama Bungeni, familia ya shahidi, familia za mashahidi wengine, wanazuoni wa dini, wanaharakati na watu mashuhuri wa kijamii, pamoja na kundi la wakazi wa mji huo na vijiji jirani.

Hafla ilianza kwa usomaji wa aya za Qur’ani Tukufu, kisha Ali Fayyadh akatoa hotuba kwa niaba ya Hizbullah, akisisitiza kwamba; hatua ya sasa inahitaji subira, hekima, uthabiti na ujasiri; kwa sababu hatari zinazolikabili taifa la Lebanon, pamoja na ukubwa wa malengo na mipango inayoendeshwa na Waisraeli na Wamarekani dhidi ya nchi, ni kubwa na zenye hatari.

Fayyadh, akieleza kuwa mhimili mkuu wa mashinikizo haya ni kunang'anywa silaha Muqawama, alibainisha kuwa; suala hilo linazidi mipaka ya silaha pekee, bali linaelekea katika mkondo wa kisiasa, kiusalama na kiuchumi ambao unaipeleka nchi katika nafasi mpya, kubadilisha utambulisho wake wa kisiasa, kuvuruga mizania ya ndani, kuiweka chini ya udhibiti wa kigeni, kunyakua mamlaka ya usalama ya Lebanon, na kuiingiza katika mtandao wa maslahi ya kiuchumi ya kikanda unaojengwa juu ya ushirikiano na adui katika sekta ya gesi na mafuta.

Mjumbe wa Muungano wa Uaminifu kwa Muqawama alisema: Kwa bahati mbaya, huku ni kurejea makosa ya zamani ambayo yaliizamisha Lebanon katika hali ya vurugu, kutokuwa na utulivu na changamoto hatarishi; mambo ambayo yanapuuza hali nyeti na dhaifu ya muundo wa kijamii wa Lebanon, ilhali kulinda muundo huo kunahitaji kujiepusha na mielekeo mikali na isiyopatana na maslahi ya taifa.

Mwakilishi wa Hizbullah aliongeza: Kinyume chake, Hizbullah inataka mpango ulio wa wastani zaidi, wa uhalisia na wa uwajibikaji; mpango unaosisitiza kushikamana na Azimio la Kimataifa namba 1701, kutangazwa kwa kusitisha mapigano, kuondoka kwa majeshi ya Israeli, kusitishwa kwa vitendo vya uadui, kuanza upya ujenzi, kuachiliwa kwa wafungwa, na kisha kuanzishwa kwa mkondo wa kurekebisha hali ya kiuchumi na kijamii pamoja na mageuzi ya kisiasa. Pia mpango huu unaweka mbele mjadala kuhusu mkakati wa kitaifa wa ulinzi, unaoendana na hali halisi na mahitaji ya Lebanon katika kulinda ardhi na mamlaka yake.

Alisisitiza kuwa: Mwelekeo wa asili wa kisiasa na kiuchumi wa Lebanon ni mazingira ya Kiarabu na Kiislamu ya eneo hili, ambayo nchi inapaswa kujenga upya uhusiano wake nayo na kuyadumisha kwa njia bora zaidi, kwa msingi wa kuheshimu mamlaka ya kila nchi na kutokuingilia masuala ya ndani.

Ali Fayyadh, mwishoni mwa hotuba yake, huku akisisitiza kwamba wote wanapaswa kukumbuka kuwa; Hizbullah ni chama kikubwa zaidi cha kisiasa kwa misingi ya uungwaji mkono wa wananchi nchini Lebanon, na kwamba uzito na nafasi yake haviwezi kupuuzwa, alisema: Vigezo vya mkataba wa kitaifa na demokrasia vinataka kuwepo kwa makubaliano na maelewano na Hizbullah. Kwa msingi huo, tunaamini kuwa Lebanon iko katika njia panda ya kihistoria, na Hizbullah inawaita wote kushirikiana kwa ajili ya kuokoa mamlaka ya nchi, kuanzisha mchakato wa urekebishaji na uimarishaji, kudumisha utulivu, na kuijenga dola.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha