Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Papa katika hotuba yake ya Krismasi alieleza masikitiko yake juu ya mateso na shida kubwa wanazokumbana nazo wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza.
Papa Leo wa Kumi na Nne aliwauliza watu akisema: “Je, tunawezaje kutozifikiria mahema ya watu wa Ghaza katika baridi hii kali, Ghaza ambayo kwa wiki kadhaa imekuwa ikikabiliwa na mvua, upepo, mazingira mabaya ya hali ya hewa na baridi inayopenya hadi kwwnyw mifupa?”
Kauli hizi za Papa zinatolewa katika hali ambayo makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Harakati ya Hamas yalitekelezwa Oktoba iliyopita, baada ya miaka miwili ya mabomu makali na oparesheni za kijeshi zilizohusisha mauaji ya watoto na raia. Hata hivyo, mashirika ya kibinadamu yanasema kuwa; misaada inayofika Ghaza ni midogo sana ikilinganishwa na hali yake mbaya kupita kiasi. Aidha, Israel pia inaweka vikwazo na matatizo katika njia ya kupitisha misaada hiyo.
Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa Israel kwa uungwaji mkono wa Marekani na Ulaya, umefanya kile kinachoelezwa kuwa ni mauaji ya halaiki kamili katika Ukanda wa Ghaza, yakiwemo mauaji ya wananchi, njaa, uharibifu, uhamishaji wa watu, pamoja na kukamatwa na kuwafunga watu. Utawala huu unaomwaga damu umekuwa ukipuuza mara kwa mara maombi ya kimataifa na maagizo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ya kusitisha vitendo hivyo, na umeendelea na mashambulizi yake.
Chanzo: Kituo cha Habari cha Palestina
Maoni yako