Jumanne 9 Desemba 2025 - 19:45
Da‘wa (Tabligh) ni Kukumu la Kwanza la Wanazuoni wa Hawza

Hawza/ Ayatullah Nouri Hamadani amesisitiza kuwa: jukumu la kwanza kabisa la wanazuoni wa Hawza ni kutekeleza kazi ya da‘wa (tabligh). Matunda ya juhudi zote yanajikusanya katika jukumu hili; yaani tangia siku ya kwanza ya kuingia Hawza hadi katika dakika za mwisho, katika hatua na ngazi zote za kawaida za Hawza, jukumu la da‘wa halijawahi kumwondokea mtu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Nouri Hamadani katika ujumbe wake kwenye hafla ya kufunga Tamasha la Ubunifu wa Kida‘wa la Jannaat, alisisitiza juu ya kuunga mkono maendeleo na uenezi wa shughuli za da‘wa, kuinua hadhi ya da‘wa miongoni mwa wanazuoni wa Hawza, pamoja na kutoa motisha na kugundua vipaji vya walinganiaji.

Matini kamili ya ujumbe wa Mtukufu huyo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

بسْمِ اللَّهِ الرَّحْمنِ الرَّحیمِ

الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِینَ وَ الصَّلَاةُ وَ السَّلَامُ عَلَی سَیِّدِنا وَ نَبِیِّنَا أَبِی ‌الْقَاسِمِ المصطفی مُحَمَّد وَ عَلَی أهلِ بَیتِهِ الطَّیِّبِینَ الطَّاهِرِینَ سیَّما بَقیَّهَ اللهِ فِی الأرَضینَ و لعنة الله علی أعدائهم أجمعین إلی یوم الدین.

الَّذِینَ یُبَلِّغُونَ رِسَالَاتِ اللَّهِ وَیَخْشَوْنَهُ وَلَا یَخْشَوْنَ أَحَدًا إِلَّا اللَّهَ وَکَفَی بِاللَّهِ حَسِیبًا

“Wale wanaofikisha jumbe za Mwenyezi Mungu, wanamuogopa Yeye, wala hawamuogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mwenye kufanya hesabu.”
(Surat: Ahzab, aya: 39).

Salamu na heshima njema ziuendee mkutano huo mtukufu:
Leo moja ya majukumu ya Hawza ni suala la da‘wa, na huenda jukumu la kwanza kabisa la wanazuoni ni utekelezaji wa kazi ya da‘wa. Matunda ya juhudi zote yanaishia katika jambo hili; yaani tangu siku ya mwanzo ya kuingia Hawza hadi katika nyakati za mwisho, katika hatua na ngazi zote za kawaida za Hawza, dhamana ya da‘wa haimuondokii mtu kamwe.

Kwa msingi huu, ni lazima kuzingatia ni nini kifanyike ili jukumu hili lilete na matunda. Mimi, kwa kuzingatia masuala ya wakati, maendeleo ya mitandao ya kijamii, na mabadiliko katika mbinu za da‘wa au kuibuka kwa mazingira mapya ya ulinganiaji, bado ninaamini katika da‘wa ya kimila; yaani da‘wa ya ana kwa ana, au kwa maneno mengine, kazi ya mimbar.

Ninaamini kwa dhati kuwa hakuna mbinu yenye athari zaidi kuliko aina hii ya da‘wa; ingawa sikatai kabisa athari kubwa ya mbinu mpya za da‘wa kama kuwepo katika mitandao ya kijamii, kurekodi klipu, kutengeneza vipindi vya kuvutia vya picha na mengineyo, kwa kuwa hali iliyopo katika jamii inaonesha wazi athari ya aina hii ya ulinganiaji pia. Hata hivyo, athari pana ya da‘wa ya mtandaoni huenda inatokana na kufifia kwa da‘wa ya kimila na ya ana kwa ana; jambo ambalo linapaswa kuchunguzwa na wataalamu wa fani hii.

Watu wanapaswa kufahamu kwamba da‘wa ni sanaa inayohitaji elimu pana. Leo, kwa mtazamo wa baadhi ya watu, da‘wa huonekana kuwa kazi rahisi zaidi, ilhali da‘wa, hotuba na mimbar ni miongoni mwa kazi ngumu zaidi; na ikiwa tunataka kuwa na athari, basi ni miongoni mwa kazi zenye tabu zaidi.

Mhubiri mwenye athari anapaswa kujifunza kikamilifu na bila upungufu ngazi za juu za taaluma mbalimbali, hususan fasihi ya Kiajemi na Kiarabu. Mhubiri mwenye athari lazima awe mwenye maadili mema na mjuzi wa zama alizo nazo; autangulize kuwatambua wasikilizaji katika hatua ya kwanza ya hotuba; na anufaike na vyanzo vyenye kuaminika. Ajiepushe na kunukuu mambo yasiyo na uthibitisho, na asipoteze muda wa wasikilizaji kwa visa vya kubuni na taarifa zisizojulikana. Aidha, ajiepushe na kauli fulani zisizolingana na hadhi ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), hata kama zimenukuliwa mahali fulani. Afuatilie shubha inayoikabili jamii na ayajibu kwa lafudhi iliyo wazi na kwa hoja zenye uthibitisho. Kwa kisingizio cha kuwa wa kimila, hapaswi kupuuzia masuala ya sasa ya kijamii kama mambo ya kitamaduni, kisiasa na kiuchumi ya watu; bali anapaswa kufikia imani kwamba mnenaji atakuwa sauti iliyo wazi na inayowakilisha pia matatizo ya watu.

Jambo jingine linalopaswa kuzingatiwa ni kwamba; katika suala la da‘wa, kanuni hii inapaswa kusimamiwa kutoka kituo kimoja cha pamoja. Kwa bahati mbaya, leo taasisi nyingi, iwe zinahusiana au hazihusiani, zinaingilia suala la da‘wa, na hili ni tatizo. Kazi hii ni ya kitaalamu; kwa hiyo ni lazima kituo kimoja kichukue dhamana ya jukumu hili ili tuondokane na hali hii ya sasa.

Jambo jingine linalopaswa kupewa umakini ni utaalamu katika nyanja mbalimbali za da‘wa: mhubiri katika anga ya mtandaoni kwa ujumla; mhubiri katika matumizi ya akili bandia; mhubiri wa utengenezaji wa vibonzo (animasheni); mhubiri anayeshughulika na makundi ya watoto na vijana. Bila shaka, Ofisi ya Usimamizi wa Hawza na Ofisi ya Da‘wa tayari zimeanza hatua fulani katika mwelekeo huu, jambo linalotia moyo.

Mwisho, ninasisitiza juu ya kuunga mkono maendeleo na uenezi wa shughuli za da‘wa, kuinua hadhi ya da‘wa miongoni mwa wanazuoni wa Hawza, kutoa motisha, na kugundua vipaji vya walinganiaji. Ninawashukuru waandaaji wote wa mkutano huu ulioheshimiwa, uliofanyika chini ya jina la Tamasha la Ubunifu wa Kida‘wa, na namwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajalie wote taufiki.

8 December 2025
Hussein Nouri Hamedani

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha