Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, serikali ya Javier Milei, katika kipindi ambacho Israel inakabiliwa na wimbi kubwa la ukosoaji wa kimataifa kutokana na mashambulizi yake dhidi ya Ghaza, imezindua rasmi mpango hatari wa “Mikataba ya Is-haq”; mpango unaochochewa na mfano wa “Mikataba ya Abrahamu”, na unaotegemea uundaji wa mhimili wa kisiasa kati ya serikali za mrengo wa kulia barani Amerika ya Kusini na mitandao ya Waevangelisti wanaounga mkono Uzayuni, kwa lengo la kubadili na kufafanua upya nafasi ya Agentina katika mizania ya kisiasa ya kikanda.
“Mikataba ya Is-haq” ilizinduliwa rasmi jijini Buenos Aires, kwa uwepo wa Javier Milei, Rais wa Agntina, na Gideon Sa’ar, Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Israel. Mpango huu wa kisiasa umechota misingi yake kutoka katika “Mikataba ya Abrahamu”; makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2020 kwa uungwaji mkono wa serikali ya wakati huo ya Donald Trump, kati ya Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa lengo la kurasimisha uhusiano wa kawaida.
Mpango huu unatangazwa katika wakati ambao utawala wa Israel, kutokana na vita vya uharibifu na matukio makubwa huko Ghaza, unakabiliwa na hali ya kutengwa na kulaaniwa kwa kiwango kikubwa kimataifa, hususan katika eneo la Amerika ya Kusini. Nchi za eneo hili kama vile Brazil, Colombia, Mexico, Chile na Bolivia zimekemea waziwazi mashambulizi ya Israel dhidi ya ardhi za Wapalestina; baadhi ya hizo kama vile Bolivia, zimekata kabisa uhusiano wa kidiplomasia, huku nyingine zikiutuhumu utawala wa Israel kwa kutenda uhalifu wa kivita.
Katika mazingira haya yenye mvutano mkali, “Mikataba ya Is-haq” inaonekana kwa Israel kama fursa ya kimkakati ya kujijengea upya nafasi yake kupitia serikali zinazolingana nayo kisiasa barani Amerika ya Kusini. Mradi huu, kwa kutegemea mtandao wa serikali za mrengo wa kulia wa eneo hilo pamoja na jumuiya zenye nguvu za Waevangelisti wanaounga mkono Uzayuni, unalenga kuunda mhimili mpya wa ushawishi wa kisiasa na kiutamaduni.
Javier Milei, ambaye tangia siku za mwanzonj za urais wake amechukua mwelekeo tofauti kabisa na asili ya sera za kigeni za Agentina, sasa anaibuka kama kinara wa mpango huu wa kikanda. Sio tu kwamba ameeleza mara kadhaa hadharani mwelekeo wake wa wazi wa kuuunga mkono Uzayuni — hadi kufikia kutoa ahadi kwamba baada ya kumaliza kipindi chake cha urais ataingia rasmi katika Uyahudi — bali pia ametangaza dhamira yake ya kuhamisha ubalozi wa Agentina kwenda mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds (Jerusalem).
Milei hapo awali ameitaja harakati ya Hamas, kuwa ni “ya kigaidi”, na katika hafla rasmi ameshiriki kusoma dua za Kiebrania; hali inayoashiria mabadiliko ya kina katika misingi ya mjadala na mwelekeo wa sera za nje wa Buenos Aires.
Kwa mujibu wa taarifa za serikali ya Agentina, Marekani ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa “Mikataba ya Is-haq”, huku miundombinu yenye nguvu ya mashinikizo ya kisiasa ya Marekani - ikiwemo taasisi kama “American Friends of Isaac Accords” na “Genesis Prize Foundation” — zikiunga mkono wa kifedha na kiutawala kwa mradi huo.
Hatua za awali za mpango huu zinalenga nchi za Uruguay, Panama na Costa Rica; nchi zinazotarajiwa kushirikiana na Israel katika nyanja za usalama, teknolojia na biashara kupitia miradi ya pamoja. Kwa hakika, mpango huu unalenga kuunda muungano wa kimataifa uliounganishwa na simulizi za pamoja kama vile “mapambano dhidi ya ugaidi” na “usalama wa kikanda”, kwa madhumuni ya kuimarisha nafasi na ushawishi wa Israel barani Amerika ya Kusini.
Kwa mtazamo wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, “Mikataba ya Is-haq” si tu kwamba inathibitisha mwelekeo mpya wa sera za nje za Agentina, bali pia inaweza kuyumbisha mizani ya kihistoria ya eneo hilo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikielemea upande wa kuwaunga mkono Wapalestina.
Maoni yako