Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, hafla ya kufunga kongamano la kimataifa lenye anuani: “Haki za Taifa na Uhuru wa Kisheria kwa mujubu wa fikra ya Mtukufu Ayatullah Khamenei” ilifanyika asubuhi ya jana, tarehe 4 Desember, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Shirika la Sauti na Televisheni ya Iran.
Kongamano la kimataifa la Haki za Taifa na Uhuru wa Kisheria kwa mujibu wa fikra ya Mtukufu Ayatullah Mkuu Khamenei lilifanyika likiwa na malengo matatu:
La kwanza, kuchambua upya fikra na mwenendo wa Mtukufu Ayatullah Mkuu Khamenei katika uwanja wa haki za taifa na uhuru wa kisheria;
La pili, kuchora mfumo bora wa haki za taifa na uhuru wa kisheria kwa msingi wa mawazo ya Mtukufu Ayatullah Mkuu Khamenei;
Na la tatu, kuhakikisha kulindwa na kuhifadhiwa haki za taifa na uhuru wa kisheria pamoja na namna ya kuziinua kwa mujibu wa mitazamo na fikra za Mtukufu Ayatullah Khamenei.
Ayatullah Sayyid Mohammad Reza Modarresi Yazdi, mjumbe wa Baraza la Uangalizi, akirejea nafasi ya mashauriano katika Uislamu, alisema: Amirul-Mu’minin Ali (a.s) amesema: “Msijiepushe na kusema ukweli wala kutoa ushauri wa haki.”
Mjumbe wa Baraza la Uangalizi alisema: Kushaurisna ni moja ya misingi ya muhimu katika Uislamu ambayo huchukuliwa kuwa ni nguzo ya uendeshaji wa jamii. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani Tukufu:
“وَ أَمْرُهُمْ شُوری بَیْنَهُمْ”
yaani, mambo ya watu yanapaswa kuendeshwa kwa njia ya kushauriana na ushiriki wao. Hata Mtume Mtukufu (s.a.w.w), ambaye ni akili kamili, aliamrishwa kufanya kushauriana na watu.
Akitaja mifano kutoka kwenye mwenendo wa Mtume (s.a.w.w), alibainisha: Katika vita vya Badr na Uhud, pamoja na kwamba maoni ya Mtume (s.a.w.w) yalitofautiana na ya wengi, ilimradi maoni yao hayakuwa kinyume na hukumu ya wazi ya Mwenyezi Mungu, Mtume aliyakubali maoni ya wengi. Lakini pale ambapo hukumu ya Mwenyezi Mungu ilikuwa wazi na ya lazima, Mtume (s.a.w.w) alitenda kwa mujibu wa amri ya Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Modarresi Yazdi aliendelea kusema: Kwa mujibu wa mwenendo wa watu wenye akili pia, katika kushauriana, maoni ya wengi ndiyo yanakuwa kipimo cha utekelezaji. Katika riwaya kutoka kwa Amirul-Mu’minin Ali (a.s) imeelezwa: “Shaurianeni na wenye maoni, kisha wafuate” – ufuataji huu unamaanisha kufuata maoni ya wengi. Uislamu ni dini ya namna hii; dini inayompa binadamu kiwango cha juu kabisa cha uhuru, na inaweka mipaka kwa ajili ya kulinda uhuru wa kiakili na wenye afya njema wa watu; iwe ni uhuru wa kisiasa, kiuchumi au nyanja nyinginezo.
Akiashiria aya za Qur’ani Tukufu, alikumbushia: Mwenyezi Mungu amesema kuhusiana na Mtume (s.a.w.w) kwamba anawaamrisha watu mema na kuwakataza maovu, na anawahalalishia yaliyo mema na kuharamisha machafu. Mengi ya masharti magumu na vikwazo vilivyokuwa vimewalazimishwa mataifa yaliyotangulia, yameondolewa katika Uislamu.
Hadaa ya wamagharibi juu ya haki za binadamu
Mjumbe wa Baraza la Uangalizi kisha akakosoa madai ya uhuru ya Magharibi kwa kusema: Nchi zinazojitambulisha kama ngome ya uhuru, kwa vitendo hazifanyi chochote ila kuwadanganya watu. Wanauonesha ulimwengu mfano wa bandia wa uhuru, lakini uhalisia ni kitu kingine kabisa. Leo hali ya Syria, Lebanon na Gaza ni ushahidi wazi wa jinsi waliojinasibisha na uhuru walivyoyaweka mataifa haya chini ya mabomu, mzingiro wa kiuchumi na kiu kwa miaka mingi.
Je, huu si ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu?!
Alisema: Taasisi za kimataifa pia kwa kaulimbiu ya haki za binadamu na haki za wanawake, huziwekea shinikizo nchi na mataifa mengine, lakini kivitendo hakuna habari ya kweli ya kuwatetea wanadamu.
Ayatullah Modarresi alisema: Laiti wanazuoni wa chuo na wa hawza wangezikosoa kielimu hoja hizi, wakawaelewesha watu ukweli. Lengo la kufanyika kwa makongamano kama haya pia ni ili jamii iende mbele kwa uelewa na maarifa, ili madhalimu na waporaji wasiweze kutumia vibaya hali hiyo.
Katika kuendelea na maelezo yake kuhusu falsafa ya hukumu za Kiislamu, alisema: Iwapo Uislamu umeweka mipaka kuhusiana na halali na haramu, biashara haramu au ulazima wa kuhifadhi hijabu kwa wanawake, hilo si kwa nia ya kufanya ugumu; bali ni kwa ajili ya kulinda uhuru wa kweli. Msingi wa dini umejengwa juu ya wepesi, na Mwenyezi Mungu anawatakia waja wake wepesi.
Wanawake wanaohifadhi hijabu yao huilinda heshima yao
Alisisitiza kuwa: Wanawake wanaohifadhi hijabu zao, kihakika huilinda uhuru na heshima yao, na hujiepusha na utumwa wa matamanio na macho maovu. Vivyo hivyo, wanaume kwa kuhifadhi mipaka ya Mwenyezi Mungu hujipatia kheri ya dunia na Akhera.
Akiwekea mkazo juu ya nafasi ya taqwa katika afya ya mtu binafsi na jamii, alisema: Taqwa ni sababu ya kumkomboa binadamu kutoka katika utumwa wa chochote kile kisichokuwa Mwenyezi Mungu. Kheri ya dunia na Akhera hupatikana tu katika kivuli cha taqwa, na bila taqwa, hakuna kheri atakayopata mwanadamu.
Maoni yako