Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa tafiti kuhusiana na Mahdawiya unaoitwa "Kuielekea jamii Bora", unalenga kusambaza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam Mahdi (a.j.f), na unawasilishwa kwa wasomi na wapenzi wa maarifa kama ifuatavyo:
Mambo ya pamoja kati ya Ahlul-Sunna na Shia kuhusu Mahdawiya
Ahlul-Sunna wametaja mara nyingi katika riwaya zao ukweli wa "fikra ya Mahdawiya". Ingawa katika baadhi ya maeneo inatofautiana na imani ya Kishia, lakini bado kuna mambo mengi ya pamoja.
Uhakika wa kuonekana na kusimama Mahdi (a.j.f)
Jambo la kwanza ambalo Shia na Ahlul-Sunna wanakubaliana nalo ni uhakika wa kuonekana na kusimama kwa Imam Mahdi (a.j.f). Hili ni miongoni mwa misingi ya imani ya makundi haya mawili; kiasi kwamba kuna makumi au hata mamia ya riwaya kuhusu jambo hili katika vyanzo vyao vya riwaya.
Nasaba ya Imam Mahdi (a.j.f)
Moja ya mambo ambayo Shia na Ahlul-Sunna wanakubaliana kwa kiasi fulani ni nasaba ya Imam Mahdi (a.j.f). Shia wameeleza nasaba hii kwa uwazi kamili hadi kwa baba mtukufu wa Imam Mahdi (a.j.f), lakini Ahlul-Sunna wametaja katika baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:
Imam Mahdi (a.j.f) ni miongoni mwa Ahlul-Bayt na ni miongoni mwa watoto wa Mtume Muhammad (s.a.w).
Ibn Majah katika kitabu chake cha Sunan amenukuu kwamba Mtume (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake) amesema:
«الْمَهْدِی مِنَّا أَهْلَ الْبَیتِ یصْلِحُهُ اللَّهُ عَزَّ وَ جَلَّ فِی لَیلَةٍ.»
Mahdi ni mmoja wetu, watu wa Nyumba, na Mwenyezi Mungu atamuweka sawa katika usiku mmoja.
(Sunan Ibn Majah, Juzuu ya 2, Hadithi ya 4085; Kashf al-Ghummah, Juzuu ya 2, uk. 477; Dala’il al-Imamah, uk. 247)
Mtume Mtukufu (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake) amesema:
«یخرج رجل من أهل بیتی عِنْدَ انْقِطَاعٍ مِنَ الزَّمَانِ وَ ظُهُورٍ مِنَ الْفِتَن یکُونُ عَطَاؤُهُ حثیاً.»
Wakati wa mwisho wa zama na kuenea kwa fitna, mtu kutoka katika watu wa Nyumba yangu atatokea ambaye atakuwa mkarimu sana.
(Ibn Abi Shaybah, al-Kitab al-Musannaf, Hadithi 37639; Kashf al-Ghummah, Juzuu ya 2, uk. 483)
San’ani katika al-Musannaf amenukuu kutoka kwa Mtume Mtukufu (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake):
«...فَیبْعَثُ اللَّهُ رَجُلًا مِنْ عِتْرَتِی من أَهْلِ بَیتِی...»
"...Basi Mwenyezi Mungu atamleta mtu kutoka katika kizazi changu, miongoni mwa watu wa Nyumba yangu..."
(San’ani, al-Musannaf, Juzuu ya 11, Hadithi 20770; Tabarani, al-Mu’jam al-Kabir, Juzuu ya 10, Hadithi 10213)
Imam Mahdi (a.t.f.s.) ni kutoka katika kizazi cha Imam Ali (a.s.)
Miongoni mwa mambo yenye makubaliano kati ya Sunni na Shia ni kwamba Imam Mahdi ametokana na kizazi cha Imam Ali (a.s.). Suyuti katika kitabu cha ‘Arf al-Wardi amenukuu kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake) alishika mkono wa Ali (a.s.) na kusema:
«سیخرج من صلب هذا فتی یمْلأ الأَرْضَ قِسْطاً وَ عَدْلاً.»
"Kutoka katika kizazi cha mtu huyu, hivi karibuni kijana atatokea atakayejaza dunia kwa uadilifu na haki."
(Jalaluddin Suyuti, al-Hawi lil-Fatawi, Kitabu: al-‘Arf al-Wardi, uk. 74 na 88)
Juwayni Shafi’i katika kitabu cha Fara’id al-Simtayn amenukuu kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake) amesema:
«إِنَّ عَلِی بْنَ أَبِی طَالِبٍ علیهالسلام إِمَامُ أُمَّتِی وَ خَلِیفَتِی عَلَیهَا بَعْدِی وَ مِنْ وُلْدِهِ الْقَائِمُ الْمُنْتَظَرُ الَّذِی یملا الله به الارض عدلا و قسطا کَمَا مُلِئَتْ ظُلْماً وَ جَوْراً...»
"Hakika Ali bin Abi Talib (a.s.) ni Imamu wa umma wangu na khalifa wangu juu yao baada yangu. Na ni miongoni mwa watoto wake al-Qa’im al-Muntadhar ambaye kwa kupitia yeye Mwenyezi Mungu ataijaza ardhi uadilifu na haki kama ilivyojazwa kwa dhulma na uonevu..."
(Juwayni Shafi’i, Fara’id al-Simtayn, Juzuu ya 2, uk. 327, Hadithi 589; Kamal al-Din wa Tamam al-Ni’mah, Juzuu ya 1, uk. 287, mlango wa 25, Hadithi 7)
Imam Mahdi ametokana na kizazi cha Fatima (a.s.)
Katika riwaya nyingi kutoka kwa Ahl al-Sunna, imesisitizwa kwamba Imam Mahdi (a.t.f.s.) ni kutoka kwa watoto wa Fatima (a.s.). Ibn Majah amenukuu kutoka kwa Ummu Salama kwamba alimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake) akisema:
«الْمَهْدِی مِنْ وُلْدِ فَاطِمَةَ.»
"Al-Mahdi ni kutoka kwa watoto wa Fatima."
(Sunan Ibn Majah, Hadithi 4086; Abu Dawud, Sunan Abi Dawud, Juzuu ya 4, Hadithi 4284; Nu’aym bin Hammad, al-Fitan, uk. 375; Hakim, al-Mustadrak, Juzuu ya 4, uk. 557)
Jina la Imam Mahdi (a.t.f.s.) ni sawa na la Mtume (s.a.w.w.)
Wafuasi wa Sunni na Shia wamekubaliana kwamba jina la Imam Mahdi (a.t.f.s.) ni sawa na jina la Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake).
(Maqdisi Shafi’i, ‘Uqud al-Durar, uk. 45, 55
Misingi ya Kudhihiri
Baadhi ya mabadiliko ya kijamii kabla ya kudhihiri kwa Mahdi yameelezwa katika vyanzo vya Kishia na Kisunni:
Watu kukata tamaa
Dawud bin Kathir al-Raqi anasema: Nilimwambia Imam Swadiq (a.s): Muda wa kudhihiri umekuwa mrefu sana kwetu kiasi kwamba vifua vyetu vimejaa dhiki... Imam (a.s) akasema:
“Wakati kukata tamaa kwa watu kuhusu faraja yetu kutakapozidi kila kitu... mwito kutoka mbinguni utaita kwa jina la Qa’im.
” (Nu’mani, al-Ghaybah, uk. 186, hadithi ya 29)
Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) alimwambia Imam Ali (a.s):
“Ewe Ali! Kudhihiri kwa Mahdi kutakuwa wakati miji itakapobadilika, waja wa Mungu watakapodhoofika na kukata tamaa na faraja na kudhihiri kwa Mahdi; hapo ndipo Mahdi Qa’im kutoka kizazi changu atadhihiri.”
(Qunduzi, Yanabi‘ al-Mawaddah, uk. 528; pia taz. al-Bayan fi Akhbar Sahib al-Zaman, uk. 42, hadithi ya 21; al-Hawi lil-Fatawi, uk. 92)
Kuenea dhuluma kila mahali
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amesema:
«لَوْ لَمْ یبْقَ مِنَ الدُّنْیا إِلَّا یوْمٌ لَطَوَّلَ اللَّهُ ذَلِکَ الْیوْمَ حَتَّی یبْعَثَ رَجُلًا مِنْ أَهْلِ بَیتِی یمْلَأُ الْأَرْضَ عَدْلًا وَ قِسْطاً کَمَا مُلِئَتْ ظُلْماً وَ جَوْراً...»
“Hata kama dunia itabaki na siku moja tu, Mwenyezi Mungu ataifanya siku hiyo kuwa ndefu hadi atakapomleta mtu kutoka katika Ahlul-Bayt wangu atakayejaza dunia uadilifu na haki kama ilivyojaa dhuluma na uonevu...”
(Abu Dawud, Sunan Abi Dawud, hadithi ya 4282)
Alama za Kudhihiri
Katika vyanzo vya riwaya vya Kishia, baadhi ya matukio yajayo yametajwa kama alama za kudhihiri. Alama hizi zimegawanywa katika makundi mawili: za lazima na zisizo za lazima. Baadhi ya alama hizi pia zimetajwa katika vyanzo vya Kisunni:
Mwito wa mbinguni
Mtume mtukufu wa Uislamu (s.a.w.w) amesema:
“Katika mwezi wa Muharram, sauti kutoka mbinguni itasikika ikisema: Mteule wa Mwenyezi Mungu ni fulani (Mahdi); basi sikilizeni maneno yake na mfuateni.”
(Na‘im bin Hammad, al-Fitan, uk. 93; Maqdisi Shafi‘i, ‘Uqd al-Durar fi Akhbar al-Muntadhar, uk. 79, 83, 99; taz. Fara’id al-Simtayn, juz. 2, uk. 316; al-Hawi lil-Fatawi, uk. 73)
Imam Ali bin Abi Talib (a.s) pia amesema:
“Wakati sauti kutoka mbinguni itasema kuwa; haki iko kwa watu wa nyumba ya Muhammad (s.a.w.w), hapo ndipo Mahdi atadhihiri
” (Ja‘far bin Muhammad bin al-Munadi, al-Malahim, uk. 196, hadithi ya 143)
Imam Swadiq (a.s) amesema:
«النِّدَاءُ مِنَ الْمَحْتُوم...»
“Wito [wa mbinguni] ni miongoni mwa alama za lazima.”
(Nu’mani, al-Ghaybah, hadithi ya 11)
Sufyani
Alama nyingine ya kudhihiri Mahdi al-Muntadhar ni kuibuka kwa mtu aitwaye Sufyani. Katika hadithi nyingi za Kishia, jambo hili limeelezwa kuwa la lazima.
(Taz. Nu’mani, al-Ghaybah, uk. 257, hadithi ya 15 na uk. 264, hadithi ya 26; Shaykh Saduq, Kamal al-Din wa Tamam al-Ni‘mah, juz. 2, uk. 650, hadithi ya 5; Muhammad bin Hasan al-Tusi, Kitab al-Ghaybah, uk. 435)
Katika baadhi ya hadithi za Kisunni pia, Sufyani ametajwa waziwazi kama mojawapo ya alama za kudhihiri kwa Mahdi (a.f).
(al-Hawi lil-Fatawi, uk. 80; ‘Uqd al-Durar, uk. 76; pia taz. Muttaqi Hindi, Kanz al-‘Ummal, juz. 11, uk. 273)
Kudidimia kwa ardhi katika Bayda’
Neno “Khasf” linamaanisha kudidimia au kutoweka ardhini, na “Bayda’” ni jina la eneo huko Makka na Madina.
Alama hii inamaanisha kuwa Sufyani atakwenda Makka na jeshi kubwa kwa nia ya kupigana na Imam Mahdi (a.f). Wakiwa njiani kati ya Makka na Madina, katika eneo linaloitwa Bayda’, watazama ardhini kwa njia ya kimiujiza.
Mtume (s.a.w.w) amesema:
«...فَیبْعَثُ إِلَیهِ جَیشٌ من الشام حَتَّی إِذَا کَانُوا بِالْبَیدَاءِ خُسِفَ بِهِمْ...»
“...Jeshi kutoka Sham litatumwa dhidi yake; watakapofika Bayda’, watazama ardhini...”
(San‘ani, al-Musannaf, juz. 11, uk. 371)
Na vile vile tazama:
(Tabarani, al-Mu‘jam al-Awsat, juz. 2, uk. 35; Muttaqi Hindi, Kanz al-‘Ummal, juz. 11, uk. 277, hadithi ya 31513; al-Bayan, uk. 44, hadithi ya 23; ‘Uqd al-Durar, uk. 80; al-Hawi lil-Fatawi, uk. 71)
Kuuawa kwa Nafsi safi
Mojawapo ya alama za lazima, ambayo pia imetajwa katika baadhi ya vyanzo vya Kisunni, ni kuuawa kwa mtu safi na asiye na hatia karibu na Ka‘aba, kati ya Rukn na Maqam, kabla ya kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.s).
(Ibn Abi Shaybah, al-Musannaf, juz. 8, uk. 679; Muttaqi Hindi, Kanz al-‘Ummal, juz. 11, uk. 277; Jalal al-Din Suyuti, al-Hawi lil-Fatawi, uk. 78)
Mambo Yanayohusiana na Kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.f)
Kurekebishwa kwa jambo la kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.f) katika usiku mmoja
Kutokana na baadhi ya riwaya, inaeleweka kuwa jambo la kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.f) litarekebishwa na kuandaliwa katika usiku mmoja. Hili pia limetajwa na vyanzo vya Kishia na Kisunni.
(al-Bayan fi Akhbar Sahib al-Zaman, uk. 31, hadithi ya 11; al-Hawi lil-Fatawi, uk. 69; ‘Uqd al-Durar, uk. 210)
Mahali pa Kudhihiri
Kuhusu mahali ambapo kudhihiri Imam Mahdi (a.f) kutaanza na kuungana kwa wafuasi wake wa karibu, kuna hadithi nyingi zilizopokewa. Mambo ya pamoja katika hadithi hizi ni kwamba kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.f) kutaanza kutoka Makka.
Na — kwa mujibu wa hadithi nyingi — kutaanza kutoka karibu na Ka‘aba.
Mtume Mtukufu wa Uislamu (s.a.w.w) amesema:
“Makundi kutoka Iraq na wakuu kutoka Sham watamjia Mahdi na watafanya naye bai‘a kati ya Rukn na Maqam...”
(Naʻim bin Hamadi, Al-Fitan, Sehemu ya Nne, uk. 242, Hadithi ya 950)
Pia amesema:
“... Bai‘a kwa Mahdi itafanyika kati ya Rukn na Maqam.”
(Maqdisi Shafi‘i, ʻAqd al-Durar, Mlango wa 2, uk. 56)
Kushuka Malaika kwa Ajili ya Kumnusuru Imam Mahdi (a.f)
Miongoni mwa masuala ya pamoja kati ya Waislamu wa Kishia na Kisunni ni kwamba malaika watashuka kumsaidia Imam Mahdi (a.f) wakati wa kudhihiri kwake.
(ʻAqd al-Durar, uk. 46, 117, 185; Al-Hawi lil-Fatawi, uk. 88; Al-Bayan, uk. 84, Hadithi ya 53)
Kuteremka kwa Nabii Isa (a.s) na Kumfuata Imam Mahdi (a.f)
Mojawapo ya matukio muhimu sana katika zama za kudhihiri ni kurejea kwa Nabii Isa (a.s). Tukio hili limetajwa katika hadithi nyingi.
Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) amesema:
«یلتفت المهدی و قد نزل عیسی بن مریم کانما یقطر من شعره الماء، فیقول المهدی: تقدم، وَصلِّ بالناس فیقول عیسی بن مریم: انما اقیمت الصَّلاة لک فیصلی عیسی خلف رجل من ولدی...»
“Mahdi atageuka na kuona Isa bin Maryam ameshuka, kana kwamba maji yanatiririka kutoka nywele zake. Mahdi atamwambia: Tangulia uswali na watu. Isa atajibu: Swala imesimamishwa kwa ajili yako. Kisha ataswali nyuma ya mtu kutoka katikaka kizazi changu.”
(Maqdisi Shafi‘i, ʻAqd al-Durar, uk. 292; Ali bin Isa Arbilī, Kashf al-Ghumma, juzuu ya 3, uk. 278)
Pia amesema:
“Jibril alikuja kwangu na kusema: Ewe Muhammad! Mwenyezi Mungu Mtukufu amewachagua watu saba kutoka Bani Hashim... na miongoni mwao yupo Qa’im ambaye Isa bin Maryam ataswali nyuma yake.”
(Al-Kafi, juzuu ya 8, uk. 50, Hadithi ya 10)
Imam Swadiq (a.s) amesema:
«...وَ ینْزِلُ رُوحُ اللَّهِ عِیسَی ابْنُ مَرْیمَ فَیصَلِّی خَلْفَهُ...»
“...Roho ya Mwenyezi Mungu, Isa bin Maryam, atashuka na ataswali nyuma yake.”
(Sheikh Saduq, Kamāl al-Dīn wa Tamām al-Niʻma, juzuu ya 2, uk. 330, Hadithi ya 16)
Sifa za Dola ya Imam Mahdi (a.f)
Kusambaza Haki
Kwa mujibu wa hadithi nyingi, kusimamisha uadilifu na usawa ni miongoni mwa malengo makuu ya harakati ya Imam Mahdi (a.f). Hili limetajwa katika hadithi za Kishia na Kisunni.
(Musannaf Ibn Abi Shaybah, Hadithi ya 19484; Sunan Abi Dawud, Hadithi ya 4282; Al-Muʻjam al-Kabir Ṭabarani, Hadithi ya 10219 na 10220)
Ustawi na Maisha Bora kwa Wote
Sifa nyingine ya serikali ya Imam Mahdi (a.f) ni ustawi wa maisha kwa watu wote. Hili pia limetajwa katika hadithi za Kishia na Kisunni.
Mtume (s.a.w.w) amesema:
«یکون فی امتی المهدی ... تعیش امتی فی زمانه عیشاً لم تعشه قبل ذلک.»
“Mahdi atakuwa katika umma wangu... watu wa umma wangu wataishi maisha ambayo hawajawahi kuyaishi kabla yake.”
(Ibn Abi Shaybah, Al-Musannaf, juzuu ya 7, Hadithi ya 19484)
Pia amesema:
«یکُونُ فِی أُمَّتِی الْمَهْدِی ... یتَنَعَّمُ فِیهِ أُمَّتِی نِعْمَةً لَمْ یتَنَعَّمُوا مِثْلَهَا قَطُّ.»
“Mahdi atakuwa katika umma wangu... watu wangu wataneemeka neema ambayo hawajawahi kuipata kabla yake.”
(Ibn Majah Qazwini, Sunan, Hadithi ya 4083; Ali bin Isa Arbilī, Kashf al-Ghumma fi Maʻrifat al-Aʼimma, juzuu ya 3, uk. 257)
Ridhaa ya Umma kwa Serikali ya Mahdi (a.f)
Baada ya kudhihiri na katika kipindi cha utawala wa Imam Mahdi (a.f), watu wote wataridhika kikamilifu na uongozi wake. Hili limetajwa katika hadithi za Kishia na Kisunni.
(Ṣanʻānī, Al-Musannaf, Hadithi ya 20770; Al-Bayān, uk. 42, Hadithi ya 21; Al-Ḥāwī lil-Fatāwī, uk. 69; ʻAqd al-Durar, uk. 73; Farāʼid al-Simṭayn, juzuu ya 2, uk. 310, Hadithi ya 561)
Usalama Kila Mahali
Mojawapo ya sifa muhimu za jamii ya zama za kudhihiri ni usalama wa kila mahali duniani.
Imam Baqir (a.s) amesema:
“Naapa kwa Mwenyezi Mungu! [Wafuasi wa Mahdi] watapigana hadi pale ambapo Mungu atakuwa akiabudiwa peke yake na hakuna atakayemshirikisha. Hadi mzee mzee asiyejiweza atasafiri kutoka upande mmoja wa dunia hadi mwingine bila mtu yeyote kumdhuru.”
(Ṭabarānī, Al-Muʻjam al-Kabīr, juzuu ya 8, uk. 179)
Watu Kujitosheleza
Mojawapo ya tabia za watu katika zama za kudhihiri ni hali ya kujitosheleza. Mtume (s.a.w.w) amesema:
«أُبَشِّرُکُمْ بِالْمَهْدِی ... وَ یمْللاً اللَّهُ قُلُوبَ أُمَّةِ مُحَمَّدٍ غِنًی...»
“Nawapeni bishara ya Mahdi... Mwenyezi Mungu atajaza nyoyo za umma wa Muhammad (s.a.w.w) kwa utoshelevu.”
(Ahmad bin Hanbal, Musnad, juzuu ya 3, uk. 37; Maqdisi Shafi‘i, ʻAqd al-Durar fi Akhbār al-Muntaẓar, Mlango wa 8, uk. 219)
Ushindi wa Uislamu Juu ya Dini Zingine
Miongoni mwa masuala ya pamoja kati ya Kishia na Kisunni ni kwamba Uislamu utashinda dini zote katika zama za kudhihiri.
ʻAqd al-Durar, uk. 95
Kuwa uongozi wa Imam Mahdi (a.f) ni wa Ulimwengu mzima
Hadithi nyingi za Kiislamu zinasisitiza kuwa serikali ya Imam Mahdi (a.f) itakuwa ya kimataifa. Mtume (s.a.w.w) amesema:
«... یبایع له الناس بین الرکن و المقام، یردالله به الدین و یفتح له فتوحاً، فلایبقی علی وجه الارض الا من یقول: لااله
“Watu watamfanyia bai‘a kati ya Rukn na Maqam. Mwenyezi Mungu atairejesha dini kupitia yeye na atamfungulia ushindi, kiasi kwamba hakuna atakayebaki duniani isipokuwa atasema: La ilaha illa Allah.”
(Maqdisi Shafi‘i, ʻAqd al-Durar, Mlango wa Pili, hadithi ya mwisho)
Imam Swadiq (a.s) amesema:
«إِذَا قَامَ الْقَائِمُ لا تَبْقَی أَرْضٌ إِلا نُودِی فِیهَا شَهَادَةُ أَنْ لا إِلَهَ إِلا اللَّهُ وَ أَنَّ مُحَمَّداً رَسُولُ اللَّهِ»
“Wakati Qa’im atakaposimama, hakutakuwa na ardhi yoyote isipokuwa sauti ya shahada ya kwamba hakuna mungu isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah itasikika humo.”
(Ayyashi, Tafsiri ya Ayyashi, juzuu ya 1, uk. 207, Hadithi ya 81)
Pia kuna hadithi nyingi za pamoja katika vyanzo vya Kishia na Kisunni kuhusiana na sifa za kimwili za Imam Mahdi (a.f).
Utafiti huu unaendelea...........
Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Darsname-ye Mahdawiyyat” kilichoandikwa na Khodamorad Salimian, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Maoni yako