Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Nasser Makarim Shirazi, siku ya Jumatano, katika kikao alichokutana na rais pamoja na kundi la wakurugenzi na watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kompyuta katika Elimu ya Kiislamu (Noor), kilichofanyika kwa kushirikiana na kundi la walimu wa elimu ya Qur’ani na tafsiri wa Hawza, kwa mnasaba wa uzinduzi wa mfumo wa akili bandia “Mazungumzo na Tafsiri,” sambamba na kupongeza juhudi za kidini zilizofanyika katika uwanja wa teknolojia, alisisitiza kuwa: “Hawza si kwamba imesalia nyuma katika msafara wa elimu na teknolojia, bali katika uwanja wa kutumia akili bandia kwenye kuihudumia Qur’ani na mafundisho ya Ahlul-Bayt (A.S.) imekuwa mstari wa mbele.”
Aliongeza kuwa: “Sikuwa najua kuwa Hawza imekuwa hai kiasi hiki katika uwanja wa akili bandia. Nimefurahia na kujivunia kukutana nanyi na kupata ripoti kamili. Nawapongeza nyote kwa kutumia fursa za kielimu za kisasa katika kuihudumia ya Qur’ani Tukufu na elimu za Kiislamu.”
Kutimia kwa maneno ya Amirul-Mu’minin (A.S.) kuhusu Qur’ani kuwa ‘chemchemu za elimu’
Kiongozi huyu mkubwa wa kidini, akirejelea maneno ya Amirul-Mu’minin (A.S.) katika Nahjul-Balagha:
«إِنَّ اَللَّهَ سُبْحَانَهُ لَمْ یَعِظْ أَحَداً بِمِثْلِ اَلْقُرْآنِ... وَ فِیهِ رَبِیعُ اَلْقَلْبِ وَ یَنَابِیعُ اَلْعِلْمِ وَ مَا لِلْقَلْبِ جِلاَءٌ غَیْرُهُ»
“Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hajamnasihi yeyote kwa mfano wa Qur’ani... ndani yake kuna majira ya moyo na chemchemu za elimu, na hakuna kitu chochote kinachoweza kuusafisha moyo isipokuwa Qur’ani,”
alisema: “Qur’ani ni chemchemu ya elimu na kipambanuzi kati ya haki na batili. Kila kilichokuwa kabla yenu na kitakachokuja baada yenu mpaka siku ya Kiyama kimeelezwa humo, na uongofu unatiririka kutoka kwake. Kauli hii ya Amirul-Mu’minin (A.S.) inaonesha kwamba Qur’ani ni chanzo cha elimu isiyo na mwisho. Kila mara mwanadamu anapoirudia, ujuzi wake huongezeka na ujinga wake hupungua. Kazi mnayofanya ninyi ni mfano halisi wa kurejea kwenye chemchemu za elimu za Qur’ani.”
Qur’ani ni chanzo cha elimu zote; tusipozipata, upungufu ni kutoka kwetu
Kisha alirejelea aya ya Qur’ani akisema:
(وَنَزَّلْنَا عَلَیْکَ الْکِتَابَ تِبْیَانًا لِکُلِّ شَیْءٍ وَهُدًی وَرَحْمَةً وَبُشْرَی لِلْمُسْلِمِینَ)
“Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachoeleza kila kitu, ni uongozi, rehema na bishara kwa Waislamu.”
(An-Nahl, 89)
Akasema: “Mwenyezi Mungu ameeleza kwamba Qur’ani ni maelezo ya kila kitu, yaani kila jambo analohitaji mwanadamu kwa ajili ya uongofu na ufanisi wake limo ndani yake. Tukishindwa kulipata jambo fulani humo, upungufu ni katika uelewa wetu, si katika Kitabu cha Mungu.”
Nafasi ya kielimu ya tafsiri na mchango wa teknolojia
Akasema zaidi: “Zamani baadhi ya watu walidhani tafsiri si taaluma ya kielimu, lakini leo imebainika kuwa tafsiri ni mojawapo ya fani za kielimu zaidi. Kwa sababu kuingia katika uelewa sahihi wa aya, uchambuzi wa kilugha, sababu za kushuka na uchimbaji wa maana, kunahitaji utafiti wa kina. Sasa kwa kutumia teknolojia ya akili bandia, njia hii inakwenda kwa usahihi zaidi, kwa kasi na kwa ushahidi wa kutosha.”
Aliongeza kuwa: “Kazi mnazofanya katika uwanja wa tafsiri ni alama ya ustawi wa Hawza katika elimu ya kisasa. Hawza haijasalia nyuma; bali katika uwanja huu nyeti wa tafsiri ya Qur’ani, iko mstari wa mbele.”
Wito wa kueneza taarifa kwa usahihi
Ayatollah Makarim Shirazi, akisisitiza ulazima wa kutoa taarifa kuhusu mafanikio ya kipekee ya Kituo cha Noor, alisema: “Kuna kazi nyingi za thamani kubwa zinazofanyika, lakini hazitangazwi. Vyombo vya habari na runinga vinapaswa kuonesha jinsi Hawza ilivyopiga hatua katika elimu na teknolojia.
Kuwajulisha watu ni nusu ya kazi, kwani uelewa wa jamii huleta motisha ya kuendeleza shughuli za kielimu.” Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwajulisha pia viongozi wakuu na maulamaa wa Hawza kuhusu mafanikio haya.
Ulazima wa kujiandaa katika vita vya kitamaduni
Kiongozi huyu mkubwa wa kidini, akirejelea amri ya Qur’ani kuhusu maandalizi dhidi ya maadui, alisema:
وَأَعِدُّوا لَهُمْ مَا اسْتَطَعْتُمْ مِن قُوَّةٍ
“Na waandalieni kwa kadri ya uwezo wenu nguvu...”
Akasema: “Amri hii ya Mwenyezi Mungu leo haimaanishi vita vya kijeshi pekee, bali inahusu pia uwanja wa elimu na utamaduni, vita ya leo ni ya kitamaduni, na tunapaswa kujiandaa kwa silaha za kielimu na akili bandia. Kama vile kwenye uwanja wa vita ya kimwili tunavyohitaji silaha, vivyo hivyo katika uwanja wa utamaduni tunahitaji zana za elimu na uchambuzi wa kiakili.”
Akili Mnemba katika kuihudumia Qur’ani.
Ayatollah Makarim Shirazi, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alisema: “Akili bandia ina uwezo mkubwa katika tafsiri na uchambuzi wa tafsiri ya Qur’ani; jambo hili linamaanisha kutumia teknolojia kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa ya Qur’ani. Tunapaswa kutumia nguvu na uwezo wetu katika uwanja wa utamaduni. Ikiwa wengine wanatengeneza programu kwa nia za kisiasa au za kimada, basi sisi pia tufanye hivyo kwa nia ya Kiungu, kwa ajili ya kueneza ukweli wa Qur’ani.”
Yeye alionesha matumaini kwamba chombo hiki kitakuwa na matumizi pia katika nyanja nyingine za Elimu za Kiislamu kama vile fiqhi, usul, rijal, na tarikh (historia).
Maoni yako