Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, mjadala wa marufuku ya hijabu nchini Ufaransa kwa bahati mbaya ni mradi unaoendelea, ambao hatua kwa hatua umefikia kiwango cha kukandamiza haki za wanawake wenye heshima na mwenendo safi.
Ufaransa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2004 iliweka vikwazo vya kuvaa hijabu mashuleni, na baada ya hapo marufuku hizo zikaenea zaidi, zikahusisha vyuo vikuu na sekta ya michezo. Kwa masikitiko makubwa, marufuku ya hijabu katika michezo ilitekelezwa pia, na wanawake wachezaji wakazuiwa kuvaa hijabu. Wale waliokataa kuvua hijabu walilazimishwa kujiondoa kwenye michezo au kuacha timu zao kabisa.
Athari za marufuku hizo zimeonekana wazi katika michezo ya wanawake, kiasi kwamba Frank Kund Tandberg, mwanachama wa shirika la kimataifa la Norway, alilitaja jambo hilo kuwa sheria isiyo halali, akilaani vikali na kuitaka Ufaransa ifute mara moja.
Akasema: “Kuwalazimisha wanamichezo kubadili imani zao binafsi na kuacha utambulisho wao kwetu sisi ni jambo linalosababisha maumivu ya kimwili na kisaikolojia, na haliwezi kukubalika kamwe.”
Bi Hélène Péan, mchezaji wa zamani wa mpira wa kikapu kutoka Ufaransa, ambaye aliondolewa kwenye mashindano kwa sababu ya kuvaa hijabu, alikemea udhaifu wa hoja ya ‘kutokuwa na upendeleo’ iliyotolewa na viongozi wa kisiasa kama kisingizio cha kumfukuza. Alisema:
“ Michezo kiasili inajumuisha tofauti za umri, jinsia, uzito, urefu, rangi, na dini.”
Akaongeza kuwa; kisingizio hicho ni cha kinafiki na ni fedheha kwa Ufaransa.
Utafiti wa kimataifa kuhusu michezo nchini Ufaransa unaonesha kuwa nchi hiyo ndiyo pekee kati ya nchi 38 zilizochunguzwa ambayo imepiga marufuku mavazi ya kidini kwa wachezaji katika michezo.
Kinyume chake, makampuni makubwa duniani kama Nike na Hijabme yanafanya jitihada za kutumia vitambaa maalum katika kutengeneza vifaa vya michezo vya wanawake wanaovaa hijabu, ili kurahisisha uchezaji na kuongeza ufanisi. Leo hii, kubuni mavazi ya michezo yenye staha kwa wanawake wacha Mungu ni mojawapo ya changamoto kuu kwa wabunifu wa mavazi ya michezo duniani — lakini Ufaransa, katika suala hili, imebaki nyuma kwa kiwango kikubwa.
Chanzo: Shia Waves
Maoni yako