Alhamisi 2 Oktoba 2025 - 07:17
Kwa nini nia ni muhimu zaidi kuliko amali?

Hawza/ Ikiwa unataka kujua kwa nini nia safi ndiyo rasilimali kubwa ya mwanadamu katika Siku ya Kiyama, basi soma riwaya ya kusisimua kutoka kwa Imam Sajjad (a.s.).

Shirika la Habari la Hawza - Imam Zaynul Abidin (a.s.) anasema:

«اللَّهُمَّ ... وَ انْتَهِ بِنِیَّتِی إِلَی أَحْسَنِ النِّیَّاتِ.»

“Ewe Mungu, nifikishe kwa nia yangu kwenye bora ya nia.” (1)

Sherehe:
Matamanio ya nafsi na Mwenyezi Mungu, dunia ya dhahiri na Akhera  hivi ni vitu viwili vinavyotakiwa, lakini mapenzi ya vyote viwili hayawezi kukusanyika katika moyo mmoja. Mtu ambaye malengo yake yote ni matamanio ya nafsi, dunia, heshima na sifa, basi katika amali zake zote atafuata hayo malengo, na hatakuwa na ikhlasi mpaka pale mizizi ya malengo yote machafu yanayomweka mbali na Mwenyezi Mungu itakapo ondoka moyoni mwake. Hivyo basi, daraja na ngazi za nia kwa watu ni nyingi mno, bali hazina idadi. (2)

Kwa hivyo mwanadamu anapaswa katika njia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu ajitahidi kwa kadri ya uwezo wake ili afikie juu zaidi katika ngazi za nia.

Kinachoongeza zaidi umuhimu wa nia safi ni kwamba hadiya ya Mwenyezi Mungu iko kwa mujibu wa nia zetu, na si amali zetu. Kama alivyoeleza Amirul-Mu’minin (a.s.):

«عَلَی قَدْرِ اَلنِّیَّةِ تَکُونُ مِنَ اَللَّهِ اَلْعَطِیَّةُ.»

“Kwa kadiri ya nia ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyotoa zawadi.” (3)

Wale waliopata kuhudhuria katika baraza la Marhum Ayatullah Burujuirdi wamesimulia hivi:

“Alikuwa akihuzunika sana na akasema: ‘Umri wetu umekwisha, tumekwenda na hatukuweza kutuma mbele yetu chochote, wala kufanya amali yoyote.’ Mtu mmoja akasema: ‘Ewe Bwana! Mbona tena wewe? Sisi ndio tunapaswa kusema maneno haya. Wewe Alhamdulillah! Umeacha mambo mengi ya kheri, umefundisha wanafunzi wengi, umeandika vitabu vingi, umejenga msikiti huu mkubwa, shule na mengineyo.’ Baada ya kusema hivi, Ayatullah Burujuirdi akasema hadithi hii:

«أَخْلِصِ اَلْعَمَلَ فَإِنَّ اَلنَّاقِدَ بَصِیرٌ.»

“Fanya amali zako kwa ikhlasi, kwa hakika mkaguzi wa amali zako ni mwenye kuona vyema na kufahamu.” (4)

Kisha akasema: ‘Unasema nini? Amali lazima zifanywe kwa ikhlasi. Je, unadhani haya ambayo kwa mtazamo wa watu ni makubwa, basi kwa Mwenyezi Mungu pia ni hivyo hivyo?’ (5)

Kwa hivyo, Imam Sajjad (a.s.) anatufundisha kumuomba Mwenyezi Mungu daraja ya juu zaidi ya nia. Kwa sababu, iwapo mtu atapambwa kwa nia za kweli na za kiungu, basi kwa maneno ya Imam Sadiq (a.s.), atakuwa mmiliki wa moyo salama:

«صَاحِبُ اَلنِّیَّةِ اَلصَّادِقَةِ صَاحِبُ اَلْقَلْبِ اَلسَّلِیمِ.»

“Yule aliye na nia ya kweli, ndiye mwenye moyo salama.” (6)

Na bila shaka, moyo huu salama utamfaa mwanadamu katika siku ile ambayo si mali wala watoto vitamfa, bali atakayekuja mbele ya Mwenyezi Mungu akiwa na moyo salama ndiye atakayekaribishwa na rehema Yake. Kama Qur’an inavyosema:

«یَوْمَ لَا یَنْفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ؛ إِلَّا مَنْ أَتَی اللَّهَ بِقَلْبٍ سَلِیمٍ.»

“Siku ambayo mali wala watoto havitamnufaisha mtu; isipokuwa atakayemjia Mwenyezi Mungu kwa moyo salama.”  (7)

Rejea:
1- Sahifa Sajjadiyya, dua ya ishirini (Makarimul Akhlaq).

2- Mafhumu ya Kimaadili, Usul al-Kafi, uk. 162.

3- Ghurar al-Hikam, juz. 1, uk. 452.

4- Kulliyat al-Hadith al-Qudsi, juz. 1, uk. 161.

5- Ta’lim na Tarbiya katika Uislamu, uk. 249 (kwa mabadiliko kidogo).

6- Tafsir Nur al-Thaqalayn, juz. 4, uk. 58.

7- Surah Shu‘ara, aya 88-89.

Imeandaliwa na kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha