Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Imamu Zayn al-'Abidīn (as) katika moja ya sehemu katika Saḥīfa Sajjadiyya humuomba hivi Mwenyezi Mungu Mtukufu:
اللَّهُمَّ ... اجْعَلْ هَمَسَاتِ قُلُوبِنَا، وَ حَرَکَاتِ أَعْضَائِنَا وَ لَمَحَاتِ أَعْیُنِنَا، وَ لَهَجَاتِ أَلْسِنَتِنَا فِی مُوجِبَاتِ ثَوَابِکَ
Ewe Mola! Yajaayo moyoni mwetu, harakati za viungo vyetu, mionekano ya macho yetu na maneno ya ndimi zetu, yafanye katika mambo yanayopelekea kupata thawabu zako. 1
Sherehe:
Ili kufikia cheo cha ufanisi wa kweli na wa milele, hakika ni lazima kuujaza uwepo wako wote kwenye mapenzi na radhi ya Mwenyezi Mungu, na kwa kweli, uwepo mtukufu wa Imamu Zayn al-ʿĀbidīn (as) kwa uzuri unatufundisha kutamani maombi haya kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. 2
Ewe Mola! Kila kitu kinachopita moyoni mwangu, kifanye kiwe chako, nifanye nifikirie tu juu yako na kwa ajili yako, tamaa na matamanio ya moyo wangu yaelekeze katika njia inayopata radhi yako.
Ewe Mola! Fanya viungo vyote vya mwili wangu vitumike katika njia yako na kwa ajili yako.
Ewe Mola! Uono wa macho yangu ufanye uwe wako ili mtazamo wangu uangukie tu katika yale unayopenda.
Na Ewe Mola! Kila ninachokitamka kwa ulimi wangu kifanye kiwe kwa ajili yako, ili nisitoe neno lolote ila kwa ridhaa yako.
Na huu ndio upeo wa mapenzi ya kweli: kwamba tuitake nafsi nzima ielekee kwa Mola, tusifikirie ila Yeye, tusitende ila kwa ajili Yake, tusimwangalie ila Yeye na tusiseme ila kwa ajili Yake, kwa sababu kila kitu kimefupishwa katika uwepo wa Mpenzi na Mola, na kila rangi hufifia mbele Yake, na kwa kweli: «Ni ipi rangi bora kuliko rangi ya Mwenyezi Mungu?» 3
Je, ili kufikia cheo cha ikhlasi mtu afanye nini?
Ni lazima tukubali kwamba kufika cheo hiki ni jambo gumu, lakini inawezekana, hakuna lengo linalofikiwa bila mazoezi na marudio, hivyo pia kwa lengo hili la kimungu, ni lazima kuwa na hima na kujitahidi.
Njia kuu ni kuihesabu nafsi, ili hatua kwa hatua mtu aujaze uwepo wake kwa nuru ya Mwenyezi Mungu, na hakika, kuzoea maneno ya Ahlul-Bayt wa isma (as) humpa mtu motisha ya kazi hii, kwani haiwezekani mtu akaishi na nuru bila yeye mwenyewe kuwa nuru.
Alama ya cheo hiki
Imamu Ṣādiq (as) anatufundisha njia na alama ya kipimo katika jambo hili, ili kupitia hapo – katika njia ya kujihesabu nafsi – mtu ajipime.
Yeye anasema: «ʿAmal safi ni ile usiyotaka mtu yeyote akusifu kwayo isipokuwa Mwenyezi Mungu». 4
Na pia anasema: «Hakuna mja atakayefikia hakika ya ikhlās, mpaka achukie watu kumsifu kwa jambo alilolitenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.» 5
Kwa hiyo, kila mahali ambapo bado katika mawazo na mioyo yetu kuna mtazamo kwa kiumbe na si kwa Muumba, basi ni dalili kwamba tunapaswa kuongeza juhudi zaidi, ili hatua kwa hatua uwepo wetu wote uwe tu kwa ajili ya Mpenzi wa kweli.
Iwapo hali itakuwa hivi, basi sifa na pongezi za watu wengine, au hata dhihaka zao, hazitatia athari katika nafsi zetu; kwani katika cheo hiki, hatumuoni ila Mola, na hatuisikii ila sauti Yake.
Tanbihi:
1. “Thawabu” katika Qurʾān Tukufu imekuja kwa maana ya malipo ya mema na mabaya yote mawili, japokuwa mara nyingi imetumika kwa malipo mema. (Nathr Ṭūbā, ʿAllāmah Shahrānī, chini ya neno “Thawb”, j.1, uk.120 / Qāmūsul-Qurʾān, Sayyid ʿAlī Akbar Qurashī, j.1, uk.321).
2. Duʿā ya tisa ya Ṣaḥīfa Sajjadiyya.
3. Qurʾān, Sūrat al-Baqara/138:
4. Uṣūl al-Kāfī, j.2, uk.16.
5. Tafsīr Majmaʿ al-Bayān, chini ya āyah 139, Sūrat al-Baqara.
Imeandaliwa na kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.
Maoni yako