Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Pamoja na uwazi na yakini ya maana ya kweli ya intidhār, tafsiri na mitazamo mbalimbali imetolewa kuhusiana nayo, Sehemu kubwa ya mitazamo hii inahusiana na uelewa wa wanafikra na wanazuoni, na sehemu nyingine inahusiana na ufahamu wa baadhi ya Mashia kuhusiana na suala la intidhār, kuna mitazamo miwili mikuu na ya msingi katika uwanja huu:
1- Intidhār sahihi na yenye kujenga
Intidhār yenye kujenga, chocheo la harakati na yenye kuleta uwajibikaji, ndiyo intidhār ya kweli ambayo katika riwaya imeitwa: “Ibada yenye fadhila zaidi” na “Jihadi bora zaidi ya umma wa Mtume (saww).”
Marehemu Mudḥaffar (1) katika maelezo mafupi na yenye kukamilika, ameifasiri intidhār kwa namna hii:
Maana ya intidhār ya kudhihiri Mrekebishaji wa kweli na Mkombozi wa Kimungu, Hadrati Mahdi (aj), si kwamba Waislamu wakae na kupuuza yale yaliyo wajibu kwao kama vile: kuusaidia ukweli, kufufua sheria na maagizo ya dini, jihadi, na kuamrisha mema na kukataza maovu; kisha wakasubiri kwamba Qā’im Aal-Muḥammad (aj) aje arekebishie mambo.
Kila Muislamu ana jukumu la kuiona nafsi yake imewajibika kutekeleza amri za Uislamu; asibakie nyuma katika jitihada za kuutambua Uislamu kwa njia sahihi; na kwa kadri ya uwezo wake asikome kuamrisha mema na kukataza maovu, kama alivyosema Mtume Mtukufu (saww):
«کُلُّکُمْ رَاعٍ وَکُلُّکُمْ مسؤول عَنْ رَعِیَّتِهِ»
Kila mmoja wenu ni mchungaji na kila mmoja wenu atawajibishwa juu ya kile alicho kichunga.
(Biharul - Anwaar, juz 72, uk 38)
Kwa msingi huu, Muislamu hawezi kwa kisingizio cha kusubiri kudhihiri Mrekebishaji Mahdi, akapuuza au akajiepusha na majukumu yake madhubuti na ya yakini; kwa kuwa kusubiri hakubatilishi wajibu wala hakutoi ruhusa ya kuchelewesha matendo, uzembe katika wajibu wa dini na kutojali dini, kwa hali yoyote ile, si jambo linalokubalika.
(Aqaaid Imaamiyyah, uk 118)
Kwa muhtasari, utamaduni wa kweli wa intidhār umejengeka juu ya nguzo tatu kuu:
1- Kutokuridhika au kutojitosheleza na hali iliyo sasa;
2- Kuwa na matumaini ya mustakabali bora;
3- Harakati na jitihada za kuipita hali ya sasa na kufikia hali inayokusudiwa.
2- Intidhār potofu na yenye kubomoa
Intidhār yenye kubomoa na inayozuia, ambayo kwa hakika ni aina ya ibāhiyya (upuuzi wa dini), daima imekuwa ikilaaniwa na kukemewa na wakubwa wa dini, na wao wamewaonya wafuasi wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (as) kuepukana nayo.
Allāmah Muṭahhari (ra) katika hili anaandika:
"Intidhār ya namna hii" ni ufahamu wa juujuu wa watu kuhusiana na Mahdiyya na Qiyām na Mapinduzi ya Mahdi mwenye kutolewa kiaga (aj), ambayo huchukuliwa kuwa na tabia ya mlipuko tu; ikitokana tu na kuenea na kusambaa kwa dhulma, ubaguzi, ukandamizaji, uvunjaji haki na ufisadi.
Ufafanuzi huu wa kudhihiri na Qiyām ya Mahdi (as), na aina hii ya kusubiria faraja ambayo huishia kuzifanya sheria na mipaka ya Kiislamu kuwa kama imesitishwa, na ikawa ni aina ya ibāhiyya, kwa namna yoyote ile haipatani na mizani ya Kiislamu na Qur’ani.
(Qiyaamu wa Inqilaabu Mahd (as), uk 54)
Mwanzilishi wa mfumo wa Kiislamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika maelezo yake yenye thamani baada ya kubainisha mitazamo potofu kuhusiana na intidhār, aliwalaani vikali wale waliokuwa na mitazamo hiyo.
(Swahifatu Nuur, juz 21)
Kwa hivyo, Msubiri wa kweli wa kudhihiri na Qiyām ya Mahdi (as) hawezi kamwe kuwa mtazamaji tu.
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka katika kitabu «Darsnāmeh Mahdawiyya» kilichoandikwa na Khodā-Morād Salīmiyān, huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Maelezo ya ziada:
(1) Muḥammad-Riḍha Mudḥaffar (1322 - 1383 Q) alikuwa ni Mujtahid maarufu, faqīh, usūliy, mutakallim, mwanafalsafa na mtafiti wa Kishia katika fani za fiqhi, usūl, manṭiq, kalām na ‘aqāid.
Maoni yako