Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kikao cha Kamati ya Kimataifa ya Kihawza ya Muqawama kimefanyika kwa kuhudhuriwa na Allama Sheikh Ali Al-Khatib, Rais wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kishia wa Lebanon, pamoja na baadhi ya viongozi wa kielimu wa Hawza.
Sheikh Ali Al-Khatib, akieleza hali ya vita nchini Lebanon, alisema: “Tuko katika hatua ngumu sana ya vita, adui ameivamia Lebanon kwa nguvu zote, na sisi, licha ya majeraha mengi, bado tunaendeleza mapambano ya muqawama.”
Ameongeza kuwa: “Katika operesheni ya kulinda eneo la Beirut, mashahidi wengi wametolewa, na wengi wao hawakuwa Waislamu wa Kishia. Hii ni ishara ya mshikamano na umoja wa makundi yote ya Lebanon katika kukabiliana na dhulma ya adui.”
Rais huyo wa Baraza Kuu la Kishia Lebanon alieleza kuwa baadhi ya vijiji vimepata madhara makubwa na nyumba nyingi katika Bekaa na maeneo mengine zimeharibiwa hata hivyo, alisisitiza kuwa mapambano bado yanaendelea.
Ameashiria mchango mkubwa wa Waislamu wa Kishia katika muqawama wa Lebanon na kusema: “Uwiano wa mashahidi wa Kishia ukilinganisha na idadi ya watu wao ni mkubwa mno, hii inaonyesha kuwa Mashia wamekuwa mstari wa mbele katika kuilinda nchi yao.”
Kwa matumaini makubwa alisema: “Licha ya matatizo na uharibifu wote, mapambano yataendelea, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na msaada wa ndugu zetu katika nchi za Kiislamu, tutashinda.”
Sheikh Al-Khatib pia aligusia shahada ya Sayyid Hassan Nasrallah (r.a) na makamanda wa muqawama, akasema: “Mafanikio yote haya yamepatikana baada ya shahada ya Sayyid Hassan mpenzi wetu na makamanda wetu, katika hali ambapo hata huduma za mawasiliano kama simu zilikuwa hazipatikani, mapambano yaliendelea kwa ujasiri.”
Amebainisha kuwa: “Israel, pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa, haikuweza kufanikisha malengo yake, vikosi vitano kamili vya Israel havikuweza kuingia Lebanon, na hii ni dalili ya azma thabiti ya wapiganaji wa muqawama.”
Kwa kutukuza roho ya mapambano alisema: “Mafanikio haya yanathibitisha kuwa irada ya Mwenyezi Mungu na azma ya watu inaweza kushinda vifaa vya kijeshi vya kisasa zaidi, mapambano ya Lebanon yamedhihirisha kwamba kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kusimama kidete, ushindi unaweza kupatikana hata katika mazingira magumu zaidi.”
Sheikh Al-Khatib alisisitiza kuwa: “Mapambano ya Lebanon yamedhihirisha msimamo thabiti katika kulinda mamlaka na umoja wa ardhi ya Lebanon, tutaendelea na njia hii hadi ardhi ya Lebanon isafishwe dhidi ya kila nguvu ya kigeni.”
Ameongeza kusema: “Tajiriba hii imetuonyesha kuwa mapambano hayapaswi kuwa yenye nguvu tu kwenye uwanja wa vita, bali pia lazima yawe na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kisiasa na kijamii, leo muqawama umekuwa imara zaidi ya zamani.”
Aidha, alibainisha kuwa baada ya kushindwa kijeshi, utawala wa Kizayuni uligeukia vita vya kisaikolojia, kisiasa na vya vyombo vya habari, pamoja na kujaribu kuleta mashinikizo ya kiuchumi ili kuiweka Lebanon kwenye hali ngumu.
Sheikh Al-Khatib alisisitiza: “Mashinikizo haya hayakuidhoofisha harakati ya muqawama, bali yaliongeza zaidi azma yetu ya kuendelea na njia hii, leo muqawama wa Lebanon umesimama macho na imara zaidi ya zamani mbele ya njama hizi.”
Akasema: “Adui lazima ajue kwamba wananchi wa Lebanon, kwa mshikamano wao na muqawama wao, wamesimama kidete kupinga mashinikizo yote, na wanailinda ardhi na mamlaka yao.”
Katika kuzungumzia shambulizi la hivi karibuni la Israel dhidi ya Qatar, Sheikh Al-Khatib alisema: “Tukio lililotokea Qatar, licha ya kuwepo kwa kituo kikubwa cha kijeshi cha Marekani na uhusiano wa karibu wa nchi hiyo na Marekani, ni funzo kwa tawala zote za Kiarabu na za eneo hili.”
Ameongeza kuwa: “Tukio hili limeonyesha kwamba ahadi zote na misaada ambayo nchi za Kiarabu zimekuwa zikiahidiwa na Marekani haviwezi kuwalinda wakati wa dharura dhidi ya dhulma na tamaa ya adui. Hata Qatar, ambayo ilidhaniwa kuwa chini ya ulinzi wa Marekani, ililengwa.”
Rais huyo wa Baraza Kuu la Kishia Lebanon alihitimisha kwa kusema: “Tukio hili ni fursa ya kuyazindua mataifa ya eneo hili, inshaallah, litakuwa sababu ya kuamsha nchi za Kiarabu na kuziweka pamoja katika mshikamano dhidi ya tamaa za Marekani na Israel, njia pekee ya wokovu ni mshikamano na umoja.”
Sheikh Ali Al-Khatib, akisisitiza juu ya kielelezo cha mapambano, alisema: “Mataifa ya eneo hili lazima yajue kwamba uwepo wa nguvu za kigeni katika eneo hupelekea tu ongezeko la udhaifu, mfano wa muqawama wa Lebanon umethibitisha kwamba kwa kutegemea nguvu za ndani na mshikamano, kunawezesha kusimama imara dhidi ya uvamizi wowote.”
Mwisho wa hotuba yake alisema: “Nchi za Kiarabu zinapaswa kupata funzo kutoka tukio hili, na badala ya kutegemea nguvu za kigeni, zishikamane na kuungana ili kuchukua hatima yao mikononi mwao wenyewe.”
Maoni yako