Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, kikao cha kimataifa cha taasisi ya “Al-Baqi‘” chini ya uongozi wa Ayatollah Sayyid Hamidul-Hasan, mwanazuoni mashuhuri kutoka India, kiliandaliwa mjini Chicago, Marekani, kwa njia ya mtandaoni kwa kushirikisha wanazuoni, watafiti na wanaharakati wa kitamaduni na kidini, kikao hiki kilipokelewa kwa hamasa kubwa na ushiriki mpana wa hadhira.
Kujengwa Bustani Tukufu Jannatul-Baqi‘ kwa Heshima na adhama ya Ahlul-Bayt (a.s.):
Katika kikao hicho, Hujjatul-Islam Sayyid Mahbub Mahdi Abidi Najafi, mwanzilishi wa taasisi ya Al-Baqi‘, alieleza malengo na mipango ya taasisi hii, na kusema: “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa pamoja na timu thabiti, madhubuti na yenye bidii, ambayo usiku na mchana inafanya kazi ya kufufua na kueneza utamaduni wa Jannatul-Baqi‘.”
Mwanazuoni huyo kutoka India, akiendelea na hotuba yake, aliwashukuru waumini kwa dua zao na wajumbe wa taasisi hiyo kwa juhudi zao, akisisitiza nafasi ya azma na mshikamano wa pamoja katika kutimiza malengo ya kimungu alisema: “Kila dua ya dhati inayotamkwa kwa ajili ya kufufua Baqi‘ na kila hatua ya kujitolea na ikhlasi ya wanachama wa taasisi hii, kwa hakika ni mbegu inayopandwa katika historia, tuna yakini kwamba siku moja mbegu hizi zitachipua, na katika siku za usoni si za mbali, tutashuhudia maua yake.”
Aliendelea kusema: “Kama ambavyo waumini, kwa mioyo iliyojaa mapenzi juu ya Ahlul-Bayt (a.s.), wananyanyua mikono yao kwa dua, na wajumbe wa timu hii wanajitahidi usiku na mchana kwa lengo hili takatifu, tunaamini kwamba siku moja pazia za huzuni zitaondoka usoni mwa Baqi‘, na bustani tukufu yenye heshima na utukufu wa Ahlul-Bayt (a.s.) itasimamishwa katika Jannatul-Baqi‘ Bustani hiyo haitakuwa tu ukumbusho wa dhulma ya kale, bali pia itakuwa alama ya heshima, mshikamano na imani juu ya Umma wa Kiislamu.”
Mapenzi juu ya Qur’ani na Ahlul-Bayt (a.s.):
Ayatollah Sayyid Hamidul-Hasan, mwanazuoni kutoka India, katika hotuba yake alisisitiza nafasi ya kipekee ya hazina mbili adhimu alizoacha Mtume wa Uislamu (s.a.w), yaani Qur’ani Tukufu na Ahlul-Bayt (a.s.), akibainisha kwamba kudumu kwa utambulisho wa Kiislamu kunategemea mapenzi na utiifu wa kweli kwa hazina hizi mbili za Mwenyezi Mungu.
Kwa masikitiko, alisema kwamba wakati mwengine ndani ya Waislamu ukweli huu hupuzwa: “Baadhi yao huishia kwenye dhahiri ya Qur’ani pekee na hawawatendei haki Ahlul-Bayt wa Mtume kwa upendo wa kweli na wa kivitendo, hali ya kuwa Qur’ani na Ahlul-Bayt hawatenganishiki, bali ni lazima kuzingatiwa na kuheshimiwa pamoja.”
Aliendelea kusema: “Kama Umma wa Kiislamu katika historia nzima ungeonyesha na kudumisha mapenzi ya dhati kwa Ahlul-Bayt (a.s.), leo hii makaburi matukufu ya wakubwa hao yasingekuwa yameharibiwa na kudhalilishwa huko Baqi‘, mapenzi kwa Ahlul-Bayt si hisia za ndani pekee, bali ni jukumu la kivitendo linalopaswa kudhihirika katika mienendo, misimamo na jitihada zetu.”
Mwisho wa hotuba yake, alisisitiza wajibu wa wanazuoni wa Uislamu duniani kote kufikisha sauti ya dhulma ya Baqi‘ na umuhimu wa kuhuisha makaburi hayo kwa mataifa na taasisi za kimataifa.
Shughuli na Mipango ya Baadaye ya Taasisi ya Al-Baqi‘:
Sajjad Lakani, mmoja wa wajumbe wenye bidii wa taasisi ya Al-Baqi‘, katika mkutano huu alieleza baadhi ya hatua zilizotekelezwa na mipango ijayo ya taasisi hiyo. Alibainisha kwamba taasisi imekuwa ikishirikiana moja kwa moja na taasisi za kimataifa: “Tayari tumewasilisha ripoti na nyaraka zinazohusiana na dhulma, uharibifu na udhalilishaji uliofanywa katika Jannatul-Baqi‘ kwa Umoja wa Mataifa na taasisi za heshima za haki za binadamu, ili jamii ya kimataifa iweze kuufahamu ukweli huu.”
Aidha, alitangaza mipango ya baadaye ya taasisi hiyo na kusema: “Miongoni mwa mipango muhimu ijayo ni ukarabati na uundaji wa mfano wa Baqi‘ kwa sura ya bustani na mahala pa ziara karibu na Waadi-Salaam, hatua hii inaweza kuwa ukumbusho wa nafasi ya kiroho ya Baqi‘ na pia fursa kwa wageni na wapenzi kujenga uhusiano wa kihisia na kiroho na urithi huu wa thamani.”
Sababu Kuu ya kuiharibiu wa Baqi‘:
Hujjatul-Islam Sayyid Haidar Hasan Aal Najm al-Millat pia alisifu shughuli za taasisi na kusema: “Juhudi za wajumbe wa taasisi hii zitabaki daima katika historia, nia chafu za Muhammad bin Abdulwahhab ndio chanzo kikuu cha uharibifu wa Baqi‘, na hadi bustani tukufu zitakapojengwa upya, majeraha yake yataendelea kubakia.”
Sayyid Sadiq Ali, miongoni mwa waimbaji wa maombolezo ya Ahlul-Bayt, aliongeza: “Uharibifu wa makaburi ya Baqi‘ umetokana na chuki na uadui dhidi ya Ahlul-Bayt (a.s.), na vizazi vilivyoharibu makaburi hayo ilikuwa ni mwendelezo wa njia ile ile ya mababu zao, taasisi ya Al-Baqi‘ kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa imeimarisha na kuifanya harakati hii kuwa ya kidunia.”
Kutojali ni Hatari:
Hujjatul-Islam Aslam Rizwi, mwanazuoni mashuhuri kutoka India, alitoa ujumbe kwa wapenda haki duniani: “Hatupaswi kukaa kimya mbele ya uharibifu wa Baqi‘. Kila mtu anapaswa kujitahidi kadiri ya uwezo wake na akumbuke kwamba thawabu hupimwa kwa amali, si kwa matokeo, kusubiri matokeo hakupaswi kutuzuia kufanya kazi.”
Mkutano huu ulimalizika kwa msisitizo wa kuhuisha makaburi ya Ahlul-Bayt huko Baqi‘, kueneza utamaduni wa Ashura na kulinda urithi wa kidini na kiroho, washiriki walisisitiza kuendelea na shughuli za kitamaduni, kielimu na kidini katika kulihifadhi urithi wa Ahlul-Bayt na wakatangaza kuunga mkono juhudi za taasisi ya Al-Baqi‘.
Maoni yako