Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Miongoni mwa dalili muhimu zaidi za Wiyaatul-Faqih ni riwaya, katika toleo lililopita tulitaja tawqi’ ya Imam wa Zama (a.s.). Katika toleo hili tunashughulikia dalili nyingine ya nakili.
Maqbūlah ya ‘Umar bin Hanzalah
Miongoni mwa riwaya ambazo mafuqaha wamezitumia kuthibitisha Wiyaatul-Faqih ni riwaya iliyopokelewa na ‘Umar bin Hanzalah, ambayo anasema:
Nilimuuliza Imam Swadiq (a.s.):
“Iwapo wawili miongoni mwa mashia watatofautiana katika suala la deni au urithi, je, inajuzu kupeleka kesi yao kwa sultani [asiye wa haki] au kwa kadhi [aliyewekwa na sultani huyo]?”
Imam Swadiq (a.s.) akasema:
“Yeyote atakayekwenda kwao kwa ajili ya hukumu… basi hakika amekwenda kwa tāghūt na amemkubali kama hakimu. Na kile atakachohukumu huyo hakimu au kadhi wake ni haramu, hata kama haki iko upande wake; kwa kuwa alichopata kimetokana na hukumu ya tāghūt, yaani yule ambaye Mwenyezi Mungu ameamrisha kuhukumiwa kwake kwa ukafiri; kama Qur’ani Tukufu inavyosema:
يُرِيدُونَ أَنْ يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَنْ يَكْفُرُوا بِهِ
“[Baadhi ya watu] wanataka wapeleke mambo yao kwa hukumu ya tāghūt, ilhali wameamrishwa kumkufuru.”
(An-Nisā: 60)
‘Umar bin Hanzalah anaendelea kusema:
(Nilipomuona Imam akitaja kwa ukali namna hii kuhusu mashia kwenda kwa hakimu wa tāghūt na kadhi wake, nikauliza:)
“Basi mashia wafanye nini katika hali kama hiyo?”
Imam (a.s.) akasema:
يَنْظُرَانِ إِلَى مَنْ كَانَ مِنْكُمْ مِمَّنْ قَدْ رَوَى حَدِيثَنَا وَ نَظَرَ فِي حَلَالِنَا وَ حَرَامِنَا وَ عَرَفَ أَحْكَامَنَا فَلْيَرْضَوْا بِهِ حَكَمًا فَإِنِّي قَدْ جَعَلْتُهُ عَلَيْكُمْ حَاكِمًا فَإِذَا حَكَمَ بِحُكْمِنَا فَلَمْ يَقْبَلْهُ مِنْهُ فَإِنَّمَا اسْتَخَفَّ بِحُكْمِ اللَّهِ وَ عَلَيْنَا رَدَّ وَالرَّادُّ عَلَيْنَا، الرَّادُّ عَلَى اللَّهِ وَ هُوَ عَلَى حَدِّ الشِّرْكِ بِاللَّهِ
Wakati wawili miongoni mwa mashia wakitofautiana, waangalie na wazingatie ni nani miongoni mwenu anayepokea hadithi zetu, anayechunguza masuala ya halali na haramu yetu, na anayejua hukumu zetu [Ahlul-Bayt]. Basi mtu huyo wakubali kuwa hakimu baina yao; kwani mimi nimemweka huyo juu yenu kama hakimu, na atakapotoa hukumu kwa mujibu wa hukumu zetu, kisha aiitwekeleze, basi hakika amedharau hukumu ya Mwenyezi Mungu na amekataa hukumu yetu. Na anayekataa hukumu yetu, basi amekataa hukumu ya Mwenyezi Mungu, na hali hiyo ni sawa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu.
(Al-Kāfī, Juz. 1, uk. 67)
Masuala muhimu yaliyomo katika riwaya hii:
Katika migogoro, hairuhusiwi kwenda kwa hakimu wa tāghūt au kadhi aliyewekwa na yeye; kwani Qur’ani na Sunna zimeharamisha hilo.
Imam Swadiq (a.s.) amesema: “Katika hali kama hiyo, warejee kwa mpokezi wa hadithi zetu, anayezifahamu na kuzijua vyema hukumu zetu.” Ni wazi kwamba asiye kuwa faqihi au mujtahid hawezi kuwa na ufahamu kamili wa hukumu za Maimamu zilizomo katika hadithi zao.
Katika riwaya hii, swali lilihusu kesi baina ya watu wawili, lakini Imam Swadiq (a.s.) mwishoni alitoa kanuni ya jumla na ya kina aliposema:
فَإِنِّي قَدْ جَعَلْتُهُ عَلَيْكُمْ حَاكِمًاYaani Imam amemfanya faqihi kama hākim miongoni mwa mashia, na hākim ni yule mwenye mamlaka na uongozi juu ya wengine na anayeendesha mambo yao.
Imam (a.s.) akaongeza kwamba iwapo hakimu huyu aliyeteuliwa na Imam atatoa hukumu, basi ni lazima ikubaliwe. Kukataa hukumu hiyo ni sawa na kukataa hukumu ya Imam, na kukataa hukumu ya Imam ni kukataa hukumu ya Mwenyezi Mungu. Kwa tamko hili la jumla, faqihi amefanywa kuwa hoja juu ya watu katika hukumu zote—za mtu binafsi na za kijamii, za mahakama na zisizo za mahakama.
Faqihi mkubwa wa Kishia, Muhammad Hasan Najafi, maarufu kama Sāhib al-Jawāhir (aliyefariki 1266 H), anasema:
Uteuzi wa jumla wa mafuqaha ni katika mambo yote; kiasi kwamba kila kitu kilicho cha Imam, pia ni cha faqihi, kulingana na kauli ya Imam
فَإِنِّي قَدْ جَعَلْتُهُ عَلَيْكُمْ حَاكِمًا
Hii inamaanisha faqihi ana mamlaka katika hukumu na mambo mengine kama vile uongozi wa kisiasa, kama ilivyo katika tawqi’ tukufu la Imam wa Zama (a.s.):
فَإِنَّهُمْ حُجَّتِي عَلَيْكُمْ
Yaani, mafuqaha ni hoja juu yenu katika kila jambo ambalo mimi ni hoja, isipokuwa yale yaliyoondolewa kwa dalili.
(Jawāhir al-Kalām, Juz. 21, uk. 396–397)Mwalimu wa mafuqaha, marehemu Shaykh Ansari (aliyefariki 1281 H), anasema: Kile kinachoeleweka kutokana na neno hākim katika Maqbūlah ya ‘Umar bin Hanzalah ni “mtawala wa jumla” (mutasallit mutlaq), yaani pale Imam aliposema:
فَإِنِّي قَدْ جَعَلْتُهُ عَلَيْكُمْ حَاكِمًاYaani sawa na kauli ya sultani anapowaambia wakazi wa mji: “Nimemweka fulani kuwa hakimu juu yenu.” Kutokana na kauli hiyo, inaeleweka kwamba sultani amempa huyo mtu mamlaka juu ya mambo yote ya raia, makubwa na madogo, yanayohusu utawala.
(Kitāb al-Qaḍā wa al-Shahādāt, Shaykh Ansari, Sh. 22, uk. 8–9)
Kutokana na yote yaliyotangulia, inaonekana wazi kuwa faqihi anapata mamlaka yake kutoka kwa Imam Ma‘sūm, kwani katika tawqi’ ya Imam wa Zama (a.s.) na katika Maqbūlah ya ‘Umar bin Hanzalah, ni Imam mwenyewe anayemfanya faqihi kuwa hoja juu ya watu na hakimu wao. Kwa hivyo, faqihi ana Wiyaatul-Faqih kwa uteuzi wa Imam na hukumu yake.
Naam, kukubalika kwa faqihi katika uongozi wake na uwezekano wa kutekeleza mamlaka hiyo, kunategemea ridhaa na mapokezi ya watu.
Imenukuliwa kutoka kitabu “Nagin Āfarīnish”, huku ikifanyiwa mabadiliko kidogo)
Maelezo ya chini:
‘Umar bin Hanzalah alikuwa miongoni mwa masahaba wa Imam Bāqir na Imam Swadiq (a.s.), na alikuwa mpokezi mashuhuri wa hadithi ambaye masahaba wakubwa kama Zurārah, Hishām bin Sālim, na Ṣafwān bin Yaḥyā walipokea hadithi kutoka kwake. Neno Maqbūlah linamaanisha riwaya iliyokubaliwa na kuaminika na wanazuoni.
Faqihi huyu mkubwa alikuwa nguzo ya fiqh ya Kishia na mwandishi wa Jawāhir al-Kalām, kazi kubwa ya fiqh katika juzuu 43, ambayo kwa muda mrefu imekuwa rejea kuu ya mafuqaha katika hawza.
Maoni yako