Jumatatu 4 Agosti 2025 - 04:48
Sheikh al-Qattan: Watoto wa Ghaza wanakufa huku wakitamani kipande cha mkate

Hawza/ Sheikh Ahmad al-Qattan amesema kuwa: “Yale ambayo watu wetu wa Ghaza wanayapitia ni jukumu la Umma mzima, maulamaa, masultani, watawala, wakuu wa kifalme, wafalme na marais.”

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ahmad al-Qattan, Rais wa Jumuiya ya “Qawluna wal-Amal” nchini Lebanon, katika maandamano ya mshikamano na watu wa Ghaza yaliyofanyika katika makao makuu ya jumuiya hiyo katika eneo la "Bar Elias" na kuandaliwa na kamati ya wanawake ya chama hicho, alisisitiza juu ya ulazima wa kuondoa vikwazo na njaa, na akasema: “Yale ambayo watu wetu wa Ghaza wanayapitia ni jukumu la Umma mzima, maulamaa, masultani, watawala, wakuu wa kifalme, wafalme na marais, hili ni jukumu la kila binadamu huru katika ulimwengu huu.”

Akiuliza kwa kejeli, alisema: “Unawezaje, kama wanadamu, kukubali kwamba watoto, wanawake, wazee na wanaume wanakufa kwa njaa, huku ukishuhudia ukimya wa Kiarabu na Kiislamu kuhusu kuunga mkono watu wetu na ndugu zetu wa Ghaza?”

Sheikh al-Qattan, akiwahutubia maulamaa wa Umma, alisema: “Ujumbe wetu kwa maulamaa wa Umma ni huu: Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuulizeni, mmefanya nini kwa ajili ya watoto, wanawake, wazee na wanaume wa Ghaza? Mmefanya nini? Mmesema nini? Je, mmelisema neno la haki mbele ya madhalimu, mbele ya watawala waovu na waoga ambao mikono yao imejaa damu ya watu wetu na ndugu zetu wa Ghaza?”

Mwanazuoni huyu wa Kisunni aliendelea kwa kusema: “Mwenyezi Mungu atatuuliza sisi maulamaa wa duniani kote, sisi maulamaa wa dini, sisi maulamaa wa Umma wa Kiislamu. Atatuuliza: ‘Enyi maulamaa, je, mlipaza sauti zenu? Je, mliwaeleza watawala wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kwamba mnapaswa kufungua kivuko cha Rafah? Enyi watu wa Misri, enyi vijana, wazee na wanawake wa Misri, je, mmesimama dhidi ya wale wanaokifunga kivuko hiki? Je, mlipaza sauti zenu? Je, mliondosha kuzingirwa watu na ndugu zetu wa Ghaza? Je, mlifikisha dawa, chakula na maji kwao ili wasife kwa njaa?”

Aliongeza kwa kusema: “Je, jambo hili si jukumu mahsusi la maulamaa, watawala, tawala na viongozi wa ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu? Sisi ni Ahlus-Sunna. Je, watu wetu wa Ghaza si Waislamu na Ahlus-Sunna? Tunawezaje katika zama hizi kuridhia watu wetu na ndugu zetu wa Ghaza wafe kwa njaa na kiu?”

Sheikh al-Qattan alibainisha: “Je, si aibu kuona watoto wanakufa kwa njaa? Tunawaona watoto mwaka 2025 wakilia na kuiambia dunia kuwa tuna njaa, huku chakula kikimwagwa barabarani na kwenye mapipa ya taka. Tunawaona watoto wa Ghaza wakifa kwa njaa, wakitamani kipande cha mkate, unga au tonge la chakula.”

Rais wa Jumuiya ya “Qawluna wal-Amal”, akiyahutubia mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, alisema: “Ujumbe wetu kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu ni huu: Enyi mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, katika kila nchi ya Kiarabu na Kiislamu, Mwenyezi Mungu atatuuliza, hatuna udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu, ni lazima tushiriki kwenye maandamano ya mamilioni na kudai kumalizika vizuizi, kumalizika kwa uharibifu, kumalizika kwa mauaji na kumalizika kwa mauaji ya kimbari ya watu na ndugu zetu wa Ghaza.”

Sheikh al-Qattan aliwaomba wanawake duniani kote, wakiwemo wanawake Waislamu, wajifunze kutoka kwa watu huru wa Ghaza, kutoka kwa wanawake wa Ghaza na kutoka kwa mabinti wa Ghaza. “Tunawasalimu watu wa Ghaza, na tunawaambia kwamba; Lebanon pamoja na idadi kubwa ya watu wake, itasimama pamoja na Ghaza, pamoja na Palestina na pamoja na wanyonge na waliodhulumiwa duniani.”

Katika hitimisho, alisema: “Sisi kama Waislamu, Waarabu na wanadamu huru, lazima tuungane dhidi ya adui huyu, lazima tuunganishe juhudi na silaha zetu, na tuelekeze nguvu zetu zote kwa ajili ya kupambana na kukabiliana na adui huyu.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha