Jumapili 3 Agosti 2025 - 15:58
Onyo la Kiongozi wa Harakati ya Uamsho ya Umma wa Mustafa nchini Pakistan kuhusu njama ya kulazimisha kukubalika utawala wa Kizayuni katika nchi za Kiislamu

Hawza/ Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Jawad Naqvi, katika hotuba yake huku akionya juu ya jitihada kubwa za kulazimisha kukubalika kwa utawala wa Kizayuni katika nchi za Kiislamu, ametaja mchakato huu kuwa ni njama hatari dhidi ya Umma wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Jawad Naqvi, Kiongozi wa Harakati ya Uamsho wa Umma wa Mustafa nchini Pakistan, katika hotuba iliyotolewa katika Msikiti wa Bayt al-Atiq huko Lahore, huku akionya kuhusu jitihada kubwa za kulazimisha kukubalika kwa utawala wa Kizayuni katika nchi za Kiislamu, amesema kwamba mchakato huu ni njama hatari dhidi ya Umma wa Kiislamu.

Akinukuu maamuzi ya hivi karibuni ya baadhi ya nchi za Magharibi kuhusu kutambua taifa la Palestina, alisema: Tangazo la kuunga mkono kwa nchi kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani juu ya kuundwa kwa taifa la Palestina, kwa juu linaonekana kama hatua chanya, lakini kwa hakika ni hila ya kina na sehemu ya mpango tata wa kuhalalisha utawala wa Kizayuni. Hatua hii si tu kwamba haitasaidia watu wa Palestina, bali itasababisha kuimarika kwa nafasi ya kisheria na kimataifa ya Israel.

Historia ya suala la Palestina

Rais wa Chuo cha "al-‘Urwa al-Wuthqa" akielezea historia ya suala la Palestina aliongeza: Tangu mwaka 1948 hadi sasa, kuundwa kwa taifa huru la Palestina kumebakia tu kwenye ahadi na matamko, ilhali Israel katika miaka yote hii imegeuka kuwa nguvu ya kijeshi, kisiasa na kiuchumi. Sasa pia katika mwezi ujao wa Septemba, inatarajiwa kwamba katika Umoja wa Mataifa, taifa la kufikirika la Palestina litambuliwe rasmi, ambapo lengo kuu la hatua hiyo ni kuimarisha nafasi ya Israel katika ngazi ya kimataifa, na si kutimiza ndoto ya Palestina.

Nafasi ya Marekani na serikali iliyopita

Ameelezea pia nafasi ya Marekani na serikali yake iliyopita, akisema: Serikali ya Trump kwa kutumia nyenzo kama vikwazo, madeni makubwa, mikataba ya mafuta na makubaliano ya kibiashara, ilizisukuma nchi za Kiislamu kuelekea hali ambayo italazimika kuikubali Israel. Katika mazingira haya, japokuwa baadhi ya watawala wa Kiislamu wanaweza kuwa na mwelekeo wa jambo hili, maamuzi ya mwisho juu ya hili hufanywa sehemu nyingine; watawala ni watekelezaji tu wa mipango iliyobuniwa na nguvu za kibeberu.

Onyo kali kwa nchi za Kiislamu

Kiongozi wa Harakati ya Uamsho wa Umma wa Mustafa, katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake alisisitiza: Iwapo nchi za Kiislamu zitakubali njama hii, hatua hiyo itakuwa ni usaliti wa wazi kwa damu ya mashahidi wa Ghaza. Adui safari hii hapigani kwa risasi, bali anatumia hila, mikataba na diplomasia. Uelewa, umoja na upinzani dhidi ya mpango huu ni jukumu la kidini, kimaadili na kibinadamu ambalo Umma wa Kiislamu haupaswi kulipuuza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha