Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, maandishi ya tamko la Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum katika kulaani hatua ya chuki dhidi ya Iran ya Umoja wa Ulaya ya kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa la kigaidi ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Hatua isiyo halali na yenye uadui dhidi ya Iran iliyochukuliwa na Umoja wa Ulaya ya kulitaja Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa la kigaidi, kwa mara nyingine imebainisha kiwango cha juu kabisa cha chuki na uadui wao dhidi ya taifa la Iran.
Tawala zinazokuza ugaidi na ufisadi, ambazo kwa miaka mingi zimehifadhi na kulinda makundi ya kigaidi ya Wanafiki (Munafiqin), na katika fitna za hivi karibuni ziliunga mkono ghasia na mashambulizi ya mamluki dhidi ya mali na maisha ya watu wa Iran; leo kwa ujasiri usio na haya, zinatoa matamko ya kisiasa na ya kichokozi dhidi ya jeshi la wananchi zaidi duniani.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ambalo kwa miaka mingi lilipambana na kundi la kigaidi lenye kiu ya damu zaidi, lililokuwa zao la serikali ya Marekani, na kwa kuwakandamiza magaidi wakatili wa Daesh (ISIS), limechangia kwa kiwango kikubwa usalama wa sasa wa nchi mbalimbali, zikiwemo nchi za Ulaya; leo linawezaje, kwa hoja ipi ya kisheria na ya kiakili, kuitwa la kigaidi na Umoja wa Ulaya?
Katika siku zile ambapo utawala wa kigaidi wa Israel ulikuwa ukiishambulia Ghaza na Palestina kwa mauaji ya kutisha zaidi, je, silaha za Magharibi na uungaji mkono wao wa kisiasa hazikuongeza moto wa mauaji hayo?! Na je, wao hawakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono utawala mkubwa zaidi wa kigaidi duniani?!
Watu duniani wanajua vyema ni utawala gani wa kigaidi ambao kwa shambulio la usiku, ulimteka nyara rais halali wa nchi huru na kujinyooshea makucha kwenye rasilimali na utajiri wa taifa hilo.
Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum, sambamba na kutangaza uungaji mkono wake thabiti kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa watoto wote wa taifa waliomo katika majeshi ya ulinzi, inalaani vikali hatua ya kijinga na yenye uadui ya Umoja wa Ulaya ya kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi kuwa la kigaidi, na inatangaza kwamba: Jeshi lenye nguvu la Walinzi wa Mapinduzi, machoni mwa wapenda uhuru duniani na watu wanyonge ulimwenguni, ni alama ya ubinadamu, uzalendo na kudai haki.
Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wapo mstari wa mbele katika kulinda misingi ya Kiislamu na ya kimapinduzi ya watu wa Iran, na katika njia hii wanajitolea na kupigania kwa kujitoa muhanga.
Utambulisho wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni mapambano ya kudumu dhidi ya dhulma na ukafiri wa kimataifa, na taasisi hii ya wananchi itaendelea kubaki thabiti juu ya azma hiyo daima.
Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Elimu ya Dini ya Qum Iran
Maoni yako