Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Sayyid Husayn Khurshid Abidi, mmoja wa wazungumzaji na watafiti wa Bangladeshi, katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Hawza, alieleza: Arubaini ni harakati kubwa inayofikisha ujumbe wa Imam Hussein (as) zaidi ya mipaka ya dini na nchi, na inawaalika wanadamu wote kushikamana na ukweli na kupambana na dhulma.
Tafadhali eleza kuhusu maana ya Arubaini na sababu ya umuhimu wake kwetu.
Sayyid Husayn Khurshid Abidi: Arubaini si tu hafla ya maombolezo; bali ni alama ya kusimama dhidi ya dhulma na kutetea haki na uadilifu. Zaidi ya miaka 1400 iliyopita huko Karbala, Imam Hussein (as) na wafuasi wake walitoa maisha yao kwa ajili ya kulinda thamani za kibinadamu na za Mwenyezi Mungu. Siku ya arobaini tangu kuuawa kishahidi, yaani Arubaini, ni ukumbusho wa kujitolea huku kukubwa, na kila mwaka mamilioni ya watu kutoka pembe zote za dunia hukusanyika ili kuhuisha ujumbe wake na kuhifadhi thamani hizi kwa mshikamano.
Kwa nini Arubaini leo imekuwa harakati ya ulimwengu?
Sayyid Husayn Khurshid Abidi:
Sababu ni ujumbe wa kibinadamu na wa kudai haki wa Arubaini ambao hauzuiliwi na taifa au dini moja tu. Kila mwaka watu wenye tamaduni na dini mbalimbali, Waislamu na wasio Waislamu, huenda kwa miguu kuelekea Karbala, na wote kwa pamoja husema: "Labbayka ya Hussein (as)". Umoja na mshikamano huu ndio ulioifanya Arubaini kuwa harakati ya kimataifa iliyovuka mipaka ya kijiografia
Tunawezaje kuutambulisha vizuri ujumbe halisi wa Imam Hussein (as) na umuhimu wa Arubaini katika dunia nzima?
Sayyid Husayn Khurshid Abidi:
Kazi muhimu zaidi ni kuufikisha historia na ukweli kwa usahihi. Kwa bahati mbaya, katika baadhi ya maeneo kuna upotoshaji na makosa mengi kuhusu historia, tunapaswa kwa msaada wa vyombo vya habari, vitabu, filamu na mitandao ya kijamii, kuonyesha ukweli kwa njia iliyo sahihi na rahisi kueleweka, ujumbe wa Imam Hussein (as) ni kuhusu haki, ujasiri na ubinadamu, na tunapaswa kukumbusha watu wote kwamba ujumbe huu si maalumu kwa kundi au dini moja, bali ni kwa ajili ya wanadamu wote.
Ujumbe wa Imam Hussein (as) una umuhimu gani katika hali ya sasa duniani?
Sayyid Husayn Khurshid Abidi:
Leo pia katika dunia tunashuhudia dhulma, ufisadi, vita na uvunjaji wa haki za binadamu. Ujumbe wa Imam Hussein (as) ni kwamba hatupaswi kunyamaza mbele ya dhulma na ni lazima tusimame, hata kama maisha yetu yako hatarini. Ujumbe huu si wa Waislamu pekee; bali ni kwa wote wanaoamini katika haki na uhuru na walio tayari kupigania hayo.
Una ushauri gani kwa wale wasioijua Arubaini?
Sayyid Husayn Khurshid Abidi:
Ushauri wangu ni kwamba iwapo inawezekana, washiriki angalau mara moja katika ibada ya Arubaini ili wahisi kwa karibu mazingira ya kiroho na ujumbe wake. Lakini iwapo hawana uwezo huo, basi angalau wafungue mioyo yao kwa mafundisho ya Imam Hussein (as) na katika maisha yao ya kila siku wajitahidi kwa ajili ya haki na kupambana na dhulma. Ujumbe mkuu wa Arubaini ni kwamba "kila siku ni Ashura na kila mahali ni Karbala"; yaani kila wakati na kila mahali ni lazima tusimame dhidi ya dhulma.
Hitimisho
Arubaini leo si tena hafla ya kidini pekee; bali ni harakati ya ulimwengu kwa ajili ya haki, usawa na ubinadamu. Imam Hussein (as) ni mwenge ambao kwa maelfu ya miaka umeangaza njia ya ubinadamu na daima utaendelea kuangaza.
Maoni yako