Shirika la Habari la Hawza - Katika utafiti wa wilayat faqihi, mojawapo ya mada muhimu zaidi ni hoja za wilayat faqihi, mara nyingi hili swali limekuwa likiulizwa kwamba: Kwa nini katika jamii ya Kiislamu, faqihi anapewa kipaumbele juu ya wengine na ndiye mwenye wilaya juu ya wote?
Kwa kujibu swali hili, tunasema: hoja ya wilayat faqihi inaweza kuchambuliwa kiakili na kinakili; yaani, akili inamuamrisha Muislamu kumtii faqihi katika zama za ghaiba, na riwaya za Kiislamu pia zinathibitisha hivyo.
Uchambuzi wa Hoja ya Kiakili Kuhusu wilayat Faqihi
Kwa kuwa mwanadamu anaishi kwa sura ya kijamii na anataka kupitia maisha haya afikie ukamilifu wa kiroho, anahitaji mambo mawili ya msingi:
1. Sheria ya Mwenyezi Mungu ambayo kwa sababu ya kuwa ya Kiungu, haina upungufu, udhaifu, au kosa lolote, ili iweze kuratibu mfumo wa kijamii na utekelezaji wake uhakikishe ufanisi na ustawi wa wote, sheria hii si nyingine bali ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna, ambayo ni mpango kamili na wa kina wa mwanadamu hadi Siku ya Kiyama.
2. Mtekelezaji na mtawala mwenye elimu na uadilifu ambaye atabeba jukumu la utekelezaji kamili wa sheria hiyo.
Ni dhahiri kwamba bila ya mambo haya mawili, au kwa kukosekana hata kimoja kati yake, jamii ya mwanadamu itakumbwa na machafuko, uharibifu, na maovu.
Matokeo ya hoja hii ya kiakili yanaonyesha ulazima wa unabii wa Mitume, na baada ya Nabii wa Mwisho, ulazima wa uimamu wa Maimamu Maasumu (as); yaani, mtu bora zaidi kwa ajili ya kutekeleza sheria za Kiungu na kutimiza hukumu za Mwenyezi Mungu ni Imam Maasum.
Maasum ni yule ambaye hana dhambi, kosa, au upungufu wowote katika fikra, mawazo, au matendo yake, sasa tunaiuliza akili: Iwapo hakuna upatikanaji wa Maasum, ni nini kifanyike?
Akili inajibu kwamba kwa kuwa haja ya utaratibu wa kijamii kwa mwanadamu na jitihada za kufikia ukamilifu wa kibinadamu na wa Kiungu bado ipo, basi ni lazima kumweka mtu aliye karibu zaidi na Maasum katika nafasi yake.
Ufafanuzi wa jambo hili ni kwamba sababu ya ustahiki wa Maasum kushika wilaya na uongozi kwa umma ni elimu yake kamili na ya kina kuhusu dini na mafundisho ya dini, pamoja na uchamungu, na isma yake vinavyomzuia kuyafanya maslahi ya umma kuwa kafara kwa manufaa binafsi na matamanio ya nafsi.
Sababu nyingine ya ustahiki wa Maasum ni uelewa na ufahamu wake wa masuala ya kijamii na uwezo wake wa kupanga na kuyasimamia.
Hivyo basi, ikiwa katika zama kama za ghaiba, upatikanaji wa Maasum hauwezekani, ni lazima kumtafuta mtu mwenye sifa hizi zaidi kuliko watu wengine, na mtu huyu si mwingine bali ni faqihi mwenye uchamungu ambaye ana uwezo wa kutosha wa kusimamia mambo ya jamii na watu; kwa sababu asiye faqihi hana elimu kamili ya Uislamu, hukumu, na mafundisho yake kiasi cha kuweza kuwa mtekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu, na mtu mwenye elimu bila ya ucha Mungu na uadilifu yupo katika hatari ya matamanio yake binafsi na ya wengine, hivyo haiwezekani kuikabidhi serikali ya Waislamu kwa asiye mwaminifu. Aidha, ikiwa hana uwezo wa usimamizi, atakosa uwezo wa kupanga mambo ya watu na katika nyakati za dharura hatoweza kufanya maamuzi sahihi na yenye manufaa kwa jamii ya Waislamu.
Utafiti huu unaendelea…
Imenukuliwa kutoka katika kitabu "Negin-e Āfarinish", huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi.
Maoni yako