Kwa mujibu wa idara ya kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Sheikh Muhammad Yaqubi, mmoja wa maulamaa mashuhuri wa Iraq, kupitia tamko lake rasmi ametoa wito wa kutolewa msaada wa haraka kwa watu wa Ghaza wanaoendelea kupigana bila silaha.
Matini ya tamko hilo ni kama ifuatavyo:
Bismillahir Rahmanir Rahim
Vyombo vya habari vimerusha picha zenye kutia uchungu mkubwa mno zinazo onesha janga la njaa na ukame ambao kwa sasa umeyakumba maisha ya watu wanaojihami na waliodhulumiwa wa Ghaza; picha ambazo zinauchoma moyo wa kila mtu mwenye hisia na dhamira, na hata jiwe gumu litakuwa laini kutokana na huzuni hiyo kubwa.
Amirul-Mu'minin Ali (as) kwa ajili ya tukio dogo sana kuliko hili, pale iliporipotiwa kuwa majeshi ya Muawiyah yamevamia mji wa Anbar na kupora mapambo ya mwanamke ambaye si Mwislamu aliye chini ya ulinzi wa serikali ya Kiislamu, alisimama juu ya mimbari ya Kufa akiwa na moyo uliojaa maumivu na huzuni na katika hotuba yake akasema: “Iwapo Mwislamu atasikia tukio hili (la kushambuliwa mwanamke ambaye si Mwislamu aliyekuwa chini ya ulinzi wa serikali ya Kiislamu), kisha akafa kutokana na huzuni, hatastahili kulaumiwa, bali mimi naona ni kifo cha haki.” (1)
Basi iweje waumini wakae kimya mbele ya janga kubwa la kibinadamu kama hili?
Tunaitaka serikali ya Iraq ianze mazungumzo na serikali ya Misri ili kuandaa mazingira ya kupitisha kwa urahisi misaada ya chakula na dawa za lazima ambazo zinaweza kuyaokoa maisha ya watu wa Ghaza kutokana na kifo.
Wananchi wa Iraq nao, kwa uwezo wao wote, watasimama kidete ili kufikisha misaada hiyo na kuwasaidia ndugu zao walioko katika dhiki.
"وَاللَّهُ مَعَكُمْ وَلَنْ يَتِرَكُمْ أَعْمَالَكُمْ."
Na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi, wala hatakunyimeni malipo ya vitendo vyenu.
(Muhammad: 35)
"وَمَا تُقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ اللَّهِ هُوَ خَيْرًا وَأَعْظَمَ أَجْرًا."Na kheri yoyote mnayo itanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtaikuta kwa Mwenyezi Mungu, imekuwa bora zaidi, na ina thawabu kubwa sana.
(al-Muzzammil: 20)
Muhammad Yaqubi – Najaf Ashraf
25 Muharram 1447 Hijria
21 Julai 2025 Miladia
--------------------------------------------------------------------------------
(1) Nahjul-Balagha, Juzuu ya 1, Ukurasa wa 69
Maoni yako