Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Dkt. Muhammad Tahir al-Qadri, mkuu wa harakati ya Minhaj al-Qur’an mjini Lahore, Pakistan, katika hotuba yake alisisitiza kwamba mapenzi na kufuata Qur'ani Tukufu na Ahlul-Bayt wa Mtume (as) ni dhamana thabiti ya kubakia katika njia ya uongofu na kuokoka dhidi ya upotofu.
Akinukuu maneno ya Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw), alibainisha kuwa: Ahadi hii ya kimungu haijatolewa na mtu wa kawaida, bali imetoka kwa Mtume wa Mwisho (saw) mwenyewe kwa ajili ya umma.
Kiongozi wa harakati ya Minhaj al-Qur’an Pakistan aliongeza: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: “Enyi watu! Ninawaachieni kati yenu vitu viwili vya thamani kubwa, mkivishikamana navyo, hamtapotoka kamwe; Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul-Bayt wangu, msivitenganishe viwili hivi na vishikeni kwa nguvu.”
Dkt. Tahir al-Qadri akiendeleza hotuba yake, alieleza kuwa: Hadithi hii tukufu, ambayo imenukuliwa katika vyanzo sahihi vya Kiislamu ikiwemo na al-Tabarani, inaangazia nafasi ya juu ya Ahlul-Bayt wa Mtume (as) katika kuwaongoza Ummah wa Kiislamu. Alinukuu kutoka kwa Mtume (saw) akisema: “Msitangulie Ahlul-Bayt wangu, kwani mtaangamia; wala msijifanye kuwafundisha jambo, kwa sababu wao ni wajuzi zaidi kuliko ninyi.”
Alisisitiza kwa kusema: Wale wanaobeba mapenzi ya Ahlul-Bayt (as) mioyoni mwao na kushikamana na mwenendo na njia yao, hawatapotea kutoka katika njia ya haki, bali Mwenyezi Mungu huwajaalia maisha yao kuwa yenye baraka na yaliyojaa kheri na rehema. Kinyume chake, wale wanaowadharau Ahlul-Bayt, hunyimwa baraka ya maisha, na Siku ya Kiyama watamkabili Mtume (saw) wakiwa na nyuso zilizotiwa weusi; hali inayodhihirisha ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na kunyimwa kwao uombezi.
Maoni yako