Alhamisi 10 Julai 2025 - 20:30
Kiongozi wa Harakati ya Minhaj-ul-Qur’an ya Pakistan: Mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as) ni sehemu isiyoepukika ya imani kwa mujibu wa Mtume Mtukufu (saw)

Hawza/ Katika kipindi cha kukaribia siku za maombolezo ya Muharram, mkutano wa “Ujumbe wa Imam Hussein (as) na Umoja wa Umma” ulifanyika katika mji wa Lahore, Pakistan kwa ushiriki mkubwa wa wanazuoni na wanafikra kutoka madhehebu mbalimbali ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjuma cha  Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kuwadia kwa mwezi wa Muharram, mkutano mkubwa uliopewa jina la “Ujumbe wa Imam Hussein (as) na Umoja wa Umma” uliandaliwa na harakati ya Minhaj-ul-Qur’an katika mji wa Lahore nchini Pakistan. Katika kongamano hilo, wanazuoni mashuhuri kutoka madhehebu tofauti ya Kiislamu walihudhuria na kusisitiza nafasi muhimu ya Ahlul-Bayt (as) katika imani ya Kiislamu na mchango wa harakati ya Ashura katika kulinda umoja wa umma.

Dkt. Muhammad Tahir-ul-Qadri, mwanzilishi na kiongozi wa harakati ya Minhaj-ul-Qur’an, katika hotuba yake alisema:

“Kuuawa kwa Imam Hussein (as) hakupaswi kuangaliwa tu kama kuuawa kwa mtu mmoja, bali tukio hilo ni udhalilishaji wa moja kwa moja kwa Mtume Mtukufu (saw), na kila aina ya udhia kwa Mtume (saw), kwa mujibu wa aya za Qur’an, ni kufuru ya wazi kabisa.”

Akiashiria hadithi maarufu ya Mtume Mtukufu (saw), alisisitiza kwa kusema:

Hussein anatokana nami nami natokana na Hussein” – kauli hii ya Mtume (saw) inaonesha wazi kwamba mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as) ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na imani, kutojali mapenzi haya humuangusha mtu kutoka katika njia ya uongofu.

Khurram Nawaz Gandapur, Katibu Mkuu wa Minhaj-ul-Qur’an, katika hotuba yake alisema:

“Harakati ya Ashura imeufundisha Umma wa Kiislamu uwezo wa kusimama dhidi ya dhulma na ufisadi, mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as) ni kiini cha imani na ni dhamana ya kuuamsha umma.”

Dkt. Ziaullah Shah Bukhari, kiongozi wa Jamaat Ahl-e-Hadith ya Pakistan, naye katika hotuba yake alisema:

“Kuendeleza kumbukumbu ya Imam Hussein (as) ni sehemu ya sunna ya Mtume (saw), Ahlul-Bayt (as) ni chemchemi ya ukweli na usafi, yeyote anayewapenda, hupata mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.”

Akiashiria juhudi za Dkt. Tahir-ul-Qadri, alisema: “Mimi niko pamoja na harakati ya Minhaj-ul-Qur’an kwa sababu wao wanaeneza utamaduni wa mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as) ndani ya jamii.”

Mufti Sayyid Ashiq Hussain Shah, pia alisema:

“Kama vile Nabii Ibrahim (as) alivyomwomba Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ardhi salama, leo harakati ya Minhaj-ul-Qur’an inapeleka ujumbe wa amani, umoja na usalama kote ulimwenguni, Dkt. Qadri ameweza kwa mwangaza wake kufichua tofauti kati ya fikra ya Husseini na fikra ya Yazidi mbele ya watu.”

Mwisho wa mkutano huo, Dkt. Mir Muhammad Asif Akbar Qadri, kwa kuwapongeza wanazuoni waliohudhuria kongamano hilo, alisisitiza juu ya umuhimu wa kuendeleza njia ya umoja na kueneza utamaduni wa Ashura.

Kongamano hili lilikuwa dhihirisho la kuvutia la umoja wa Kiislamu, mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as) na uenezaji wa ujumbe wa kimataifa wa Imam Hussein (as), jambo ambalo lilipata mwitikio mkubwa katika mazingira ya kidini na kitamaduni ya Pakistan.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha