Ijumaa 28 Februari 2025 - 13:27
Wasia wa Allamah Abdullah Al-Mamaqani kwa Mwanae

Hawza / "Itafute Dunia (itafute mali, pambana uwe tajiri uondokane na umasikini na ufukara,) kama kwamba hutokufa na utaishi milele duniani, lakini tenda (fanya amali njema) kwa ajili ya kuitafuta Akhera kama kwamba utakufa kesho".

Shirika la Habari la Hawza – Samahat Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C), katika Darsa lake la Akhlaq ya Kiislamu (Maadili ya Kiislamu), linalobeba anuani ya “Wasia wa Baba”, ameyanukuu maneno mazuri ya Wasia wa Mwanachuoni wetu mkubwa, Allamah Abdullah Al-Mamaqani kwa Mwanae, ambapo alimwambia Mwanae:

"أوصيك بني وفقك الله لكل خير وجنبك من كل سوء وشر بإخراج حب الدنيا عن قلبك"

“Nakuusia Mwanangu Mwenyezi Mungu akupe kila la kheri na akulinde / akukinge na mabaya yote na shari zote kwa kuyaondoa mapenzi ya dunia moyoni mwako”

Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, akifafanua maneno haya mazuri ya Allamah Al-Mamaqani amesema:

Allamah Abdullah Al-Mamaqani katika Wosia huu hakuwa akimuusia mwanae tu, bali anatuusia sisi sote na vijana wote kuitoa dunia katika mioyo yetu. Kwamba tuhakikishe tunaifanya dunia kuwa ni namba mbili, na Akhera kwetu iwe ni namba moja.

Hivyo katika wosia huu, Allamah Al-Mamaqani anamwambia mwanae ahakikishe kuwa mawazo yake yote na fikra zake zote zinakuwa kwa ajili ya kuitafuta Akhera, kisha ndio aitafute dunia. Kwamba Mwanangu isiwe kwako wewe Dunia ndio ya kwanza, kisha ndio Akhera, hapana! Bali itangulize Akhera kwanza, kwa sababu Mwenyezi Mungu atakwenda kukuuliza, atazungumza na wewe, na atakuhoji kwa kila jambo lako ulilolitenda duniani, kwahiyo hakikisha kwanza unafikiria juu ya Akhera, na unajiandaa vizuri kwa ajili ya Akhera yako, kisha ndio uitafute dunia. Wosia huu unaelekezwa kwetu sote kwamba juhudi zetu za kwanza ziwe ni kwa ajili ya Akhera, kisha ndio tuitafute Dunia.

Kwa nini usiitangulize Dunia? Al-Allamah Al-Mamaqani anasema:

"فإنه سمٌ ناقع وداءٌ مهلك وقائدُك إلى النار ومبعدك عن نيل ألطاف الملك الجبار"

“Ni sumu mbaya na ni ugonjwa hatari, na itakupeleka kwenye Moto wa Jehanamu na kukuweka mbali na Fadhila za Mfalme (Al-Malik) Al-Jabbar”.

Akifafanua maneno hayo amesema kuwa:

Al-Allamah Al-Mamaqani, anamwambia Mwanae kuwa Dunia ni sumu inayoua, na sio sumu tu, bali ni sumu mbaya inayoua, ukiishikilia dunia ujue utakufa vibaya sana, hii dunia ni ugonjwa unaomuangamiza mtu, na sio ugonjwa tu, bali ni ugonjwa hatari unaomuangamiza mtu yeyote aliyeipupia Dunia ya kupita na kusahau kuwa Akhera ndio maisha ya milele. Ukishaanza kuitia nafsi yako kwenye mambo ya kidunia, ujue wewe Akhera hutoijali tena.

Na ukisha ivua Akhera na ukajishughulisha na Dunia, basi ujue kuwa Dunia hiyo ni Kiongozi wako kuelekea katika Moto wa Jahannam. Mwenyezi Mungu atukinge na hilo.

Amirul-Muuminina Ali bin Abi Talib (a.s) amesema:

"اِعْمَلْ لِدُنْيَاكَ كَأَنَّكَ تَعِيشُ أَبَداً وَاِعْمَلْ لآِخِرَتِكَ كَأَنَّكَ تَمُوتُ غَداً"

“Fanyia kazi dunia hii kana kwamba utaishi milele, na fanyia kazi akhera yako kana kwamba utakufa kesho”. (Rejea: Manla Yahdhurhu Al-Faqih, Juzuu ya 3, Ukurasa wa 156, Al-Wafi, Juzuu ya 17, Ukurasa wa 41, Mustadrak Al-Wasa’il, Juzuu ya 1, Ukurasa wa 149).

Amirul-Muuminina (amani iwe juu yake) anatwambia kuwa: Itafute Dunia (itafute mali, pambana uwe tajiri uondokane na umasikini na ufukara,) kama kwamba hutokufa na utaishi milele duniani, lakini tenda (fanya amali njema) kwa ajili ya kuitafuta Akhera kama kwamba utakufa kesho.

Maneno haya Matukufu ya Amirul Muuminin (amani iwe juu yake), yanaendana na ufafanuzi tulioutoa kuhusiana na Wosia wa Allamah Al-Mamaqani kwa Mwanae kuwa anamtaka Mwanae aitangulize Akhera kwanza, kisha ndio aitafute Dunia, kwa sababu ikiwa wewe utakuwa ni mwenye kuipenda sana Dunia kuliko Akhera, basi utambue kuwa hiyo ni sumu mbaya inayoua, na ni ugonjwa hatari unaoangamiza, na itakuongoza kukupeleka motoni, na itakuaondoa katika kuzipata rehema na fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ndiye Mfalme wa wafalme, Al-Jabbar.

Mwanangu, Kijana wangu, Mwenyezi Mungu akupe Taufiq katika kuitanguliza Akhera mbele ya Dunia.

Wassalam Alaikum warahmatullah wa Barakatuh.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha