Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Al-Udhma Sheikh Bashir Hussein Najafi, miongoni mwa Maraji' wa Najaf Ashraf, ametoa taarifa ya rambirambi akieleza masikitiko yake makubwa kufuatia kufariki Ayatullah Al-Udhma Sheikh Hussein Wahid Khorasani, Maraji' mkubwa na mlezi mashuhuri wa Hawza.
Maandishi ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
Ambao wanapopatwa na msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika kwake Yeye tutarejea.
[Suratul-Baqarah: Aya ya 156]
Kwa huzuni, maumivu na masikitiko makubwa mno, tumepokea habari za kufariki mwanachuoni mwenye kutekeleza elimu yake kwa vitendo, mtetezi wa ngome ya Wilaya ya Muhammad na kizazi chake kitoharifu (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao), mlezi mkuu wa zama hizi, kiongozi wa Hawza ya kielimu ya Qum na mfasiri wa masuala ya zama zake; Marji' mwenye hadhi kubwa, Ayatullah Al-Udhma Sheikh Hussein Wahid Khorasani (Mwenyezi Mungu autakase udongo wake wa kaburi).
Baada ya kuishi kwa takribani karne moja, sehemu kubwa ya maisha yake ikiwa imetumika katika kuleta athari, kuwa na ushawishi na kujenga Hawza za kielimu, hatimaye amerejea kwa Mola wake. Katika kipindi chote cha maisha yake yenye baraka, aliwaandaa na kuwalea wanazuoni wengi.

Kwa hakika, kufariki mwanachuoni huyu mtukufu kumeacha pengo ambalo hakuna kitu kinachoweza kuliziba. Kwa hiyo, tunamwelekea Mwenyezi Mungu pekee kwa kulalamika na kumwelezea huzuni yetu. Pia tunatoa rambirambi zetu kwa Mtukufu Sahibuz-Zaman (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), Hawza, waumini wote, na hasa wanawe watukufu pamoja na familia yake tukufu, kufuatia msiba huu mkubwa.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu, Aliyebaki milele na Aliye Juu kabisa, amfunike kwa rehema na radhi Zake, na amuweke katika makazi ya kweli, pamoja na wapenzi na wasaidizi wa Muhammad na Aali Muhammad (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao).
Wala hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliye Juu na Mtukufu.
Bashir Hussein Najafi
7 Jamadithani 1448 Hijria
Maoni yako