Jumapili 8 Novemba 2026 - 20:48
Hawza yaitahadharisha Serikali ya Bahrain/ Hatutarejea Nyuma Katika Kutetea Haki za Wananchi wa Bahrain na Wanazuoni Wetu Wakubwa

Hawza/ Mkurugenzo wa Hawza nchini Iran, Ayatullah Alireza A'rafi, ametoa tamko kali la kulaani hatua za ukandamizaji zinazotekelezwa na utawala wa Bahrain pamoja na mahakama za kubuni zinazotumiwa dhidi ya wanazuoni wa dini.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, maandishi kamili ya tamko la Mkuu wa Hawza nchini Iran, la kulaani hatua za ukandamizaji za utawala wa Bahrain na mahakama za kubuni dhidi ya wanazuoni wa dini, ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

«Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi imara kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Wala chuki za watu fulani zisiwe sababu ya nyinyi kuacha kutenda haki. Fanyeni uadilifu, kwani huo ndio ulio karibu zaidi na uchamungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za yote mnayoyatenda». (Surat Al-Ma'idah, aya ya 8).

Katika hali ambayo uadilifu umekuwa jukumu kuu la Mitume wa Mwenyezi Mungu, hatua za hivi karibuni za serikali ya Bahrain si tu kwamba zimevuka mipaka ya dhuluma, bali pia ni mfano wa wazi wa «uvunjaji wa haki za msingi» na «shambulio la moja kwa moja dhidi ya nguzo za uongofu wa Umma». Sisi hatuzichukulii hatua hizi kama kosa la kisiasa, bali tunaziona kuwa ni sera ya makusudi ya ukandamizaji, ambayo lengo lake ni kudhoofisha nafasi ya dini na Uislamu.

Kutolewa hukumu za mahakama mnamo tarehe 8 Februari 2026 dhidi ya zaidi ya watu 60 miongoni mwa wasomi mashuhuri, maprofesa wenye vyeo vya juu na viongozi mashuhuri wa Hawza, pamoja na kutengwa tarehe 17 Aban 1405 (8 Novemba 2026) kwa ajili ya kutekeleza hukumu hizo zisizo za haki, ni njama ya wazi inayolenga kukabiliana na alama na mihimili ya kielimu na kidini ya Mashia.

Mahakama hizi za kubuni, ambazo hazina uhalali wowote kwa mujibu wa Sheria wala hadhi yoyote ya kisheria, si chochote isipokuwa vyombo vya kikatili vinavyotumiwa kutekeleza shinikizo la kisiasa na kukandamiza uhuru wa kidini.

Kwa niaba ya wanazuoni wakubwa, maprofesa, wanafunzi wa Hawza na wanazuoni wenye elimu na maarifa ya kina katika Hawza, tunasisitiza mambo yafuatayo:

Kwanza: Onyo kali kwa serikali ya Bahrain

Tunaionya serikali na utawala wa Bahrain kwamba njia mnayoifuata kwa sasa ni njia inayoelekea katika kutengwa na jumuiya ya kimataifa na kupoteza hadhi na uaminifu wake kimataifa. Kunyimwa haki wanazuoni, pamoja na kuchukua hatua dhidi ya dini na madhehebu, ni sawa na kuchukua hatua dhidi ya uthabiti na usalama wa jamii za Kiislamu. Upanuzi wowote wa hatua hizi za ukandamizaji utasababisha madhara makubwa ya kisiasa na kijamii kwa utawala wa Bahrain, ambayo hatimaye yatakuwa nje ya uwezo wake wa kuyadhibiti.

Pili: Kufichua nafasi ya maadui wanaochochea mifarakano

Tunazichukulia hatua hizi kuwa ni sehemu ya mipango mibaya na iliyopangwa kwa utaratibu na maadui wa Uislamu na ubinadamu, hususan Marekani na utawala wa Kizayuni. Tawala hizi za kibeberu, kwa kubuni migogoro ya kidini katikati ya nchi za Kiislamu, zinalenga kuzusha mifarakano na kudhoofisha nguvu na mamlaka ya Umma wa Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.). Kwa hiyo, Umma mzima wa Kiislamu, wasomi wake na vituo vyake vya kielimu, vinapaswa kusimama kidete kukabiliana na vitendo vya aina hii vya kueneza ufisadi na kuchochea mifarakano.

Tatu: Kuwatetea wanazuoni wa Uislamu na wananchi wapendwa wa Bahrain

Kuwatetea wasomi, watu wenye upeo mkubwa wa kielimu na wanazuoni mashuhuri wa Bahrain, sambamba na kuwaunga mkono wananchi wake wanaodhulumiwa lakini wenye msimamo imara, ni wajibu wa kila mmoja. Hawza nazo zitatekeleza wajibu wake katika medani hii.

Mwisho

Inasisitizwa kwamba hatutarejea nyuma kwa njia yoyote ile katika kuunga mkono na kutetea haki za wananchi wa Bahrain, vijana wake na wanazuoni wetu wakubwa. Aidha, ufuatiliaji wa suala hili utaendelea kupitia njia zote za kisheria, za kimataifa na kwa kushirikisha mamlaka na taasisi kuu za Kiislamu. Iwapo uadilifu hautasimamishwa katika mahakama zisizotenda haki, basi bila shaka utasimamishwa katika uwanja wa historia na mbele ya Mwenyezi Mungu. Na mataifa yatapata tena haki, uhuru na heshima yao.

Na ushindi hautoki isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Ayatullah Alireza A'rafi
Mkurugenzi wa Hawza Nchini Iran.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha