Jumanne 20 Oktoba 2026 - 09:00
Migawanyiko katika Ulimwengu wa Kiislamu Inatoa Fursa kwa Marekani na Israel Kujinufaisha

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hassan Mousavi, katika taarifa yake, ameonya kuhusu madhara ya mvutano na makabiliano kati ya nchi za Kiislamu huku akisisitiza kuwa; umoja na mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu, pamoja na kutatua tofauti kupitia mazungumzo na diplomasia, ni jambo la msingi kwa ajili ya kulinda maslahi ya pamoja ya Waislamu na kudumisha amani na utulivu katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hassan Mousavi, Mkuu wa Jumuiya ya Kisheria ya Mashia wa Jammu na Kashmir, katika taarifa yake, ameonya kuhusu madhara ya mvutano na makabiliano kati ya nchi za Kiislamu, huku akisisitiza kuwa umoja na mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu, pamoja na kutatua tofauti kupitia mazungumzo na diplomasia, ni jambo la msingi kwa ajili ya kulinda maslahi ya pamoja ya Waislamu na kudumisha amani na utulivu katika eneo hilo.

Amewataka Waislamu duniani kote kujiepusha na migawanyiko na makabiliano ya pande kwa pande, kuimarisha umoja na mshikamano wao, na kufuata njia ya mazungumzo, diplomasia na kuheshimiana kwa ajili ya kutatua migogoro.

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu kutoka Kashmir pia ameonya kuwa; kuongezeka mvutano kati ya nchi za Kiislamu kunazinufaisha nguvu zinazotaka kuendeleza maslahi yao katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa; mvutano na makabiliano yanayoendelea kati ya nchi za Kiislamu na makundi mbalimbali vinadhoofisha nguvu ya pamoja ya Umma wa Kiislamu, na kutoa fursa kwa mataifa yenye nguvu, kama vile Marekani na utawala wa Israel, kutumia migawanyiko iliyopo ili kuendeleza maslahi yao ya kimkakati katika eneo hilo.

Mkuu wa Jumuiya ya Kisheria ya Mashia wa Jammu na Kashmir, huku akizungumzia nafasi tukufu ya Makkah Mukarramah na Madina Munawwarah miongoni mwa Waislamu, amesisitiza kuwa maeneo matakatifu ya Kiislamu yamekuwa daima yakiheshimiwa na Umma wa Kiislamu, hivyo masuala nyeti yanayohusiana na maeneo hayo yanapaswa kushughulikiwa kwa umakini na uwajibikaji.

Ameongeza kuwa, ili kuzuia kuumizwa hisia za kidini na kuongezeka migawanyiko miongoni mwa Waislamu, ni lazima kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa na kutoa kauli za uchochezi kuhusu masuala nyeti ya kidini.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hassan Mousavi pia amewataka viongozi wa nchi za Kiislamu, wanazuoni wa dini na vyombo vya habari kupambana na mivutano ya kimadhehebu na kujiepusha na kuchochea migawanyiko, ili waweze kutekeleza jukumu lenye manufaa katika kuleta amani na utulivu katika eneo hilo.

Amesisitiza kuwa; vita na makabiliano si suluhisho la matatizo; bali mazungumzo, diplomasia na kuheshimiana ndivyo vinavyoweka mazingira ya kufikia amani ya kudumu.

Mwishoni mwa taarifa yake, Rais wa Jumuiya ya Kisharia ya Mashia wa Jammu na Kashmir; amezitaka nchi zote za Kiislamu na mataifa ya Kiislamu kuvuka mipaka ya tofauti zao, kuimarisha umoja na mshikamano wao, na kufanya juhudi za dhati na zilizoratibiwa kwa ajili ya kulinda maslahi ya pamoja ya ulimwengu wa Kiislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha