Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, ametoa ujumbe kufuatia marufuku ya kuvaa hijabu katika taasisi za elimu nchini Jamhuri ya Azerbaijan.
Maandishi kamili ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Suala la hijabu na mavazi, hususan mavazi ya wanawake waheshimiwa, limekuwa likizingatiwa katika dini tukufu ya Uislamu, mtindo wa maisha na mila halisi za Kiislamu kuwa ni wajibu wa kisheria na wa Kiislamu katika kipindi chote cha historia. Kimsingi, wajibu wa kisheria wa Kiislamu hauwezi kubatilishwa kwa waraka wa kiutawala, sheria zilizowekwa na wanadamu au kanuni za mamlaka za serikali, wala ulazima wa kutekeleza wajibu huo hauondoki kwa Waislamu.
Zaidi ya hayo, katika mfumo wa itikadi wa madhehebu ya Uislamu, hijabu ni dhihirisho la imani, kujisitiri na utambulisho wa kidini wa mwanamke Mwislamu. Pia, inachukuliwa kuwa ni jambo linalotokana na imani na uchaguzi wa wanawake waumini uliofanywa kwa ufahamu na utashi wao. Hakuna nchi yoyote ya Kiislamu yenye haki ya kuwanyang’anya wanawake na wasichana katika jamii yake haki hii ya kisheria ya Kiislamu, wala kuwanyima haki zao, kama vile kupata elimu, kufundisha na kushiriki katika nyanja za kielimu na kijamii, kwa namna inayokiuka haki za kibinadamu na utu wa mwanadamu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya ya 31 ya Suratul Nur:
وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ...
“Na waambie wanawake Waumini wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayoonekana, na waangushe vifuniko vyao vya vichwa juu ya vifua vyao...”
Kwa mujibu wa Aya hii tukufu, wanawake wanapaswa kufunika vichwa vyao na shingo zao mbele ya wanaume ambao si maharimu wao, na kuzingatia hijabu ya Kiislamu. Hakuna mtu anayeweza kubatilisha hukumu iliyo wazi ya Qur’ani Tukufu kwa kutumia waraka wa kiutawala au sheria zilizowekwa na wanadamu.
Suala la hijabu nchini Jamhuri ya Azerbaijan, ambako hivi karibuni mamlaka za serikali na baadhi ya taasisi za nchi hiyo zimeweka vikwazo vinavyowahusu walimu waheshimiwa na wanafunzi wapendwa, liko katika hali hiyo hiyo, hasa kwa kuzingatia kwamba wananchi wengi wa nchi hiyo ni Waislamu.
Kwa hiyo, inatarajiwa kwamba viongozi na maafisa waheshimiwa wa nchi hiyo watazingatia matakwa ya kidini ya wananchi, hususan wanafunzi wa kike na walimu wanawake wa nchi hiyo ya Kiislamu yenye watu wanaoshikamana na dini yao. Matakwa hayo yanatokana na Qur’ani Tukufu na mafundisho ya madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.). Aidha, wanapaswa kuhakikisha kwamba hawaruhusu ushikamanifu wa wananchi Waislamu kwa dini yao na matakwa yao ya kidini kuathiriwa au kudhoofishwa.
Ayatullah Alireza A‘rafi
Mkurugenzi wa Hawza nchi Iran.
Maoni yako