Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Abdullah Jabri, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ummah nchini Lebanon, katika taarifa yake amelaani hatua na mienendo inayolenga hijabu ya Kiislamu nchini Jamhuri ya Azerbaijan, ambayo inaambatana na kuweka vikwazo dhidi ya uhuru wa wanawake Waislamu wa kushikamana na mavazi yao ya kidini.
Alibainisha kuwa kila uamuzi unaozuia uvaaji wa hijabu au kuweka vikwazo vya kiholela dhidi yake ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa imani na haki za msingi za binadamu.
Alisisitiza kwamba hijabu si kipande tu cha kitambaa, bali ni alama ya kidini na ishara ya utambulisho wa Kiislamu. Alieleza kuwa kuheshimu uhuru wa mwanamke kunahitaji kulinda haki yake ya kuvaa hijabu, badala ya kumlazimisha kuivua kwa kisingizio cha “usasa”, usekula au kuweka utaratibu katika maisha ya umma.
Sheikh Jabri alieleza kushangazwa kwake na kuona nchi yenye Waislamu walio wengi, kama Azerbaijan, ikishuhudia vitendo vinavyoweka shinikizo dhidi ya alama za kidini, huku kauli mbiu zinazodai kuheshimiwa kwa wingi wa mitazamo na uhuru wa mtu binafsi zikiendelea kutolewa.
Alihoji: “Inawezekanaje kuzungumzia uhuru wa mwanamke wakati mwanamke huyo anawekewa shinikizo kwa sababu ya kushikamana kwake na dini? Na haki za binadamu ziko wapi pale hijabu inapogeuzwa kuwa sababu ya ubaguzi au kunyimwa fursa ya kupata elimu na ajira?”
Kwa maoni ya Sheikh Jabri, kulenga alama za Kiislamu hakuchangii kuimarisha mshikamano wa kijamii. Badala yake, kunafungua njia ya kuibuka migawanyiko na kuzidisha hisia za kudhulumiwa na kutengwa katika jamii.
Aidha, alisisitiza kwamba nguvu ya serikali haipimwi kwa namna inavyopambana na alama za kidini, bali hupimwa kwa uwezo wake wa kulinda utu wa wananchi na kuheshimu imani zao.
Sheikh Jabri alizitaka mamlaka za Azerbaijan kupitia upya hatua zozote zinazoweka vikwazo dhidi ya uvaaji wa hijabu, na kuhakikisha uhuru wa kutekeleza ibada na desturi za kidini unalindwa bila kutumia mabavu wala ubaguzi.
Vilevile, alizitaka taasisi za Kiislamu na mashirika ya haki za binadamu kutetea uhuru huo kwa kutumia njia za amani na taratibu za kisheria.
Katika hitimisho la taarifa yake, Sheikh Jabri alisisitiza kwamba uhuru wa mwanamke haupatikani kwa kumvua hijabu kwa nguvu, bali hupatikana kwa kuheshimu utashi wake, utu wake na haki yake ya kufanya uchaguzi.
Maoni yako