Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Al-Khatib, Naibu Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon, ameashiria mwaliko wa Rais wa Lebanon wa kuandaa mazungumzo mapana ya kitaifa yatakayoweka mtazamo wa kitaifa kuhusu mustakabali wa nchi, pamoja na kuachana na sera ya kutumia njia moja pekee ya mazungumzo ya moja kwa moja, ambayo katika awamu saba zilizopita haikuzaa matokeo yoyote.
Alipitia hali ya Lebanon na eneo la Mashariki ya Kati, na kusema: “Eneo lote bado linaendelea kuchemka juu ya moto mkali; kuanzia Lebanon hadi Mlango-Bahari wa Hormuz, Yemen, Syria na Palestina, huku kukiwa na ongezeko la mvutano wa kisiasa na kijeshi na hofu kwamba wigo wa vita unaweza kupanuka. Haya ni matokeo ya miradi ya Marekani na Uzayuni ambayo yameligeuza eneo hili kuwa volkano ya migogoro, pengine kile kinachotokea katika medani ya Yemen ni mfano hai wa ukweli huu.”
Naibu Mwenyekiti huyo wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia aliongeza: “Jambo lililo wazi hadi sasa ni kwamba matarajio ya kufikiwa suluhisho hayapatikani kutokana na ukaidi unaooneshwa na Marekani na utawala wa Kizayuni, lugha ya mazungumzo imesitishwa huku ikisubiriwa matokeo ya uchaguzi wa Marekani na Israel ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili ijayo, wengi wanaweka matumaini yao katika jambo hili, kwa sababu mazungumzo wakati wa uchaguzi hugeuka kuwa mazungumzo ya watu wasioweza kusikilizana, kiasi kwamba mambo yanaonekana kufikia mkwamo, kwa mujibu wa wachambuzi na wataalamu, baada ya uchaguzi inatarajiwa kwamba hali itakuwa wazi zaidi; ima uwanja utalipuka kwa kiwango kikubwa, au makubaliano yatafikiwa yatakayopelekea kwa namna fulani kwenye suluhisho lenye uwiano.”
Sheikh Al-Khatib aliendelea kusema: “Wakati Rais wa Marekani akitegemea uchaguzi huu na kutoa ahadi kwamba suluhisho litapatikana baada ya uchaguzi, baadhi ya watu hata miongoni mwa timu yake ya kazi wana wasiwasi kwamba mvutano utaendelea hadi mwisho wa kipindi chake cha urais. Hili linaonesha kwamba serikali ya Marekani inaendelea kusukuma mbele mipango na matukio yake ya hatari kwa lengo la kuilazimisha eneo lote kusalimu amri, huku mradi wa upanuzi wa Kizayuni, ambao viongozi wa adui wanaueleza waziwazi na kwa jeuri, ukiwa si jambo lililofichika tena kwa mtu yeyote.”
Aliongeza kusema: “Katika mazingira ya ukweli huu, sisi nchini Lebanon si kisiwa kilichojitenga na matukio yanayoendelea katika eneo hili, hata kama baadhi ya watu wanajaribu mara kwa mara kuhusisha mambo na mipangilio ya ndani bila kuwepo dhamana yoyote inayoweza kuwapa wananchi uhakika kuhusu mustakabali wao. Wanataka kuunyang’anya Muqawama silaha ili kufungua njia kwa ajili ya suluhisho, wakati viongozi wa adui wanasisitiza kwamba hawataondoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kusini mwa Lebanon. Jambo hili linapingana na mantiki ya kawaida ya mambo, muqawama ulizaliwa kutokana na ukaliaji wa ardhi, wala si kinyume chake, wakati ukaliaji wa ardhi utakapoondolewa, ndipo inaweza kujadiliwa hatima ya Muqawama kupitia mkakati wa kitaifa wa ulinzi ambao viongozi wa Lebanon, na hasa Rais wa nchi, wameutaka.”
Sheikh Ali Al-Khatib alisisitiza: “Kunyang’anywa silaha wakati kuna ukaliaji wa ardhi si jambo linalowezekana wala la kawaida, hili ndilo jambo ambalo tumewaeleza wote wanaofanya mashauriano katika suala hili, na huu ndio msimamo ambao sote tumejifunga nao, tukiwa na msimamo mmoja na ulioungana. Kwa wale wanaoujali na wale wasioujali msimamo wa kitaifa wa Mashia, tunasema kwamba msimamo wa Mashia, katika sehemu zake zote na kuhusiana na masuala yote yanayoendelea sasa, ni mmoja na ulioungana.
Baadhi ya dosari ndogo ambazo daima hujaribu kuzitumia kama fursa ya kupotosha ukweli huu hazitaathiri msimamo huo.”
Aidha, alisema: “Tumesema na tunarudia tena mwaliko wa Rais wa kuachana na sera ya kutumia njia moja pekee ya mazungumzo ya moja kwa moja, ambayo katika awamu saba haikuzaa matokeo yoyote; wakati Israel inatumia damu yetu, kulipuliwa kwa nyumba na taasisi zetu kama karatasi ya uchaguzi, na kuwahamisha wapendwa wetu kutoka katika ardhi, miji na vijiji vyao. Mlipuko mkubwa uliotokea katika eneo la Ali Al-Taher usiku uliopita ulikuwa mfano mkubwa zaidi wa ukatili wa Kizayuni na nia zake za uchokozi.”
Aliongeza: “Wiki iliyopita tuliwasilisha ukweli huu kwa uwazi kabisa kwa ndugu zetu nchini Iraq na ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika ngazi za juu kabisa za kisiasa na kidini, na tukawaambia kwamba tunapozungumza nanyi kwa uwazi namna hii, kwa hakika tunazungumza na nafsi zetu. Kuna zaidi ya familia 40,000 zilizohama makazi yao ambazo zinahitaji kwa dharura matunzo na makazi hadi zitakaporejea katika maeneo na vijiji vyao, na sisi sote tunawajibika kuzihudumia. Tumekutana na majibu chanya, na tunatumaini kwamba majibu hayo yatatekelezwa katika siku za usoni.”
Sheikh Al-Khatib alimalizia kwa kusema: “Kwa mara nyingine tena, tunarudia na kusisitiza mbele ya kila mtu kwamba, sisi ni miongoni mwa wale wanaoshikamana zaidi na serikali inayowalinda wananchi wake na kulinda mamlaka yake. Sisi ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa kupelekwa jeshi la kitaifa la Lebanon katika maeneo yote ya ardhi ya Lebanon na kufikiwa usalama utakaowapa wananchi wetu katika maeneo yao hali ya kujiamini na utulivu. Mtu yeyote anayefikiri kwamba tunatamani kuwa na dola ndani ya dola, au kwamba tunaota mradi wa kujitenga, yuko katika dhana potofu, hatujawahi kuwa hivyo hapo zamani, wala hatutakuwa hivyo katika siku zijazo, tunataka tu ushirikiano wa kitaifa wenye haki, ambao utaleta heshima na uadilifu kwa wananchi wetu.
“Endapo serikali ingewekeza katika mipaka yake ya kusini hapo zamani, tusingefikia nafasi tuliyofikia leo, na tungekuwa tumehifadhi kwa ajili ya wananchi wetu na vijana wetu damu hizi safi na zisizo na hatia, ambazo zimemwagika kwa ajili ya nchi nzima pekee.”
Maoni yako