Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Wizara ya Sheria, Mambo ya Kiislamu na Wakfu imetangaza kuendeleza taratibu za kusimamia utoaji wa vibali vya uhubiri na uongofu wa kidini; hatua ambayo imedaiwa kuwa inalenga kuimarisha mifumo ya usimamizi wa shughuli za kidini.
Wizara hiyo, katika taarifa iliyochapishwa kupitia Shirika rasmi la Habari la Bahrain “BNA”, imetangaza: Uamuzi huo unasisitiza jukumu lililowekwa juu ya maafisa wanaohusika na suala hili, na utazuia matumizi ya sehemu za ibada na Husainiya katika shughuli zinazokwenda kinyume na sheria; kwa mujibu wa madai ya wizara hiyo, kwa sababu imebainika kuwa kuna ukiukwaji mwingi na matumizi ya maeneo hayo kinyume na malengo na dhamira zake.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, kamati maalumu zitaanzishwa katika idara za umma zenye mamlaka husika, na zitawajibika kuweka vigezo na masharti ya utoaji wa vibali kwa ajili ya shughuli za uhubiri na uongofu wa kidini katika sehemu za ibada, Husainiya na maeneo mengine, pamoja na kubainisha nyaraka zinazohitajika ili kupata kibali.
Wizara hiyo imedai: Mkusanyiko wa masharti umewekwa kwa ajili ya wenye vibali, ambao wanapaswa kuyafuata. Masharti muhimu zaidi ni kushikamana na maamuzi, maelekezo na kanuni zinazosimamia shughuli za kidini; kuzingatia kanuni na adabu zinazotumika katika mawasiliano ya kidini; kuhifadhi nafasi ya sehemu za ibada, Husainiya na maeneo mengine pamoja na yaliyomo ndani yake; na kutotumia au kuruhusu kutumika maeneo hayo kwa madhumuni yasiyo yale yaliyotengewa.
Uamuzi huo umetolewa na Waziri wa Sheria, Mambo ya Kiislamu na Wakfu, na unasimamia shughuli za uhubiri na uongofu wa kidini, utoaji wa hotuba za kidini na shughuli zinazohusiana nazo; huku kupata kibali cha awali kwa ajili ya kutekeleza shughuli hizo kukiwa ni jambo la lazima.
Inapaswa kuzingatiwa kwamba hatua hii inachukuliwa katika mfumo wa kuwalenga Mashia na kubana zaidi nafasi ya kutekeleza ibada na alama zao za kidini, baada ya kukamatwa maulama wakubwa na kuzuiwa baadhi ya wahutubu na waimbaji wa maombolezo ya kidini kushiriki katika shughuli za umma; wakati huo huo ambapo mamlaka za Bahrain zinadai kuheshimu dini na kuvumilia tofauti za kidini, licha ya hatua hii ambayo inaweza kuwachochea Mashia wengi.
Maoni yako