Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Ofisi ya Baraza Kuu la Wakfu na Uongozi wa Kidini, Kitengo cha Utamaduni na Kitengo cha Wanazuoni cha Mkoa wa Sa’dah nchini Yemen, leo wameandaa mkutano uliowahusisha wanazuoni, makhatibu na wahubiri kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (saww) na kulaani dharau ya Marekani dhidi ya Qur’ani Tukufu.
Katika mkutano huo, Sheikh Ahmad Huriya, Mwenyekiti wa “Jumuiya ya Kiislamu” na mwanachama wa “Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen”, alisisitiza: Maadhimisho ya Maulid ya Mtume Mtukufu (saww) ni kituo cha kuimarisha nyanja za kiimani na kiutendaji, hususan katika uwanja wa jihadi, subira na ustahimilivu.
Akisifu msimamo wa wananchi wa Yemen katika kukabiliana na adui wa Saudi Arabia, Israel na Marekani, alirejelea mapambano ambayo mashujaa wa vikosi vya kijeshi wameyapitia na wanayoendelea kuyafanya baharini dhidi ya maadui, na kuongeza: Miungano iliyokuwa imelenga kuishambulia Yemen imeporomoka kwa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na pande mpya zilizojiunga nayo pia zimeshindwa.
Sheikh Huriya alibainisha: Siri ya nguvu ya Wayemeni haiko katika wingi wao wa idadi wala silaha, bali iko katika kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuwa na imani naye, na wakati huohuo kutumia nyenzo zilizopo na kuwa tayari.
Alifafanua: Kushikamana na Qur’ani Tukufu, Mtume Muhammad (saww) na viongozi wa uongofu ni ufunguo wa uthabiti na ushindi, na lengo kuu la kuadhimisha matukio ya kidini ni kutafsiri dhana hizi katika matendo na mwenendo.
Katika muktadha huo, Sheikh Muhammad al-Hadi, mwanachama wa “Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen”, alisisitiza: Mashambulizi ya Marekani na Wazayuni dhidi ya Qur'an Tukufu ni jinai kubwa inayohitaji msimamo thabiti na mwitikio wenye nguvu kutoka kwa kila mtu aliye na uhusiano na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Alifafanua kuws: Dharau zinazofanywa na maadui wa Mwenyezi Mungu dhidi ya matukufu ya Umma zinathibitisha umuhimu wa kukabiliana na mradi wa Kizayuni na Marekani na kushikamana na kaulimbiu “Kifo kwa Marekani, Kifo kwa Israel” dhidi yao.
Al-Hadi alibainisha: Tawala za Magharibi na Wazayuni zinajitahidi kwa nguvu kukata uhusiano wa Umma na Mtume Mtukufu (saww) na Qur’ani Tukufu, ili kuwanyima chanzo cha nguvu na heshima yao.
Sheikh Al-Hadi aliwaalika wote, hususan wanazuoni, kutekeleza majukumu yao ya kuuongoza Umma na kuulea kwa msingi wa kumfuata Mtume Mtukufu (saww) kama kiongozi, mwalimu, mwanasiasa na mlezi; kwa namna itakayouwezesha Umma kukabiliana na hatari zinazoukabili.
Aliwahimiza wote kutafuta suluhisho na mikakati inayohitajika katika Sira ya Mtume na misimamo ya Qur’ani kwa ajili ya kukabiliana na mzingiro, dhuluma na njama ambazo Umma unakabiliana nazo leo, na kutumia maadhimisho ya Maulid ya Mtume Muhammad (saww) kama kituo cha kiutendaji cha kurejea kwa unyofu katika mwenendo wa Qur’ani na Mtume.
Maoni yako