Jumamosi 18 Julai 2026 - 15:50
Ripoti Yaibua Hofu: Wanazuoni wa Kishia Bahrain Wadaiwa Kudhalilishwa na Kulazimishwa Kukiri Makosa ya Uongo

Hawza/ Jumuiya ya Al-Wefaq Al-Watani Al-Islamiyyah imefichua kuwa imepata "taarifa hatari na sahihi" kuhusu mazingira ya kuwazuia wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Al-Wefaq Al-Watani Al-Islamiyyah, imetangaza kuwa imepata "taarifa hatari na sahihi" kuhusu hali ya kuwashikilia wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain, na imewashutumu viongozi wa nchi hiyo kwa kutekeleza ukiukwaji wa haki za binadamu ambao imeuelezea kuwa ni "uhalifu wa kutisha" unaofanyika katika vituo vya siri vya mahabusu.

Jumuiya ya Al-Wefaq Al-Islamiyyah ilisisitiza kuwa; hatua hizi ni sehemu ya kampeni iliyopangwa ya kulenga dhehebu fulani. Katika taarifa yake, jumuiya hiyo ilisema kuwa taarifa walizozipata zinaonesha kwamba maagizo yametolewa kutoka ngazi za juu za serikali yakilenga kuwavunjia heshima wanazuoni waliofungwa gerezani na kuwadhalilisha kupitia vipigo, matusi, kuwatemea mate na kuwatishia kuwafanyia unyanyasaji wa kingono. Mashinikizo hayo yanafanywa kwa lengo la kuwalazimisha kutia saini maungamo ya "uongo na ya kutungwa."

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa; idadi ya wanazuoni na wakuu wa vyuo vya elimu ya dini (Hawza) wamepigwa na maafisa wa vituo vya mahabusu. Hatua hizi zinafanyika katika utekelezaji wa maagizo yanayolenga kuwafanya wasalimu amri kwa kuwazidishia udhalilishaji na kuwafanyia vitendo vya ukatili, jambo ambalo Jumuiya ya Al-Wefaq imelielezea kuwa ni ukiukaji mkubwa wa heshima ya utu wa binadamu.

Jumuiya ya Al-Wefaq ilieleza kuwa; ukiukaji huu wa haki haujaishia kwenye ukatili wa kimwili pekee, bali umefikia pia kutukana imani za kidini. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, yametolewa maagizo ya kuyatukana Madhehebu ya Ja'fari, kubeza itikadi na alama za Kishia, kuwatusi Ahlul-Bayt (as), kutukana nembo na ibada za dini, Maimamu, wanazuoni, matukufu ya dini pamoja na hukumu za Fiqhi. Hali hii inaonesha kuongezeka kwa kiwango kisicho na mfano cha kulenga dhehebu fulani.

Katika taarifa hiyo, baada ya kuorodhesha vitendo mbalimbali vilivyopewa jina la "mateso na udhalilishaji", ilitaja mifano kama kuwafunga mikono wanazuoni waliofungwa nyuma ya migongo yao kwa muda mrefu, kuwafunika nyuso zao kikamilifu kuanzia asubuhi hadi jioni, kuwanyima dawa na mapumziko pamoja na kuwatemea mate usoni. Aidha, ilisisitiza kuwa kuna ukiukaji mwingine wa haki ulio "hatari zaidi" ambao Jumuiya ya Al-Wefaq imeamua kutoufichua kwa sasa kwa ajili ya kulinda heshima ya wanazuoni hao waliowekwa kizuizini.

Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wefaq ilimtaja Mfalme wa Bahrain na Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuwa wanawajibika kikamilifu katika ukiukaji huu wa haki. Aidha, imeeleza kuwa kinachoendelea ni "ugaidi wa kimadhehebu" na "vita vilivyopangwa dhidi ya Madhehebu ya Ja'fari", ambavyo vinayalenga makumi ya wanazuoni wa Kishia.

Jumuiya hiyo imeutaka Umoja wa Mataifa, taasisi za kimataifa na za haki za binadamu, serikali mbalimbali, mabunge pamoja na taasisi za kidini na kijamii kuingilia kati mara moja ili kusitisha kile ilichokiita "vita vya kimadhehebu", kufanya uchunguzi kuhusu ukiukaji huu wa haki, kuwalinda waliowekwa kizuizini na kuwafikisha mbele ya sheria wale wanaohusika.

Inafaa kutajwa kuwa mamlaka za Bahrain zimeanzisha kampeni isiyo na mfano ya kuwakamata wanazuoni wa Kishia, ambapo katika hatua mbili tofauti zaidi ya wanazuoni 50 wa dini wamekamatwa. Mamlaka za Bahrain zinawashutumu watu hao kwa kueneza kile wanachokiita "fikra ya Wilayatul Faqih", huku zikiwa hazijawasilisha ushahidi wowote wa msingi kuthibitisha madai hayo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha