Jumapili 5 Julai 2026 - 12:53
Misingi Imara ya Imam Khamenei Haikuwahi Kubadilika

Hawza/ Rais wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Muqawama ameelezea kumbukumbu za mikutano na mawasiliano yake kwa njia ya barua na Imam Khamenei, akisimulia hatua mbalimbali zilizowaunganisha katika safari yao ya pamoja.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Ulimwengu wa Kiislamu na watu wengi huru duniani wanajiandaa kumuaga Ayatullah al-Udhma, Imam Shahidi Sayyid Ali Khamenei; mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi waliounganisha kwa ustadi undani wa dini, uzoefu wa kisiasa na roho ya Muqawama. Katika maisha yake yote, jina lake lilihusishwa na utetezi wa misingi halisi ya Uislamu, kuunga mkono malengo ya wanyonge na waliodhulumiwa, pamoja na juhudi za kuimarisha dhana za umoja na heshima katika Umma wa Kiislamu. Wengi wanakumbuka misimamo yake iliyodhihirisha uwazi wake kwenye mikondo mbalimbali ya fikra, madhehebu, makundi na dini tofauti.

Rais wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Muqawama, Sheikh Maher Hamoud, alipokuwa akikumbuka mikutano na mawasiliano yake kwa njia ya barua, alisimulia hatua mbalimbali zilizomunganisha na Imam Khamenei. Alisema kuwa; uhusiano huo ulianza mwaka 1981 (1359 Hijria Shamsia), wakati ambapo Imam Khamenei alikuwa Rais wa chama cha Jamhuri ya Kiislamu na Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Tehran, kabla hajawa Rais wa Jamhuri na baadaye Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Sheikh Hamoud alisema kuhusu mkutano huo: “Ulichukua takribani saa tatu, ukiwahusisha wajumbe wachache wa Kipalestina. Tulijadili miungano ya Mapinduzi, mtazamo wake kuhusu maadui, pamoja na misingi iliyokuwa ikiiongoza tabia ya Mapinduzi kabla na baada ya ushindi wake.” Alisisitiza kuwa mambo yote yaliyosemwa katika mkutano huo yalibaki thabiti na hayakubadilika kwa kipindi chote cha miaka arobaini na saba.

Aidha, Sheikh Hamoud aliitaja mikutano mingine iliyofanyika mwaka 1982 (1360 Hijria Shamsia) baada ya Imam Khamenei kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri, na mkutano mwingine mwaka 1989 (1367 Hijria Shamsia) baada ya kuchaguliwa kuwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambao aliuelezea kuwa ulikuwa mkutano wao wa mwisho.

Msimamo wa Kudumu wa Sayyid

Sheikh Hamoud alisisitiza kwamba; maudhui ya maneno aliyoyasikia kutoka kwa Imam Khamenei mwaka 1981 yalibaki yale yale hadi wakati wa shahada yake. Alisema jambo hilo linaonesha uwazi wa maono yake na uthabiti wake katika kushikamana na misingi.

Aliongeza kuwa; kushikamana huko na misingi, ambako kulitawala mwenendo wa Mapinduzi ya Kiislamu na wa Kiongozi wake, kunastahili kuheshimiwa na Waislamu wote, hata watu wote huru duniani. Hata hivyo, njama za Marekani zilijaribu kuharibu taswira hiyo kwa kuibua tofauti za kimadhehebu na kikabila na kwa kueneza hofu kwamba Mapinduzi yalikuwa na ajenda ya “upanukaji wa ushawishi” au “mradi wa Kifarsi.”

Alisisitiza kuwa; Imam Khamenei alidumu katika msimamo wake usiobadilika, fikra zake zilizo wazi, na ikhlasi yake kwa Mapinduzi na kwa wananchi, kwa namna ambayo hakuna mtu mwenye uadilifu anayeweza kuwa na shaka nayo. Alimtaja kuwa alikuwa kiongozi mwenye kuhamasisha, ambaye matendo yake, ustahimilivu wake, na juhudi za maadui kumlenga, vyote vinathibitisha nafasi yake hiyo.

Mawasiliano Endelevu na Kiongozi Shahidi

Sheikh Hamoud alisema kuwa; mawasiliano yao kwa njia ya barua yaliendelea kwa muda mrefu, na mara kwa mara alikuwa akimtumia Imam Khamenei maoni yake kuhusu masuala mbalimbali.

Alikumbusha tukio la filamu ya Majid Majidi kuhusu utoto wa Mtume Muhammad (saww), ambayo ilioneshwa mjini Beirut mwaka 2015 (1393 Hijria Shamsia). Baada ya kuona ndani ya filamu hiyo makosa ya wazi ya kisheria (kifiqhi), alimtumia Imam Khamenei barua, na baada ya hapo maonesho ya filamu hiyo yakasitishwa.

Pia alitaja barua mbalimbali zilizohusiana na mialiko ya kushiriki makongamano, na kusema kwamba; hivi karibuni alipokea barua kutoka kwa Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei, iliyokuwa na shukrani kwa barua aliyokuwa amemtumia.

Barua kutoka kwa Imam Khamenei

Sheikh Hamoud alizungumzia barua aliyopokea kutoka kwa Imam Khamenei, ambapo alimhimiza kuendelea na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni. Kwa mujibu wa barua hiyo, mapambano hayo yana sura nyingi, zikiwemo mapambano ya kijeshi, ya vyombo vya habari, ya kitamaduni na ya kielimu.

Mazungumzo ya Kudumu ya Kiongozi Shahidi na Wanazuoni wa Ahlus-Sunnah

Sheikh Hamoud alieleza pia uwazi wa Imam Khamenei na heshima aliyokuwa akiionesha kwa dini na madhehebu mbalimbali. Alisema kwamba: Imam Khamenei alikuwa na shauku kubwa ya kukutana na kufanya mazungumzo.

Aliongeza kuwa kitabu “Muhammad”, kilichosambazwa kwa upana, kinaakisi fikra zake za kuhimiza umoja. Aidha alisema kuwa wanazuoni wa Ahlus-Sunnah kutoka Baluchistan, Kurdistan na Saudi Arabia walikuwa wakifanya mazungumzo naye mara kwa mara, na daima alikuwa akiwapokea na kuwaheshimu.

Alifikia Kile Alichokuwa Akikitamani

Kwa mujibu wa Sheikh Hamoud, Imam Khamenei, ambaye alikuwa na takribani miaka 87, aliutumia maisha yake yote katika njia ya haki.

Alisema: “Imam alikuwa akijirudia mara kwa mara akisema: ‘Waisraeli wanataka nini kutoka kwangu? Wanataka kuniua, mimi si ndiye ninayeiongoza nchi; wanaoiendesha nchi ni vijana. Hivyo basi, ikiwa Mwenyezi Mungu atauhitimisha uhai wangu kwa shahada, hilo ni jambo kubwa, na ndilo ninalolitamani.’”

Mwishoni, Sheikh Hamoud alisema: “Imam alipata kile alichokuwa akikitamani, maisha yake, yaliyokuwa yamejaa kujitolea na utoaji kwa kiwango cha juu kabisa, yalihitimishwa kwa shahada.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha